'Hatuhitaji usaidizi wa Uganda kukabiliana na ufisadi Zimbabwe'

Chanzo cha picha, Getty Images
Raia wa Zimbabwe waandamana baada ya jaji mkuu nchini humo kumualika jaji wa Uganda kutoa mafunzo kwa mahakimu wa Zimbabwe kuhusu jinsi ya kukabiliana na ufisadi.
Taarifa hizo hazikupokelewa vizuri na raia wa Zimbabwe katika mitandao ya kijamii ambao wamesema kwamba Uganda sio nchi sahihi ya kujifunza kutoka kwake.
"Tafadhali muache kuharibu raslimali za wananchi. Je tunahitaji usaidizi wa Uganda kukabiliana na ufisadi nchini Zimbabwe" Leonard Koni ameandika.
"Uganda, kukabiliana na ufisadi... Mulifanikiwa vipi kuchanganya maneno hayo mawili NICK? Kwanza tazama nchi ambayo munaiomba ushauri na usaidizi," TB Mandlazi ameandika.
"Uganda sio mfano mzuri kwa nchi zenye kukabiliana na ufisadi pengine Rwanda, Singapore, Netherlands, Malaysia na kadhalika wala siyo Museveni.
Bado tuko mbali sana katika suala la kuanza kupiga vita ufisadi," Takudzwa Munangwa ameandika.
"Lakini kwanini Uganda na wala sio Rwanda au Kenya ama Afrika Kusini," Nelson Tuwadya aliuliza.
"Mataifa ya Afrika ambayo kiwango chao cha ufisadi kiko chini ni 1. Seychelles 2. Botswana 3. Cape Verde 4. Rwanda 5. Mauritius 6. Sao Tome and Principe 7. Namibia 8. Senegal. Kulingana na orodha ya makadirio ya kiwango cha ufisadi iliyotolewa na shirika la Transparency International," Tarrysnun ameandika.
Jaji mkuu wa Zimbabwe Luke Malaba aliwaambia wanahabari kwamba hakimu Justice Lawrence Gidudu, kiongozi wa jopo la kukabliana na ufisadi Uganda, atatoa mafunzo ya wiki moja katika mji mkuu wa Zimbambwe, Harare.
Jaji Malaba amesema Zimbabwe ina mengi ya kujifunza kutoka kwa Uganda ambayo imewashtaki na kuwafungwa jela watu waliopatikana na makosa ya ufisadi kwa miaka mingi tu.
Hatua hiyo imechukuliwa kabla ya kuanzishwa kwa mahakama mpya za kukabiliana ufisadi tu.
Katika hotuba yake ya mwaka wa sheria 2020, Jaji mkuu Malaba amesema mfumo wa mahakama unaimarisha juhudi za kukabiliana na ufisadi ambako kumeorodheshwa kuwa adui namba moja na rais Mnangagwa.
Uganda ambayo imekuwa na mahakama maalum za kukabiliana na ufisadi kwa karibia kipindi cha miaka 10 iliyopita, iliorodheshwa kuwa bora zaidi ya Zimbabwe katika orodha ya makadirio ya nchi fisadi na shirika la Transparency International mwaka 2019.
Katika orodha hiyo, Uganda ilikuwa namba 137 kati ya nchi 180 huku Zimbabwe ikiorodheshwa kuwa namba 158.
Lakini nchi jirani za Zimbabwe kama Botswana, Namibia na Afrika Kusini - ziliorodheshwa katika nafasi nzuri zaidi ya Uganda.
Unaweza kusoma:












