Moto Australia: Maelfu watorokea baharini huku moto mkali ukielekea pwani

Wakazi wa Batemans Bay mjini New South Wales pia walikimbilia baharini kujiepusha na moto huo

Chanzo cha picha, ALASTAIR PRIOR

Maelezo ya picha, Wakazi wa Batemans Bay mjini New South Wales pia walikimbilia baharini kujiepusha na moto huo
Iliyochapishwa

Maelfu ya watu nchini Australia wamekimbilia ufuo wa bahari kujinusuru na moto wa nyikani ambao unaoelekea maeneo ya pwani.

Wakaazi wa Mallacoota wameuelezea moto huo kuwa "kisa cha kuogofya" huku wakisimulia jinsi walivyoona anga ilivyobadilika rangi nyekundu wakiwa ndani ya boti.

Maafisa wamethibitisha kuwa watu wawili wamefariki kutokana na moto huo katika mji wa New South Wales (NSW) kufikia sasa vifo 12 vimehusishwa na janga hilo la moto.

Mamlaka pia zinasema watu wanne hawajulikani waliko katika miji ya Victoria na NSW.

Miili ya waathiriwa wa hivi punde ambayo inaaminiwa kuwa ya baba na mwanawe wa kiume ilipatikana katika mji wa Corbargo eneo la NSW, ambalo lilikumbwa na moto siku ya Jumanne.

Watu wa Mallacoota waliokolewa na kupelekwa katika fukwe za bahari katika mazingira ya kutisha

Chanzo cha picha, PETER HOSKIN

Maelezo ya picha, Wakaazi wakiokolewa na kupelekwa katika fukwe za bahari baada ya moto kuteketeza mji wa Mallacoota

"Hali ya kusikitisha," alisema naibu wa kamishena wa polisi katika eneo la NSW Gary Worboys. "[bila shaka] walikuwa wanajaribu kujinusuru kutokana na moto huo kwa sababu ulizuka mapema saa za asubuhi."

Mjini Mallacoota, Wahudumu wa kitengo cha kuzima moto walisema mkondo wa upepo umebadilika na kuongeza kuwa hali hiyo imegeuza mkondo wa moto kutoka maeneo ya makazi.

Maeneo kadhaa ya kujivinjari msimu wa sherehe katika mwambao wa pwani kati ya miji ya Sydney na Melbourne kwa sasa yamekatizwa kutokana na moto huo.

Gavana wa jimbo la Victoria Daniel Andrews amesema meli huenda zikatumwa kuwapelekea wahanga wa moto huo chakula, maji na nguvu za umeme katika maeneo hayo.

Map

Barabara kuu ya Princes Highway imefungwa.

"Baadhi ya watu waliotengwa wanaweza kufikiwa kupitia bahari,"alisema.

Mamlaka zilitoa wito kwa watu wa eneo hilo wengi wao watalii kutoondoka lakini ilipofika Jumatatu hali ilikuwa mbaya na hatari kufanya shughuli ya kuwahamisha.

Moto wa nyikani katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo imetokana na ongezeko la viwango vya joto, upepo mkali na radi ya wakati wa ukame.

Presentational grey line

Mamlaka pia zinasema zimeripoti kwa watu saba hawajulikani waliko katika eneo hilo wanne kutoka Victoria na watatu wa New South Wales.

"Tunahofia usalama wao. Wamekuwa katika mazingira ya moto na hatuwezi kubainisha waliko kwa sasa," alisema Waziri Mkuu wa Victoria Daniel Andrews siku ya Jumanne.

'Tuko tayari kuruka majini'

Wakaazi wameiambia BBC kuwa hali ilikuwa ya ''kuogopesha'' huku majivu yaliyotokana na moto huo, yakianguka katika fukwe za bahari.

Mwanamke mmoja aliwasilisha picha ya mwanawe wa kiume akiwa amevalia kifaa cha kumsaidi kuvuta pumzi na boya la kujiokoa familia yake ilipoingia kwenye boti kutoroka moto katika mji wa Mallacoota

Chanzo cha picha, ABC NEWS

Maelezo ya picha, Mwanamke mmoja aliwasilisha picha ya mwanawe wa kiume akiwa amevalia kifaa cha kumsaidi kuvuta pumzi na boya la kujiokoa familia yake ilipoingia kwenye boti kutoroka moto katika mji wa Mallacoota

Mji wa Mallacoota, umeathiriwa zaidi na moto huo, na siku ya Jumanne wakaazi walilazimika kukimbilia usalama wao

"Ilikuwa mchana lakini kulikuwa na giza sawa na usiku wa manane na kile tulichosikia ni sauti ya moto mkali uliokuwa usambaa kwa kasi ya ajabu," alisema David Jeffrey, mmoja wa wafanyibiashara. "Sote tunahofia usalama wetu."

Moto huo umeharibu majengo kadhaa, lakini ulikatiza makali yake baada ya mkondo wa upepo katika ufuo wa bahari kubadilika.