Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Polisi inamsaka mama wa taifa wa Lesotho kwa tuhuma za mauaji huku Waziri Mkuu Thomas Thabane akitangaza kujiuzulu
Waziri Mkuu Lesotho na mke wake wanakabiliwa na uchunguzi unaohusiana na tuhuma za mauaji ambayo yanaweza kuangaziwa katika tamthilia ya kitabu cha hadithi za uhalifu. Mwandushi wa BBC Pumza Fihlani anajaribu kuchambua kisa chao kutoka mji mkuu wa taifa hilo la kusuni mwa Afrika, Maseru.
Watu wanaendelea na shughuli zao za kila siku katika mji huo. Wauzaji mboga wamepanga bidhaa zao kando ya barabara, magari ya uchukuzi wa umma kama vile taxi pia zinawachukua abiria na kuwapeleka katika sehemu tofauti za kazi na kukimbilia wateja wengine.
Kwa kweli kila kitu kinaendeshwa kwa mpangilio utadhani mambo ni shwari. Lakini ukisoma gazeti utapatana na tangazo maalum. Tangazo hilo limewekwa kwenye mabango ya biashara katika barabara kuu za mji wa Maseru na hata katika madirisha ya maduka jijini humo kuashiria kwamba kuna jambo ambalo haliko sawa Lesotho.
Tangazo lenyewe ni la kumtafuta "Mama taifa aliyetoweka." Hii bila shaka inaelezea bayana kuwa hali sio shwari nchini Lesotho.
Moja ya taarifa kuu katika gazeti imeandikwa: "Polisi inamsaka mama taifa." Nyingine inasema: "Waziri mkuu aliye mashakani akubali kujiuzulu."
Kiongozi huyo wa ngazi ya juu nchini - Waziri Mkuu Thomas Thabane pamoja na mke wake wa sasa Maesaiah Thabane - wanatakiwa kuhojiwa kuhusiana na mauaji ya mwaka 2017 ya mke wa kwanza wa Bw. Thabane, Lipolelo Thabane.
Bi Lipolelo mwenye umri wa miaka 58, alikuwa ametengana na mume wake na amekuwa akiishi kivyake tangu mwaka 2012, aliuawa siku mbili kabla ya Bw. Thabane kuapishwa kuwa waziri mkuu.
Jioni moja akiwa njiani kurejea nyumbani kutoka kwa shughuli zake za siku, alishambuliwa na kupigwa risasi mara kadhaa na baadae kupatikana akiwa amekufa kando ya bara bara.
Kifo chake kilishangaza nchi nzima. Wakati huo Bw. Thabane alielezea mauaji hayo kuwa ya "kinyama".
Wakati huo mauaji hayo tylisemekana kutekelezwa na watu wasiojulikana. Lakini ushahidi wa hivi karibuni uliowasilishwa mahakamani na kamishena wa polisi wa nchi hiyo, Holomo Molibeli, umeibua maswali mengi zaidi ambayo yanahitaji ufumbuzi.
Baadhi ya stakabadhi za mahakama, zilizoonekana na shirika la habari la AFP, ilikuwa ni nakala ya barua iliyoandikwa tarehe 23 Desemba 2019, iliyoandikwa na kiongozi huyo wa polisi kwa waziri mkuu aliye na umri wa miaka 80 na ilisema:
"uchunguzi umebaini kwamba kulikuwa na mawasiliano ya simu katika eneo la uhalifu tunaochunguza... kwa kutumia nambari nyingine ya simu. Nambari hiyo ya simu ya rununu ni yako."
Kutoweka kwa mama wa taifa
Waranti ya kukamatwa kwa Maesaiah Thabane, 42, ilitolewa Januari 10 baada ya mshukiwa huyo kukataa agizo la kumtaka afike kituo cha polisi kwa mahojiano.
Hajaonekana hadharani kwa wiki mbili na hakuna mtu anayejua alipo na wala hakuna mtu yeyote anayetaka kuzungumzia suala hilo.
