Baba yake Beyonce Mathew Knowles afichua kuwa aligundulika na saratani ya matiti

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Mathew Knowles, baba yao wanamuziki maarufu wa wanamuziki wa pop Beyonce na Solange Knowles, amefichua kuwa alipatikana na ugonjwa wa saratani ya matiti.

Bwana Knowles mwenye umri wa miaka 67-amezungumzia kuhusu hali yake katika mahojiano na kipindi cha Good Morning America, ambacho kitatangaza mahojiano hayo baadae leo katika kituo cha wa televisheni nchini Marekani cha ABC

Kionjo cha mahojiano kilitumwa Jumanne kuambatana na siku ya kwanza ya mwezi wa kutoa uelewa juu ya saratani:

Saratani ya matiti ambayo ni nadra kwa kawaida hutokea kwa wanaume wenye umri wa zaidi ya miaka 60.

Katika kionjo hicho cha mahojiano, Bwana Knowles ameonyeshwa akiulizwa ni jinsi gani alitangaza kwa mara ya kwanza taarifa ya ugonjwa huo kwa familia yake.

Bwana Knowles ambaye ni mjasiliamali na msemaji wa umma amesema kuwa "atatoa tangazo maalum " katika kipindi cha Jumatano.

Knowles, ambaye ni afisa mauzo wa zamani katika kampuni ya Xerox anafahamika zaidi kwa kuunda kikundi cha bendi ya Destiny's Child, bendi ambayo illimuinua binti yake mkubwa Beyonce hadi kufikia kiwango cha kuwa nyota kimuziki .Pia alikuwa meneja wa muziki wake wa solo hadi mwaka 2011

Alitalikiana na mama yake Beyonce na Solange Tina mwaka 2011 na tangu wakati huo alipata watoto wawili na mke wake wa pili Gena.

Saratani ya matiti miongoni mwa wanaume

Ni saratani inayopatikana kwa nadra sana miongoni mwa wanaume ikilinganishwa na ilivyo kwa wanawake - Nchini Uingereza wanaume 319 walipatikana na saratani ya matiti mwaka 2017, ikilinganishwa na wanawake ambao mwaka huo huo walikuwa ni 46,000 kwa mujibu wa ofisi ya taifa hilo ya takwimu.

Madhara ya saratani e kwa wanaume hutegemea ni kwa umbali gani ugonjwa huo umesambaa mwilini wakati inapogunduliaka,

Dalili za saratani ya matiti kwa wanaume zinaweza kujumuisha uvimbe katika titi , kuingia ndani kwa chuchu na kutoka kwa majimaji katika chuchu.