Tunachofahamu kuhusu ndege ya Marekani isio na rubani ilioangushwa na ndege za Urusi

Iliyochapishwa

Ndege isiyo na rubani ya Marekani iliyoanguka kwenye Bahari Nyeusi ndiyo kitovu cha mzozo mpya kati ya Washington na Moscow. Marekani imesema iliiangusha ndege hiyo isiyo na rubani baada ya ndege ya kivita ya Urusi kuigonga mabawa yake

Moscow imekanusha hili, ikisema kuwa ndege hiyo isiyo na rubani ilikumbwa na hitilafu ya mitambo

Siku ya Alhamisi asubuhi, Pentagon ilitoa video ya tukio hilo. BBC haijaona picha zinazoonyesha matukio kabla au baada ya mgongano huo.

Hapa kuna kile tunachojua juu ya kile kilichotokea.

Marekani imesema nini?

Marekani ilisema ndege yake isiyo na rubani ya MQ-9 Reaper ilipata uharibifu tarehe 14 Machi baada ya ndge mbili za kijeshi za Urusi aina ya Su-27 kuiangusha kwenye Bahari Nyeusi.

Ndege moja ya kijeshi iligonga bawa moja la ndege hiyo isyo na rubani, Marekani ilisema, na kulazimisha vikosi vya Marekani "kuiangusha MQ-9 kwenye maji ya kimataifa".

Makabiliano hayo yalidumu kwa takriban dakika 30-40, maafisa wa Marekani walisema. Walidai kuwa ndege za Urusi zilimwaga mafuta kwenye ndege isiyo na rubani mara kadhaa kabla ya kuigonga.

Vitendo vya rubani wa Urusi "karibu kusababisha ndege zote mbili kuanguka," alisema msemaji wa Pentagon Pat Ryder, akiongeza kuwa ndege ya Urusi huenda iliharibika lakini bado iliweza kutua.

Maafisa wa Marekani hawajasema iwapo ndege hiyo isiyo na rubani ilikuwa imebeba makombora.

Video hiyo inaonyesha nini?

Video ambayo haijawekwa bayana, ambayo ina urefu wa sekunde 42, inaonyesha mlisho kutoka kwa kamera iliyowekwa chini ya ndege isiyo na rubani ya uchunguzi.

Ndege ya Urusi SU-27 inaonekana ikitoa kile kinachoonekana kuwa mafuta inapokaribia.

Katika tukio la kwanza SU-27 inaonekana kuchafua lenzi ya kamera kwa mafuta. Njia ya pili iko karibu zaidi - kutatiza muonekano wa video kutoka kwa ndege inayoendeshwa kwa mbali.

Picha inaporudi, mbawa moja ya ndege isiyo na rubani inaonekana umepinda na kupoteza umbo lake.

Urusi imedai kuwa ndege hiyo isiyo na rubani ilikuwa inakaribia eneo lake, lakini tunachoweza kuona kwenye video hiyo ni bahari, anga na mawingu.

Urusi inasema nini?

Urusi inakanusha madai ya Marekani . Inalaumu ajali hiyo kutokana na "ujanja" uliofanywa na ndege isiyo na rubani, badala ya kugusana na ndege hizo.

Moscow pia imekanusha kuwa ndege zake zote ziliharibiwa wakati wa mgongano huo.

Maafisa wa Urusi walisema ndege hiyo isiyo na rubani ilikuwa ikiruka na vidhibiti vyake vya mawasiliano vikiwa vimezimwa, na kwamba ilikuwa imekiuka anga yenye vikwazo.

Baada ya kuitwa kuzungumza na maafisa mjini Washington, balozi wa Urusi nchini Marekani, Anatoly Antonov, alisema Moscow iliona tukio hilo la ndege isiyo na rubani kama "uchochezi".

Kwa mtazamo wa Kremlin, Bw Antonov aliongeza: "Shughuli zisizokubalika za jeshi la Marekani katika ukaribu wa mipaka yetu ni sababu ya wasiwasi."

Baada ya kuzungumza kwa njia ya simu na waziri wa ulinzi wa Marekani kwa mara ya kwanza tangu Desemba, waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu alilaumu tukio hilo kwa "kuongezeka kwa shughuli za upelelezi dhidi ya maslahi ya Shirikisho la Urusi".

Jitihada za uokozi

Urusi imethibitisha kwamba inajaribu kuokoa mabaki ya ndege hiyo isiyo na rubani ya Marekani , ambayo huenda ilizama hadi kina cha futi 5,000 (m 1,500) chini ya bahari.

"Sijui kama tutaweza kuokoa au la lakini lazima ifanyike," katibu wa baraza la usalama la Urusi Nikolai Patrushev alisema kwenye runinga ya serikali.

Jenerali Mark Milley, jenerali mkuu wa kijeshi wa Marekani , alisema kuwa "hatua za haraka " zilichukuliwa ili kuzuia data yoyote nyeti kuanguka kwenye mikononi ya Urusi.

Siku ya Jumatano, alisema kuwa Marekani haina meli yoyote katika Bahari Nyeusi, jambo linalotatiza juhudi za utafutaji na uokoaji, lakini "ina washirika na marafiki wengi katika eneo hilo".

"Tutafanya kazi kupitia shughuli za uokoaji, hiyo ni mali ya Marekani," aliwaambia waandishi wa habari, akiongeza kuwa "pengine hakuna mengi ya kukokoa" hata hivyo.

Bado haijafahamika ni wapi tukio hilo lilifanyika. Afisa mmoja wa Marekani ambaye jina lake halikutajwa aliiambia CNN kwamba ilitokea takriban maili 45 kusini-magharibi mwa rasi ya Crimea, na kwamba ndege isiyo na rubani ilianguka maili 70 kusini-magharibi mwa eneo la Ukrainia lililoshikiliwa na Urusi.

Je ilikuwa ni makusudi?

Hakuna upande unaokanusha kuwa tukio hilo lilitokea baada ya Urusi kujaribu kuizuia ndege hiyo isiyo na rubani.

Huko Marekani, maafisa wamezungumzia ikiwa ndege hiyo iliangushwa kwa makusudi au kwa bahati mbaya.

Jenerali Milley alisema Jumatano kwamba bado ni mapema sana kusema.

Lakini msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Ned Price aliwaambia waandishi wa habari kwamba "tathmini bora hivi sasa ni kwamba labda haikuwa kukusudia".

"Pengine ilikuwa ni matokeo ya uzembe mkubwa kwa upande wa mmoja wa marubani hawa wa Urusi."

Bila kujali, hatari ni kubwa wakati kuna tukio kama hili , amesema Jenerali wa Marekani David Berger, kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Marekani.