Mzozo wa Lebanon: Makumi ya watu wamejeruhiwa katika siku ya pili ya makabiliano Beirut

Protesters stand near burning tents during anti government protests in Beirut

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Waandamanaji walionekana wakiwa wamesimama karibu na mahema yaliyokua yakiungua mtoto wakati wa usiku wa pili wa maandamano mjini Beirut
Iliyochapishwa

Polisi wa kutuliza ghasia na wandamanaji wa wanaoipinga serikali wamekabiliana katika usiku wa pili wa ghasia za maandamano katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut, na kuwaacha makumi kadhaa ya watu wakiwa na majeraha.

Waandamanaji waliwarushia chupa na vijinga vya moto maafisa wa polisi, ambao walijibu kwa gesi za kutoa machozi na kuwamwagia maji ya kuwasha.

Wakati huo huo, Waziri wa mambo ya ndani wa Lebanon Raya el-Hassan ameagiza kufanyika kwa msako mkali wa vikosi vya usalama.

Maandamano dhidi ya matumizi mabaya ya kiuchumi yanayoongozwa na wasomi nchini humo yalianza mwezi Oktoba.

Makabiliano hayo ni baadhi ya ghasia mbaya zaidi tangu kuanza kwa maandmano ambayo yalikuwa awali ni ya amani kwa kiasi kikubwa. Yalisababisha kujiuzulu kwa Waziri Mkuu, Saad al-Hariri, lakini mazungumzo ya kuunda serikali mpya yamekwama.

Jumatatu, bunge la Lebanon litaangalia ni nani linaeweza kumteua kama waziri mkuu, huku bwana Hariri akitarajiwa kurejea katika wadhifa huo.

Polisi wa kutuliza ghasia na vikosi vya usalama walisambazwa kwa wingi Jumapili huku maelfu ya waandamanaji wakirejea mitaani.

Vikosi vinavyolinda usalama wa ndani ya nchi (Lebanon's Internal Security Forces) vilisema kuwa viliwafyatulia waandamanaji gesi za kutoa machozi waliokua wakiwarushia vijinga vya moto na mawe.

Demonstrators use their phone lights during an anti-government protest in Beirut

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Maandamano katikakati ya mji mkuu wa Lebanon Beirut yalianza kama maandamano ya amani

Jeshi la ulinzi wa raia la Lebanon lilisema kuwa liliwapatia matibabu watu 46 waliokuwa wamejeruhiwa na kuwapeleka wengine 14 hospitalini, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.

Muandamanaji, Omar Abyad, mwenye umri wa miaka 25- ambaye ni nesi ambaye hajapata ajira tangu alipohitimu masomo miaka miwili iliyopita, aliliambia shirika la habari la Reuters: " Vikosi vya usalama vilituvamia kinyama utafikiri hatukua tunaandamana kwa ajili yao, ya watoto wao."

Lebanese security forces remove protesters during an anti-government demonstration

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Vikosi vya usalama vya Lebanon wakati wa maandamano.
Demonstrators move metal barriers while engulfed in tear gas during clashes with security forces in Beirut

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Makumi ya watu walijeruhiwa katika makabiliano

Waziri wa mambo ya ndani aliagiza vikosi vya usalama kufungua uchunguzi "wa haraka na wa uwazi" juu ya ghasia za Jumamosi, lakini akaonya dhidi ya "wachochezi " wanaotaka kutumia maandamano kuchochea "maluimbano".

Diala Haidar, kutoka shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, alisema "vikosi vya usalama vilitumia nguvu kupita kiasi kuwatawanya waanndamanaji waliokuwa wanaandamana kwa amani ", aliongeza: "Inatuma ujumbe wa wazi kwamba vikosi vya usalama viko juu ya sheria na vitachukua hatua zozote zile kumaliza maandamano vitakapohitaji kufanya hivyo ."

Maandamano hayo yamekuwa makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Lebanon katika kipindi cha zaidi ya muongo. Wamevuka mipaka ya matabaka - jambo ambalo ni nadra kutokea tangu vilipomalizika vita vya wenyenyewe kwa wenyewe vya 1975-1990 -na kuwahusisha watu kutoka sekta zote za jamii.

Unaweza pia kusoma:

Waandamanaji wamegadhabishwa na viongozi wao kwa kushindwa kushughulia mkwamo wa uchumi, kupanda kwa bei za bidhaa, ukosefu wa ajira wa hali ya juu, huduma mbaya za umma na ufisadi.

Madai yao ni pamoja na kuitaka serikali kumaliza ufisadi, kuchunguzwa kwa mfumo wa kisiasa na kuundwa kwa baraza la mawaziri huru lisilo la kimatabaka.