Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Rais Magufuli amfuta kazi mtumishi wa serikali aliyechana kitabu kitakatifu cha Kurani
Rais wa Tanzania, John Magufuli ametangaza kumfukuza kazi mtumishi wa serikali aliyechana kitabu kitakatifu cha Kurani kisha picha yake kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha akitekeleza kitendo hicho.
Kauli hiyo ameitoa alipokuwa kwenye hafla ya uzinduzi wa ofisi za wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam
Juzi nilikuwa namsikia mheshimiwa Jafo , mtu mmoja kule Kilosa nafikiri alichana kitabu kitakatifu, nakushukuru umechukua hatua ya kumsimamisha kazi lakini mimi ninamfukuza moja kwa moja muandikie barua ya kuondoka moja kwa moja, ashinde kesi asishinde huyo si mfanyakazi wa serikali hatuwezi kukaa na wafanyakazi wapumbavu katika serikali hii''.
Juma lililopita Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo aliagiza kusimamishwa kazi kwa mtumishi wa Halmashauri ya Kilosa mkoani Morogoro Daniel Elimringi, kwa kosa la kuchana kitabu cha dini ya Kiislamu, Kurani.
"Jambo hili lililofanywa na mtumishi huyu halileti kabisa afya kwa taifa letu kwani watu wake wa dini zote wamekuwa wakiishi katika mazingira ya amani na kuheshimia kwa kila mtu," alisema Jafo.
Kauli hiyo ya Jafo, inakuja baada ya kusambaa kwa picha katika mitandao mbalimbali ya kijamii zikimuonyesha mtumishi huyo katika Halmsahauri ya Kilosa kitengo cha biashara idara ya fedha akichana na kutupa kitabu cha Kurani.
Gazeti la Mtanzania linaripoti kuwa tayari mtumishi huyo amefikishwa mahakamani na amenyimwa dhamana.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kesi hiyo itatajwa tena Februari 20 mwaka huu.