Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Gereza la Makala DRC: Wafungwa wapoteza maisha kwa ukosefu wa chakula na dawa.
Wafungwa takriban 17 wamekufa gerezani katika kipindi cha wiki moja iliyopita kwenye gereza kuu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, shirika moja lisilo la kiserikali limesema.
Wafugwa karibia 10 wamekufa katika gereza hilo kuu lililopo mjini Kinshasa tangu kuanza kwa mwaka 2020.
Wafanyakazi wa kutoa msaada wanasema kwamba vifo hivyo vimesababishwa na ukosefu wa chakula na dawa pamoja na mazingira machafu.
Gereza la Makala lililopo Kinshasa halijapokea chakula katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, hayo ni kulingana na maafisa wa serikali ya DRC.
Hali ni mbaya kiasi gani?
Ukosefu wa chakula katika gereza hilo kuna maanisha kwamba zaidi ya wafungwa 8,000 wanategemea familia zao angalau kupata lishe ya kila siku.
"Hali ni mbaya! watu wanakufa karibu kila siku," afisa wa gereza hilo ambaye hakutaka atajwe aliiambia BBC.
Pia inasemekana kwamba wafungwa wanakufa kwasababu ya joto jingi.
Gereza hilo limejaa wafungwa kupita kiasi huku idadi yao ikiongezeka mara tano zaidi ya lilivyokusudiwa wakati linajengwa.
Pia unaweza kusoma:
Mazingira katika gereza hilo ni mabaya kiasi kwamba mashirika yasiyo ya kiserikali yanakadiria kwamba karibia wafungwa 100 wanaumwa kupita maelezo wakikaribia kufa.
Emmanuel Adu afisa wa wakfu wa Bill Clinton amesema, ''Hali yao ni mbaya sana, wafungwa wanafariki dunia kiholela kila siku kutokana na njaa na ukosefu wa matibabu, tangu mwezi Oktoba mwaka jana katika magereza yote hakukuwa na vyakula wala dawa.''
Hata hivyo naibu waziri wa sheria Celestin Tunda Kasende, amesema ni vigumu kufahamu kama wafungwa wanafariki kwasababu ya uhaba wa chakula kwasababu baadhi ya wafungwa hufika hali ya afya zao zikiwa tete sana.
''Tumewapa matibabu katika kituo cha gereza na kama hali itaendelea kuwa mbaya zaidi tutawahamishia katika hospitali kuu'', amesema Celestin Tunda.
Msongamano wa wafungwa
Asilimia 6 pekee ya wafungwa wa gereza hilo ndio wamehukumiwa huku wengine waliosalia wamesubiri hatma hayo kulingana na mfumo wa sheria ulivyo ambapo kesi zinaweza kuchukua hata miaka kadhaa kusikilizwa.
''Gereza la Makala kwa sasa limepokea msaada kusaidia kuimarisha hali'', amesema naibu waziri wa sheria nchini DRC kwa vyombo vya habari vya eneo.
"Ni kweli kwamba mchakato wa kulipa wasambaji chakula ulichelewa na hapo ndo tatizo lilipoanzia," Waziri Celestin Tunda Ya Kasende ameliambia shirika la habari la AFP, na kuongeza kuwa, "kwa sasa hali imekuwa shwari".
Aidha, ameahidi kwamba pesa zaidi zitaelekezwa katika gereza hilo, lakini mwandishi wa BBC Gaïus Kowene mjini Kinshasa anasema mashirika la haki za kibinadamu yanatilia mashaka taarifa hiyo.
Mashirika ya kutetea haki yanataka serikali iwajibishwe
Naibu waziri wa sheria Celestin Tunda Kasende amekiri kwamba hali ni mbaya na kwamba bejeti ni ndogo na haiwezi kuhudumia wafungwa 9,000 waliopo sasa hivi katika gereza la Makala.
Vifo hivyo vya wafungwa 17 katika gereza la Makala kuliripotiwa na wakfu wa Amani wa Bill Clinton, ambao hauna uhusiano wowote na shirika lenye jina sawa na hilo la wakfu wa Clinton lililoanzishwa na aliyekuwa rais wa Marekani.
Mwaka jana, kuliripotiwa kwamba wafungwa 40 wamega dunia katika mazingira sawa na hayo ndani ya kipindi cha miezi 18 katika gereza jengine lililopo huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.