Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Serikali Tanzania yawaagiza polisi kuacha kunyanyasa bodaboda
Kilio cha madereva wa bodaboda nchini Tanzania kuwa wananyanyaswa na askari wa usalama barabarani limetua bungeni nchini humo.
Wabunge wamelalamikia tabia ya polisi kuwasimamisha waendesha bodaboda kwa makosa ya kukiuka sheria za barabarani na kisha kuwapiga.
Waziri Kangi Lugola aliliambia Bunge: ''Polisi wanaruhusiwa kuwatoza faini ..lakini hawapaswi kuapiga au kuzishikilia pikipiki zao".
''Ni wajibu wetu kuwalinda vijana ambao wanataka kupambana na umasikini na kujibunia ajira wenyewe''.
''Hakuna boda boda itakayokamatwa na askari wa usalama barabarani na kupelekwa kituoni kama haiko kwenye haya makundi matatu yafuatayo, kundi la kwanza bodaboda iliyohusika katika uhalifu, itapelekwa kituoni, bodaboda kundi la pili isiyo na mwenyewe iliyookotwa imetelekezwa itaokotwa na kupelekwa kituoni na kundi la tatu ni boda boda iliyohusika kwenye ajali au iliibiwa na kupatikana itapelekwa itakuwa kama kielelezo.''Alieleza Waziri Lugola
Tangazo hilo limewafurahisha sana waendesha boda boda kwa kuwa suala lao limejadiliwa bungeni lakini bado wana hofu kuwa mambo huenda yakawa vilevile.
''Hakuna boda boda itakayokamatwa na askari wa usalama barabarani na kupelekwa kituoni kama haiko kwenye haya makundi matatu yafuatayo, kundi la kwanza bodaboda iliyohusika katika uhalifu, itapelekwa kituoni, bodaboda kundi la pili isiyo na mwenyewe iliyookotwa imetelekezwa itaokotwa na kupelekwa kituoni na kundi la tatu ni boda boda iliyohusika kwenye ajali au iliibiwa na kupatikana itapelekwa itakuwa kama kielelezo,'' alieleza Waziri Lugola.
Bodaboda wanasemaje?
Kassim Maulid ni mwendesha bodaboda na anasema kauli hiyo ya waziri ni faraja kubwa kwake na madereva wengine wa vyombo hivyo
"Humu barabarani kuna maudhi makubwa sana kwetu, na askari wa usalama barabarani ni sehemu ya maudhi hayo," amesema na kuongeza: "Kiufupi, sidhani kama kuna dereva yeyote wa bodaboda jijini Dar es Salaam ambaye hajawahi kuonewa na askari."
Madeeva hao pia wamekuwa wakilaumiwa kwa kuvunja sheria kwa makusudi na bwana Maulid anakiri hilo,"...kama serikali inawataka askari wake kujirekebisa, hata sisi pia lazima tujirekebishe. Inakuwaje unaingia barabarani bila kofia ngumu mbili? Ama huna leseni? Wakati mwengine ni sisi ambao tunatengeza mazingira ya askari kutunyanyasa."
"Jana jioni nimetoka kughasiwa na trafiki, alinikamata akisema taa za breki haziwaki vizuri, wakati uhalisia ni kuwa zipo vizuri. Alichomoa ufunguo wa bodaboda yangu na kukaa nao kwa zaidi ya saa moja. Ikabidi nimpatie elfu 10 ndio akanirudishia funguo nikaendelea na shughuli zangu," mwendesha bodaboda Cladius John ameiambia BBC.
Cladius anaamini kuwa askari wa barabarani wanawachukulia kama watu wa daraja la chini na visa vya manyanyaso vitaendelea licha ya agizo la waziri, "Ni kauli nzuri, inatia moyo. Tunashukuru wabunge wamekiona kilio chetu. Lakini sioni askari hao wakiacha kutunyanyasa, sisi ndio wanyonge wao. Hatuna pa kuwapeleka ama kuwashtaki."