Amos Wako: 'Nilishangaa kusikia taarifa ya vikwazo vya Marekani dhidi yangu nikiwa safarini nchini Uganda''

Amos Wako
Iliyochapishwa

Mwanasheria mkuu wa zamani wa Kenya Amos Wako amepinga vikali hatua ya Marekani kumwekea marufuku ya usafiri yeye na familia yake nchini humo.

Bwana Wako anasema hatua ya hivi punde ya Marekani dhidi yake ni kufufua kesi ya zamani ambayo haelewi lengo lake ni nini.

''Kwa miaka minane sijakuwa serikalini. Tangu nilipostaafu japo visa vya ufisadi vimekithiri mno, jina langu halijatajwa au kuchunguzwa kuhusiana na visa vya ufisadi.'' aliwaambia wanahabari.

Anasema sababu ya yeye kuwekewa marufuku ya usafiri mara ya kwanza na hivi sasa ilikuwa kuhusishwa kwake na visa vya ufisadi na kwamba vyote vinatokana na kazi yake ya zamani kama mwanasheri mkuu.

Wako aidha amesema kuwa haelewi kwa nini anawekewa vikwazo vipya wakati kuna marufuku inayohusiana na suala hilo miaka 10 iliyopita.

Amos Wako anasema sasa anataka Marekani itoe ushahidi unaomhusisha na ufisadi
Maelezo ya picha, Amos Wako anasema sasa anataka Marekani itoe ushahidi unaomhusisha na ufisadi

''Badala ya kukabiliana na ufisadi wanafufua visa vya zamani ambavyo havina msingi wowote'' alisema.

Mwanasheria huyo mkuu wa zamani sasa anataka Marekani itoe ushahidi unaomhusisha na ufisadi.

Hii ni mara ya pili, mamlaka nchini Marekani imempiga marufuku Amos Wako, ikidai ''alijihusisha pakubwa na ufisadi''.

Kulingana na waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani Mike Pompeo marufuku hiyo ni kwa sababu ya Wako kuhusishwa na ulaji rushwa na ufisadi.

Hatahivyo, taarifa hiyo haijaelezea waziwazi ni vitendo gani vya rushwa au ufisadi Wako alihusika navyo.

''Marufuku hiyo pia inamhusisha mkewe na mwanawe.

Hatua ya Marekani ya kumpiga marufuku bwana Amos Wako imechukuwa sura mpya, baada ya tume ya serikali ya kupambana na ufisadi maarufu kama EACC kusema kwamba ilishiriki kikamilifu katika hatua hiyo.

Mkuu wa tume ya EACC Daktari Eliud Wabukala amenukuliwa na vyombo vya habari nchini Kenya akisema kuwa tume yake imekuwa msitari wa mbele kutoa habari na maelezo kuhusu ufisadi kwa Marekani na balozi za kigeni.

Bw. Wabukala ameashiria kwamba huenda Wakenya wengine mashuhuri wakakumbwa na hali kama iliyomfika bwana Wako.

Wadadisi wa mambo wanasema kwamba huenda vikwazo vya usafiri vinavyomkumba bwana Wako vilitokana na kashfa ya kifedha ya Anglo Leasing, ambayo ilisababisha serikali ya Kenya kupoteza mabilioni ya pesa.

Kashfa hiyo ililipuka wakati bwana Wako alipokuwa akihudumu kama mkuu wa sheria, na alinyoshewa kidole cha lawama kwa madai ya kuwa kizuizi katika uchunguzi wa sakata hiyo.

Mnamo mwaka wa 2009, naibu wa zamani wa waziri wa mashauri ya nje wa Marekani Johnnie Carson, ambaye alikuwa anazuru Kenya, alitangaza kwamba Bwana Wako amepigwa marufuku kuzuru Marekani kwa madai kwamba amekuwa kikwazo kwenye vita dhidi ya ufisadi nchini Kenya.

Washington inasema kuwa hatua ya vikwazo dhidi ya Wako inakusudiwa kuisadia Kenya katika vita dhidi ya ufisadi
Maelezo ya picha, Washington inasema kuwa hatua ya vikwazo dhidi ya Wako inakusudiwa kuisadia Kenya katika vita dhidi ya ufisadi

Hatua ya sasa ya kuwanyima vibali vya kusafiri bwana Wako, mkewe Flora Ngaira na mtoto wake wa kiume Julius Wako inamaanisha kwamba watatu hao hawawezi kuzuru Marekani au kufanya biashara na kampuni za Marekani.

Hatahivyo, bwana Wako, ambaye kwa sasa ni Senata nchini Kenya, anaweza kukanyaga kwenye ardhi ya Marekani ila tu kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, ingawa haruhusiwi kwende nje ya mipaka ya makao hayo.

Tume ya kupambana na ufisadi nchini Kenya(EACC) kupitia kwa mwenyekiti wake Eliud Wabukala ilidai ilishirikiana pakubwa na wachunguzi wa Marekani katika kuwekwa kwa marufuku hiyo.

Washington ilisema kuwa hatua hiyo inakusudiwa kuisadia Kenya katika vita dhidi ya ufisadi.

Wadadisi wanadai kuwa huenda matatizo ya Bwana Wako yalitokana na sakata ya Anglo Leasing iliyohusu kandarasi za usalama zenye thamani ya mamilioni ya madola ambapo serikali ilipoteza fedha hizo zinazoaminika ziliishia kufichwa katika mataifa ya nje.

Bwana Wako alikuwa akihudumu kama Mwanasheria mkuu wakati sakata hiyo ilipoanza na analaumiwa kwa kuwa kuzuizi kwa uchunguzi wa wizi huo.

Mwaka 2009, aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Johnnie Carson, akizuru Kenya, alitangaza kuwa bwana Wako alipigwa marufuku ya kuingia nchini Marekani kwani alionekana kuwa kizingiti dhidi ya ufisadi.

Marufuku hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Bwana Wako.

Marufuku hii sasa inamaanisha kuwa Bwana Wako na familia yake ya karibu kando na kutoruhusiwa kuingia Marekani pia hawatakubaliwa kufanya biashara yoyote na serikali ama kampuni za Marekani.

Hatahivyo, Bwana Wako ambaye anahudumu kama seneta nchini Kenya bado anaweza kuingia Marekani kama mgeni katika makao makuu ya Umoja wa mataifa (U.N) ingawa hatakuwa na uhuru wa kutembea ndani ya Marekani.

Wako alikuwa mwanasheria mkuu wa Kenya kwa muda wa miaka 20, kati ya mwaka 1991 na 2011.