Bw. Thabane, ambaye bado yupo nchini, amekwepa kujibu maswali kuhusiana na alipo mke wake.
BBC imewasiliana na maafisa wa serikali kwa tamko rasmi kuhusiana na sakata hii lakini juhudi hizo zimegonga mwamba. Msemaji wa chama cha waziri mkuu amesema kuwa "swala hilo halijashughulikiwa".
Wiki iliyopita alikubali shingo upande kuhojiwa na polisi kuhusiana na suala hilo.
Bw. Thabane na mke wake hawajafunguliwa mashtaka kuhusiana na mauaji hayo.
Sheria iko wazi kuhusu mamlaka ya mahakama na mamlaka ya kisiasa nchini Lesotho kwamba waziri mkuu anaweza kutakiwa na polisi kwa mahojiano lakini uchunguzi wa polisi haujakuwa rahisi.
Vitisho vya mauaji
Kamishene wa polisi Bw Molibeli, ameimbia BBC kuwa uchunguzi dhidi ya Thabane ni moja ya kesi hatari amewahi kushughulikia katika taaluma yake ya miaka 32 kama afisa wa polisi.
"Haijakuwa rahisi, kumekuwa na majaribio kadhaa ya kutupilia mbali uchunguzi huu."
"Naamini tunachokifanya ni sahihi, alimradi dhamira yangu ipo wazi. Watu wa Lesotho wanataka kujua ukweli na wajibu wetu ni kuchunguza ili tupate majibu kamili kuhusu kile kilichotokea," alisema.
Watu wamemtishia kwa kuendelea mbele na uchuguzi, aliongezea lakini anasisitiza kuwa hilo halijamuogopesha.
"Sina uwoga hata kidogo. Nipo na watu wanaoniunga mkono. Zamani watu ambao wangenitisha ni wanajeshi lakini hata wao, tuna uhusiano mzuri wa kikazi nao.
"Sote tunataka kuondoa Lesotho katika sakata hili."
Japo polisi haijatoa maelezo kuhusiana na ushahidi wa kesi hii, Bw Molibeli amesema ushahidi wao ni "mzito".
Wale waliomfahamu Bi Lipolelo wanasema hakupendelea kuangaziwa na vyombo vya habari ndiposa aliamua kuishi kimya kimya viungani mwa mji mkuu.
Lakini miezi kadhaa kabla ya kifo chake aligonga vichwa vya habari kuhusu kesi ya talaka.
Taarifa za juhudi zake za kisheria za kutaka kutambuliwa kama mama taifa halali wa Lesotho na Bw. Thabane mara kwa mara ziliangaziwa na vyombo vya habari.
Talaka haikukamilishwa
Baada ya kutengana na Bi Lipolelo, bwaba Thabane alikuwa akiishi na Maesaiah kama mke wake na amekuwa akifaidi sifa zote zinazotokana na nafasi hiyo, huku Lipolelo akihangaika mwenyewe vijijini.
Mwaka 2015, baada ya mgogoro mrefu wa kisheria Bi Lipolelo alishinda kesi katika mahakama kuu ambayo ilitoa agizo kwa serikali kukoma kutumia fedha za umma kumsaidia Maesaiah.
Mahakama hiyo pia iliamurua akome "kutekeleza majukumu yoyote ya kitaifa ambayo alipewa mlalamishi [Lipolelo] kama mama taifa ". Uamuzi huo ulikuwa pigo lililomdhalilisha waziri mkuu.
Uamuzi huo ulimaanisha kuwa hadi mchakato wa talaka utakapokamilika, Lipolelo anasalia kuwa mama wa taifa kisheria na kwamba serikali itamtambua kama mke wake na kumsaidia.
Talaka yao haikuwahi kukamilishwa.
Nchi hii ina amani lakini inafahamika kwa mauaji ya maafisa wa ngazi wa juu. Siku za nyuma, hilo lilionekana kusababishwa na mgogoro ndahi ya jeshi au kada za kisiasa.
