Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Saudi Arabia: Ruksa wanawake na wanaume sasa watatumia mlango mmoja migahawani
Saudi Arabia sasa haitohitaji tena migahawa kuwa na milango tofauti ya kuhudumia wateja kulingana na jinsia na familia, serikali imesema.
Awali, ilikuwa lazima kuwa na mlango mmoja kwa ajili ya familia na wanawake na mwengine wa wanaume.
Sharti hilo kwa sasa limeondolewa huku migahawa mingi pamoja na maeneo mengine ya kufanyia mikutano ikifuata mkondo huo.
Hata hivyo mabadiliko ambayo yamejitokeza katika miaka ya hivi karibuni nchini Saudi Arabia yamekuwa yakiponzwa vikali na wapinzani.
Mapema mwaka huu, agizo kutoka kwa mfalme lilihitaji wanawake wa Saudia kuruhusiwa kusafiri hadi mataifa ya nje bila ya kupata ruhusa ya msimamizi wa kiume pamoja na kuondoa marufuku ya wanawake kujiendesha wenyewe ambayo ilifikia ukomo wake mwaka 2018 iliyokuwa imedumu kwa miongo kadhaa
Hata hivyo wanaharakati wanalalamika kwamba sheria nyingi zinazobagua wanawake bado zinaendelezwa na watu wengi mashuhuri wanaotetea haki za wanawake wamekamatwa hata wakati ambapo serikali inafanya mabadiliko haya.
Jumapili iliyopita, mamlaka ya serikali ya mitaa ya Saudia ilisema migahawa haitokuwa na ulazima wa kuwa na mlango unaotenganisha wanawake na wanaume badala yake uamuzi wa suala hilo umeachwa mikononi mwa mmiliki wa biashara.
Hadi kufikia sasa, ndani ya migahawa ya Saudia, familia na wanawake hutenganishwa na wanaume kwa kutumia skrini au vioo vikubwa.
Tangu Mohammed bin Salman alipotawazwa na kuwa mfalme mwaka 2017, amefanya mabadiliko katika jamii ambayo imekuwa ikikumbatia tamaduni zake za tangu jadi.
Mabadiliko yake yameungwa mkono na jamii ya kimataifa lakini yamekuwa yakikandamizwa.
Hata hivyo kifo cha mwanahabari mashuhuri Jamal Khashoggi mwaka 2018 katika ubalozi wa Saudi Arabia huko Istanbul, ulikosolewa vikali na jamii ya kimataifa japo viongozi wakuu duniani akiwemo Rais Donald Trump wameendelea kuiunga mkono Saudi Arabia
Maafisa wa Saudi Arabia wamesema Khashoggi, aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Riyadh, aliuawa katika oparesheni iliyotekelezwa na timu ya majasusi. Hata hivyo wakosoaji wengi wanaamini vyenginevyo, huku mtaalam wa Umoja wa Mataifa akitoa ripoti iliyosema kuwa kifo cha Khashoggi kilitekelezwa na "maafisa wa serikali".