Uchungu wa kutojua huku makuburi ya pamoja ya Mariupol yakiongezeka

Zaidi ya makaburi mapya 1,500 yamechimbwa katika eneo la makaburiya umma karibu na mji wa kusini mwa Ukraine wa Mariupol, kulingana na uchambuzi wa picha mpya za satelaiti uliofanywa kwa niaba ya BBC.
Eneo la kaskazini-magharibi mwa jiji lina uwanja mkubwa wa makaburi ambayo maafisa wa Ukraine na mashahidi wanasema ina maelfu ya miili.
Mariupol, mji wa bandari ulio karibu na mpaka na Urusi, ulikuwa lengo kuu la kimkakati kwa Warusi.
Tangu kuanza kwa vita ilipigwa bila kuchoka kutoka angani na kutoka ardhini. Kufikia wakati ilipoanguka kwa Warusi mnamo Mei, maelfu ya raia walikuwa wamekufa na sehemu kubwa ya jiji ilikuwa imeharibiwa.
Picha za hivi majuzi za satelaiti kutoka Maxar zinaonyesha kuwa maeneo matatu ya mazishi ya watu wengi karibu na Mariupol yaliyoko Staryi Krym, Manhush na Vynohradne, yamekuwa yakiongezeka kwa kasi tangu majira ya machipuko.
The Centre for Information Resilience kilichanganua picha za Staryi Krym katika kipindi cha Panorama cha BBC na kugundua kuwa makaburi mapya 1,500 yamechimbwa humo tangu kilipochambua picha kwenye tovuti hiyo mara ya mwisho mwezi Juni. Sasa inakadiria kuwa zaidi ya makaburi 4,600 yamechimbwa hapo tangu mwanzo wa vita, ingawa inasema haiwezi kujua ni miili mingapi iliyozikwa kwenye eneo hilo.
Maafisa wa Ukraine sasa wanaamini kuwa watu wasiopungua 25,000 waliuawa katika mapigano huko Mariupol, na kwamba 5,000-7,000 kati yao walikufa chini ya vifusi baada ya nyumba zao kulipuliwa.
Mashahidi huko Mariupol wameiambia BBC kwamba wameona mamlaka ya Urusi ikiondoa miili kutoka kwa vifusi vya majengo yaliyoharibiwa katika jiji hilo katika miezi ya hivi karibuni na kuipeleka kwa mazishi.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Simulizi ya kutisha ya Olga Sagirova ni taswira ya kile ambacho watu wengi huko Mariupol walipitia. Alikuwa mtu pekee ndani ya nyumba yake aliyenusurika wakati ilipolipuliwa na Warusi. Mume wake na wazazi wake waliuawa, na kama wengi ambao sasa wametoroka jiji, hajui miili yao iko wapi.
Mhasibu huyu mwenye umri wa miaka 48 aliishi na mumewe Valery katika nyumba ya ghorofa mbili na bustani iliyopambwa, katika kitongoji cha makazi cha Mariupol. Watoto wake wawili watu wazima waliishi kwingine.
Kulikuwa na utulivu katika eneo lake mwanzoni mwa Machi, licha ya mashambulizi makali katika maeneo mengine ya jiji. Hata hivyo, kila usiku yeye na mume wake walikuwa wakilala kwenye handaki chini ya nyumba yao . "Nilikuwa nalia kila wakati, mume wangu alijaribu kunituliza," alisema Olga. "Alisema nisiwe na wasiwasi, kwamba tutapitia hili."
Jioni ya Machi 10, siku ya 15 ya shambulio la bomu la Urusi, mlango uligongwa. Wazazi wa Olga, ambao walikuwa na umri wa miaka 80, walikuwa wamesimama pale wakionekana kutikiswa sana.

