Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Toni-Ann Singh: Malkia wa urembo wa Jamaica ashinda taji la Miss World 2019
Toni-Ann Singh amejishindia taji la 69 la shindano la malkia wa urembo la Miss World.
Ni mara ya kwanza katika historia kwamba mwanamke mweusi anamiliki mataji ya Miss USA, Miss Teen USA, Miss America, Miss Universe na Miss World.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 23 ni mzaliwa wa eneo la St Thomas nchini Jamaica na anapanga kusomea utabibu na kuwa daktari.
Alituma ujumbe wa twitter siku ya Jumamosi akisema: ''Tafadhali mujue kwamba muna thamani na uwezo wa kuafikia ndoto zenu ....muna malengo''.
Toni-Ann aliwafurahisha majaji katika hafla hiyo mjini London baada ya kuimba wimbo wa Whitney Houston ' I Have Nothing', na kujibu maswali tofauti.
Alisema: ''Hii ni kama ndoto, nimeshukuru sana. Chochote kile munachokiona ndani yangu, ahsanteni, niko tayari kuanza kazi''.
Aliwashinda wagombea wengine 111 wa taji hilo waliokuwa wakiwakilisha mataifa yao, na kuwa mshindi wa nne wa Jamaica tangu shindano hilo lizinduliwe.
Alipoulizwa na jaji Piers Morgan iwapo angependelea kuwa mwimbaji, alisema: Iwapo milango itafunguliwa nitaingia.
Waliochukua nafasi ya pili walishirikisha Ophely Mezino kutoka Ufaransa na Suman Rao kutoka India.
Kitu kimoja kilichovutia hisia za watu mitandaoni ni jinsi malkia wa urembo wa Nigeria alivyotoa hisia zake kufuatia ushindi wa Toni-Ann.
Nyekachi Douglas, ambaye alikuwa katika nafasi ya tano alirukaruka na kupiga kelele na furaha wakati mshindi alipotangazwa.