Bwana Thabane mwenyewe aliwahi kutorokea Afrika Kusini kwasababu ya kile kilichoonekana kama kukwepa kukosolewa sana.
Mme Lipolelo, kama alivyokuwa akifahamika, hakuwa mwanasiasa wala mtu aliyekuwa na maadui wa kisiasa. Kwa wengi, kifo chake kilizua maswali mengi kuliko majibu.
'Haki itendeke kwa Lipolelo'
"Nilishutuka niliposikia kwamba ameaga dunia," mkaazi wa Maseru, Lebohang Liballo amesema.
"Kilichomtokea kilikuwa kitu cha ajabu sana - hata wakati huu, usiri uliopo kwa kifo chake ni wa kushtusha. Mme Lipolelo anahitaji kutendewa haki."
Japo watu wanafuatilia kwa karibu kesi hii kutaka kujua yaliyojiri, bado kuna hofu.
Wale waliokubali kuzungumza na BBC, waliomba kwamba sura zao zisiwekwe wazi.
"Imekuwa aibu kubwa kwa nchi," amesema Bakwena Mofoka.
"Inatufanye tuonekane vyenginevyo. Mama wa taifa lazima arejee."
Lakini Maesaiah hajaonekana kukataa.
Mawakili wake wamekuwa wakijaribu kubatilisha waranti ya kukamatwa kwake ila mahakama bado haijatoa uamuzi kuhusioana na suala hilo.
Mawakili wake wameiambia mahakama kuu mjini Maseru kuwa mke wa waziri mkuu yuko tayari kushirikiana na polisi lakini alikuwa katika shughuli rasmi siku aliyotakiwa kufika kituoni kuhojiwa.
Hawajaelezea kwanini anadhaniwa kuwa nje ya nchi.
Sio mara ya kwanza kwa mke huyo wa pili wa waziri mkuu kujipata mashakani-miaka michache iliyopita alituhumiwa mara kadhaa kwa kujaribu kuingilia shughuli za serikali, hatua ambayo ilitajwa na watu wa Lesotho kuwa "mapinduzi ya chumbani ".
Bw. Thabane amekanusha madai hayo lakini mke wake ametofatiana na baadhi ya watu katika chama tawala.
Migawanyiko ya kisiasa
Sakata hii pia inamuathiri kisiasa Waziri Mkuu.
Wafuasi wake wanahoji muda wa uchunguzi dhidi yake, wakidai kiongozi wao ni muathiriwa wa kampeini mbaya, ameshinikizwa kujiuzulu, japo hajasema ni lini atachukua hatua hiyo.
Amesema atajiuzulu kwasababu ya umri wake lakini hakuhusisha hatua hiyo na uchunguzi unaomkabili.
Chama tawala cha All Basotho Convention (ABC) kimekuwa kikikumbwa na mgawanyiko mkali tangu kuibuka kwa kashfa hii huku wanachama wake wakijaribu kujionesha kuwa kitu kimoja - kama mbinu ya kukabiliana na wapinzani wao na kumpatia nafasi Bw. Thabane kutathmini hatua atakayochukua.
Lakini huenda hana muda mrefu wa kufanya hivyo.
Mamia ya watu wanaojiita "Wananchi wanaojali maslahi ya Lesotho", wiki iliyopita waliandamana katika mji mkuu wa Maseru na kuahidi kufanya msururu wa maandamano yanayolenga kumshinikiza waziri mkuu kuachia madaraka mara moja.
"Tumejitolea kuandamana hadi pale atakapoondoka madarakani
"Kama hiyo itamaanisha nchi kupoteza uthabiti, basi na iwe hivyo, kwasababu itakuwa imechangiwa na waziri mkuu," mshirikishi wa maandamano hayo Ramahoana Mathlosa alisema.
Je hii ni ishara kwamba watu wamechoshwa na kashfa za Bw. Thabane?
Yote tisa, kumi ni kuwa kujiuzulu kwake madarakani sio mwisho wa sakata inayozingira kuuawa kwa mke wake wa kwanza Lipolelo Thabane.