Simba wanaokufa njaa katika hifadhi moja Sudan wasababisha hasira kwa Umma

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 1

Wito ulitolewa kwenye mitandao ya kijamii wa kusaidia simba watano waliokosa chakula na wanaougua kwenye hifadhi ya wanyama iliyopo mji mkuu wa Sudan, Khartoum, kulingana na shirika la habari la AFP.

Jumapili, watu walienda kutembelea hifadhi hiyo ya wanyama baada ya picha za simba hao ambao wako wanaonekana wakiwa katika hali ya kuaga dunia kusambaa katika mitandao ya kijamii, limesema shirika la AFP.

"Mwili wangu ulinitetemeka baada ya kuona simba hawa katika hifadhi... mifupa yao inaonekana juu ya ngozi," mwandalizi wa kampeni ya kunusuru simba hao, Osman Salih, amenukuliwa akizungumza na shirika la AFP.

Simba hao watano wamehifadhiwa katika Bustani ya Al-Qureshi ya Khartoum lakini wamekuwa na wakikosa chakula na dawa kwa wiki kadhaa sasa, shirika la AFP limeongeza.

Maafisa wa hifadhi hiyo ya wanyama na madaktari husika wanasema baadhi ya simba hao wamepoteza karibia theluthi mbili ya uzito wao katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita.

"Chakula huwa ni nadra sana kupatikana na mara nyingi huwa tunanunua kutoka kwa mifuko yetu ili wapate chakula," Essamelddine Hajjar, meneja katika hifadhi hiyo amezungumza na shirika la AFP.

Hifadhi hiyo ya wanyama inamilikiwa na manispaa ya Khartoum na kwa kiasi fulani inafadhiliwa na wahisani lakini Sudan inakumbwa na mgogoro wa kiuchumi uliotokana na kupanda kwa bei za chakula na upungufu wa fedha za kigeni, AFP imesema.