Mafuriko Jakarta: 'Hii sio mvua ya kawaida', maafisa wanasema

Iliyochapishwa

Karibu watu 21 wamefariki baada ya mafuriko mabaya yaliyosababishwa na mvua kubwa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 24 kukumba mji mkuu wa Jakarta, nchini Indonesia .

Shirika la utabiri wa hali ya hewa linalojulikana kama Meteorology, Climatology and Geophysics Agency (BMKG) kilirekodi kiwango cha mvua ya 377mm (kwa siku katika uwanja moja wa ndege kusini mwa Jakarta.

Kiwango hicho kikitajwa kuwa cha mvua kubwa kuwahi kunyesha kwa siku moja tangu mwaka 1996, wakati shirika hilio lilipoanza kunakili rekodi ya mvua.

"Mvua hiyo iliyoanza kunyesha mkesha wa mwaka mpya ... sio mvua ya kawaida," lilisema shirika hilo.

Pia liliongezea kuwa mvua hiyo imesababishwa na vitu kadhaa ikiwemo upepo wa kusi, viwango vya juu mvuke wa maji katika hewa ambayo inaathiri kusanyika kwa mawingu juu ya kisiwa cha Java.

Karibu watu 62,000 wameondolewa katika mji huo huku baadhi yao wakilala juu ya paa la nyumba wakisubiri kuokolewa.

Mvua kubwa inatarajiwa kunyesha hadi wikendi hii.

Kwengineko katika eneo la Mashariki mwa Jakarta, mvua ya 335mm ilirekodiwa huku mji wa Bekasi, mashariki ya mbali, ikishuhudia kiwango cha mvua ya 259mm.

Mvua ya zaidi ya 150mm kwa siku inachukuliwa kuwa kubwa zaidi.

Mvua kubwa ilianza kunyesha mkesha wa mwaka mpya na kuendelea kwa usiku kucha, hali iliyosababisha baadhi ya maeneo viungani mwa mji huo kukumbwa na maporomoko ya udongo.

Walioathiriwa ni watu kati ya miaka minane na 82. Baadhi yao walikufa maji baada ya kuzama na wengine kutokana maporomoko ya udongo.

Kijana mmoja wa miaka 16 alifariki baada ya kukanyaga nyaya za umeme ndani ya maji.

Huduma za umeme zimekatizwa katika wilaya za Jakarta huku baadhi ya njia za reli zikifungwa.

Katika ukurasa wa Twitter wa Rais Joko Widodo alilaumu miundo mbinu ya kudhibiti mafuriko kwa kusababisha uharibifu mkubwa.

Mafuriko hukumba mji huo wakati kama huu wa mwaka.

Hii ndio moja ya sababu Bw. Widodo anapanga kuhamishia mji kuu hadi Borneo mashariki kwa miaka michache ijayo.

Jakarta ni moja ya miji inayozama kwa kasi duniani na wataalamu wanasema huenda ikazama yote ifikapo mwaka 2050.