Virusi vya corona: Baadhi ya mataifa yameanza kuondoa raia wake China

"Mke wangu anajaribu kuridhia sisi tuondoke lakini kwakweli ana wasiwasi ."
Virusi vya corona ambavyo vimesababisha maambukizi zaidi ya watu 7,711 na wengine 170 wamefariki nchini China,vivyo hivyo familia zinalazimishwa kutengana kutokana na mlipuko huo.
Mtaalamu wa teknolojia ya komputa ambaye ni raia wa Uingereza amejikuta anapaswa kufanya maamuzi magumu ya kumuacha mke wake ili asafiri na binti yao Jasmine mwenye umri wa miaka 9,kurejea nyumbani kwao.
Hali ya wageni ikoje China
Siddle na mke wake Sindy, ambaye ni raia wa China walikuwa wamesafiri na binti yao katika jimbo la Hubei ili kusheherekea mwaka mpya wa China pamoja na ndugu zake.
Hubei ni eneo ambalo watu zaidi ya 3,500 wamethibitishwa kuwa na ugonjwa huo, haswa katika mji wa Wuhan, eneo ambalo mlipuko wa ugonjwa huo ulianzia.
Jimbo hilo lina makazi ya raia wa kigeni elfu kumi ambao wafanyakazi na wanafunzi.
Mataifa mengi yametangaza mipango ya kuwaondoa raia wake katika eneo hilo.
Marekani na Japani tayari wamewaondoa mamia ya raia wake.

Chanzo cha picha, Reuters
Siddle anatarajiwa kusafiri Februari 1, lakini ndege zote za Wuhan zimefungiwa kutoka na serikali imefunga uwanja wa ndege na usafiri wote wa Umma pamoja na barabara kufungwa ikiwa ni jitihada ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.
Waliambiwa na mamlaka ya Uingereza kuwa Sindy, hawezi kuondoka licha ya kuwa na viza ya kudumu ya Uingereza tangu mwaka 2008, kwa sababu ndege hiyo ni maalum kwa ajili ya kuwaokoa raia wa Uingereza katika mji huo .
Ndege hiyo inaweza kuwasili mapema siku ya alhamisi.
"Ofisi ya mambo ya nje imetuambia kuwa ndege hiyo ni kwa ajili ya raia wa Uingereza peke yake kwa sababu mamlaka ya China inakataza raia wake kuondoka nchini humo,"Siddle aliiambia BBC.
"Ilinibidi nifanye maamuzi ya kuondoka na binti yangu ambaye ana hati ya kusafiria ya Uingereza au tubaki wote watatu."
China ni miongoni mwa nchi ambazo haitambui uraia wa nchi mbili.
Unaweza pia kusoma
'Ni majonzi makubwa'
Familia ya Siddle iliamua kuchagua kutengana, uamuzi ambao unasababisha masikitiko makubwa sana.
"Yalikuwa ni maamuzi magumu sana na yanayoumiza," Jeff Siddle alisema.
"Kumtenganisha binti wa miaka tisa na mama yake, na hakuna anayejua itachukua muda gani?"
"Binti yangu amelia sana, yani anashindwa kuelewa na amekuwa na majonzi makubwa. "

Chanzo cha picha, Getty Images
Hali ikawa mbaya zaidi ,wakati Siddle alipotaarifiwa na mamlaka ya Uingereza kuwa yeye na binti yake wanapaswa kutafuta namna ya kufika katika uwanja wa ndege wa Wuhan wenyewe ili waweze kuondoka.
"Inachukua saa tatu kuendesha gari mpaka uwanja wa ndege lakini barabara zote zimefungwa, huwezi tu ukaendesha gari," Siddle alisema. "Tulipiga simu mamlaka ya China na kuwaambia kuwa tunahitaji kupata kibali maalum cha diplomasia ili kuturuhusu kupata gari ya kutupeleka."
"Ofisi ya mambo ya nje ilisema kuwa hatuko kwenye nafasi ya kufanya hivyo," Siddle aliongeza.
BBC iliwasiliana na ofisi ya mambo ya nje, na kueleza kuwa wameshataarifu suala hilo kwa mamlaka ya China.
Lakini kwa sasa, Siddle na familia nyingine zenye raia wa China wanapaswa kufanya maamuzi magumu.












