Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kura ya maoni Ethiopia: Jinsi kura ya Sidama inavyomuweka katika mizani waziri mkuu Abiy Ahmed
- Author, Christine Yohannes
- Nafasi, BBC Amharic
- Iliyochapishwa
Shughuli ya upigaji kura inaendelea katika eneo la Sidama nchini Ethiopia katika kura ya maoni itakayoamua iwapo taifa hilo litakuwa na jimbo la 10.
Zaidi ya watu milioni mbili wamesajiliwa na tume ya uchaguzi kushiriki katika uchaguzi huo. Mwandishi wa BBC Kalkidan Yibeltal ana mengi kutoka Hawasa, kusini mwa Ethiopia.
Vituo vya kupiga kura vilifunguliwa rasmi mwendo wa saa sita asubuhi lakini wapiga kura wengi katika mji wa Hawassa walianza kuweka foleni kubwa saa kadhaa kabla ya hilo.
Wapiga kura wanaweza kushiriki katika shughuli hiyo hadi mwendo wa saa kumi na mbili jioni. Afisi za umma , shule na biashara zimefungwa siku ya Jumatano.
Magari pia yamezuiliwa katika hatua kadhaa zilizochukuliwa na utawala ili kuhakikisha kuwa shughuli ya upigaji kura inafanyika kwa amani.
Mwezi Julai mwaka huu wanakampeni kutoka makundi ya kikabila ya Sidama waliuawa katika ghasia wakati walipojitangazia jimbo lao kinyume na sheria.
Sidama ni kundi la tano kwa ukubwa likiwa na zaidi ya watu milioni nne. Matokeo ya kura hiyo ya maoni yanatarajiwa kutangazwa baadaye wiki hii.
Iwapo matokeo hayo yataunga mkono uundaji wa jimbo jipya, Watu wa Sidama watajiondoa katika taifa la kusini ambalo wanagawanyana na makundi mengine hamsini kwa zaidi ya miongo miwili.
Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed anakabiliwa na kibarua kigumu kujaribu kuzuia ukabila ambao unatishia kuongeza mgawanyiko nchini humo.
Kura hiyo ya maoni inaonekana kama jaribio la iwapo hofu kuhusu makabila yanayotaka kujitenga inaweza kutatuliwa kwa amani.
Pia huku taifa hilo likijiandaa kufanyika kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa mwezi Mei mwaka ujao, kura hiyo pia inatarajiwa kuupima mfumo wa uchaguzi wa taifa hilo.
Kwa nini hilo linafanyika?
Tangu alipoingia madarakani mwezi Aprili 2018, waziri mkuu Abiy amesifiwa kwa kuleta mabadiliko chungu nzima.
Amebadilisha kile kilichojulikana kuwa taifa lenye udhibiti wa usalama wa hali ya juu.
Pia aliongoza mchakato wa amani na maadui zao wa jadi Eritrea - hatua ambayo ilimfanya yeye kushinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka huu.
Lakini hatua yake ya jinsi anavyoangazia mashirika na vyama vinavyopigania haki ya makabila tofauti imezua hofu.
Ghasia katika maeneo tofauti ya tafa hilo zimelazimu takriban watu milioni kutoroka makaazi yao katika kipindi cha miezi 20 iliopita.
Kura ya maoni kuhusu uzinduzi wa jimbo jipya ni miongoni mwa mchakato wa kikatiba ambao unatarajiwa kuridhisha tamaa za kikabila katika eneo moja la taifa hilo.
Kucheleweshwa kwa kura hiyo mapema mwaka huu , kulizua ghasia katika baadhi ya miji huko Sidama ambapo takriban watu 25 walifariki.
Je ni nini ambacho wale wanounga mkono jimbo la Sidama wanakitaka?
Katiba ya Ethioipia ya mwaka 1995 iliunda majimbo tisa ya kikabila . Kwa mfano jimbo la Tigray linamilikiwa na watu wa kabila la Tigraya.
Huku lile la Amhara likitawaliwa na watu wa kabila la Amharic. Lakini Sidama ilikuwa ndani ya SNNPR ambapo kuna makaazi ya makabila 50.
Likiwa na asilimia 4 ya idadi ya watu nchini humo , Sidama ni kabila la tano kwa ukubwa na kwamba wengi wanahisi kwamba wanahitaji utambulizi mkubwa kisiasa na katika serikali.
Chini ya katiba ya zamani kulikuwa na mkoa wa pekee kwa jina Sidamo ambao licha ya kujumuisha makabila kadhaa ulitambua Sidama kama jina lake.
Jimbo Jipya lingemaanisha kwamba Sidama inaweza kutengeza sera zake , kudhibiti kikosi cha polisi, na kusimamia matumizi yake ya bajeti ambayo yangeangazia matumizi ya watu wa Sidama pekee.
Pia jimbo hilo lingewapatia watu wa Sidama utambuzi wa lugha na utamaduni wao.
Je athari za uundaji wa jimbo jipya ni zipi?
Huku kukiwa hakuna upinzani mkubwa miongoni mwa watu wa Sidama kufuatia pendekezo la jimbo jipya , kuna wasiwasi kwamba kura hiyo ya maoni inaweza kuwa mfano wa kuigwa na makabila mengine.
Kwa mfano ndani ya SNNPR baadhi ya watu wa makabila ya Wolayta na Hadiya pia wanapigania kuwa na majimbo yao .
Wito kama huo wa kujitenga pia umetolewa na makundi ya Amhara na Tigray.
Changomoto kuu kwa waziri mkuu na serikali yake itakuwa jinsi atakavyoangazia mahitaji hayo yote bila kushinikiza hofu zaidi , ama kuhatarisha mgawanyiko zaidi ndani ya taifa hilo.
Je ni nini unachopasa kujua kuhusu kura hiyo?
Takriban watu milioni 2 wamejisajili kushiriki katika uchaguzi huo wa siku ya Jumtano , kulingana na tume ya uchaguzi ya taifa hilo.
Ili kushiriki katika kura hiyo , watu walitakiwa kuthibitisha kwamba wamekuwa wakiishi katika eneo la Sidama kwa takriban miezi sita.
Katika karatasi ya kupigia kura, wapiga kura watahitajika kuweka alama katika viboksi viwili.
Wale wanaotaka jimbo jipya wataweka alama karibu na ishara ya shafeta, bakuli la kitamaduni la Sidama.
Wale wanaotaka eneo la Sidama kusalia ndani ya SNNPR wataweka alama katika karatasi ya kupiga kura karibu na ishara ya nyumba ya kitamaduni.
Tume ya uchaguzi inasema kwamba matokeo hayo yatajulikana siku ya Alhamisi.