Chanzo cha picha, MAXAR/CIR
Nyumba yao ilikuwa imevamiwa na kuteketea kwa moto. Olga aliwaleta ndani na kuwasihi walale naye kwenye maficho yake .Lakini hawakutaka, hivyo akawapa chumba cha kulala katika nyumba kuu.
Saa 22:30 Valery alipanda ghorofa kutoka sebuleni kwa sababu milipuko ilikuwa imetulia na alitaka kupumzika. Lakini alimtuliza Olga, akisema angerudi ikiwa chochote kitatokea.
Saa 03:30 aliamka na kusikia sauti ya ndege. Ghafla nyumba nzima ikashuka juu yake.
"Yote yalitokea kwa sekunde moja. Kila kitu kilikuwa kinaniangukia," alisema.
"Miguu yangu ilikuwa imezikwa nusu, hivyo sikuweza hata kusogea. Usikivu wangu uliporudi polepole, niliweza kusikia sauti ya mume wangu mahali fulani: 'Olga, nisaidie, nitoke nje,' alisema. "Niko karibu na ngazi."
Olga aliweza kumuona Valery umbali wa futi sita tu lakini hakuweza kumfikia. Alizikwa kwa undani zaidi kuliko yeye.
Alichoweza kufanya ni kuendelea kuzungumza naye. "Baada ya muda, nilimsikia akipumua," alisema. "Kisha alikuwa kimya."
Akiwa peke yake gizani, Olga alijaribu kupiga mayowe lakini hakuna aliyemsikia. Hatimaye, aliona tochi ikimsogelea. Ni majirani zake waliojaribu kumtoa kwenye kifusi. Hawakuweza kufanya hivyo, walisema wangerudi jua linapochomoza.
Olga alikuwa peke yake tena, na mumewe, ambaye alikuwa amezungumza maneno yake ya mwisho, alizikwa kwenye kifusi karibu naye.
Saa kadhaa chini ya vifusi
Kulipopambazuka, Olga alianza kujua mazingira yake. Alipotazama juu aliona bamba la zege – lililoinama na kutishia kumwangukia.
"Nilijua kwamba hakuna jambo la maana zaidi. Nilikuwa nikifa," anasema. Wakati huo, anasema, alijaribu kujiua.
Hatimaye majirani zake walirudi na wengine na wakajaribu kumchimbua. Walifanikiwa kuutoa mguu mmoja wa Olga. Lakini bamba moja la zege lilikuwa linakandamiza lile lingine.
Kwa saa sita zenye uchungu zaidi walijaribu kuufungua mguu wake wa kulia. Hatimaye waliamua kuzungushia kebo kwenye mguu wa Olga na kuuvuta kwa nguvu.
"Niliogopa sana kwamba hawakuweza kutoa mguu wangu na ningeachwa bila mguu," anasema.
Baada ya majaribio matatu, Olga aliachiliwa. Miguu yake yote miwili ilivunjika sehemu nyingi na hakuweza kutembea kwa karibu miezi mitano. "Mguu wangu wa kulia ulivunjwa kabisa," alisema.
Usiku huo Olga alipoteza sio tu mume wake, lakini wazazi wake, ambao walikuwa wamelala katika eneo kuu la nyumba wakati ilipopondwa.
Lakini mateso yake yalikuwa bado hayajaisha.
Olga alipokuwa akitunzwa kwenye pishi la karibu huko Mariupol alipata habari zenye kuhuzunisha zaidi.
Dada yake na shemeji yake pia walikuwa wameuawa nyumbani kwao siku tatu zilizopita.
"Walikuwa wamekaa kwenye bustani yao wakinywa kahawa wakati bomu lilipopiga," Olga alisema.
"Nilipoteza watu wangu watano wa karibu katika siku chache."
Nilipokutana na Olga, alikuwa akiishi Huizen karibu na Amsterdam, akiwa salama pamoja na watoto wake wawili waliokuwa watu wazima. Sasa anaweza kutembea tena, baada ya miezi kadhaa ya kuhitaji kutumia kiti cha magurudumu.
Anajifunza Kiingereza na anapenda kutembea na kutazama maua na bustani zinazomkumbusha nyumbani.
Yeye ni mwanamke mchangamfu na anayezungumza kwa upole na tabasamu la urafiki sana. Olga aliniambia anafurahi kuwa hai na anaamini kwamba alikuwa amejaliwa kuishi.
Nilipomtumia meseji siku nyingine kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa, alijibu: "Hata iweje, maisha yanaendelea na nina ufahamu kwamba lazima niishi!"
Alikuwa ametumia muda mwingi wa siku akilia.
Hadi katikati ya majira ya kiangazi alijilazimisha kukesha hadi asubuhi ili kuepukana na jinamizi ambalo alikumbuka hali ya kutisha. Yeye husogeza bila kikomo picha za maisha yake ya awali na anasema bado hajaelewa kikamilifu kile kilichompata.
Katika watoto wake wawili watu wazima anamuona mumewe. Anamkosa Valery sana hivi kwamba anashindwa kuvumilia. Walikuwa wakiogelea pamoja, kufanya karamu mara moja kwa wiki, na sasa Olga anaishi katika gorofa ndogo katika nchi ya kigeni.
Olga ameshindwa kupata taarifa kuhusu miili ya familia yake, lakini inashukiwa bado imezikwa chini ya vifusi vya nyumba yake.
Warusi wanaudhibiti mji huo sasa, lakini Olga aliambiwa msimu huu wa joto kwamba mwili mmoja unaweza kuonekana umekwama kwenye magofu ya nyumba yake ya zamani.
Mchimba kaburi
Olga ni mmoja tu wa watu wengi kutoka Mariupol ambao hawawezi kupata miili ya jamaa zao waliopotea.
Baadhi yao walizikwa katika makaburi ya halaiki katikati mwa Mariupol, yaliyochimbwa na raia wa Ukraine ambao walijizatiti kwa ufyatuaji wa makombora ili kuchukua maiti zilizokuwa zimeachwa mitaani na majumbani.
Mapema mwezi Machi, Vaagn Mnatsakanian, mwanaikolojia wa eneo hilo, alikuwa akijaribu kutafuta mahali pa kumzika babake ambaye aliuawa katika mapigano hayo. Vaagn aligundua kwa kuchukizwa kwake kuwa vyumba vya kuhifadhia maiti vimejaa.
Alienda kwa viongozi wa eneo hilo kuuliza ni wapi angeweza kumzika baba yake na - akigundua ni wangapi wengine walikuwa katika hali kama hiyo - alijitolea kuanza kuandaa mazishi ya dharura.
Alianza kupanga timu za wenyeji wengine kuchimba maeneo matatu ya makaburi ya watu wengi katikati ya jiji kwa mamlaka ya manispaa ya Kiukreni. Kwa siku tano mnamo Machi yeye na timu yake walikusanya miili kutoka karibu na Mariupol, chini ya makombora makali.

Miili iliingizwa kwa haraka kwenye mitaro, mara nyingi bila mifuko ya mwili. "Katika baadhi ya siku za kutisha tuliambiwa kulikuwa na zaidi ya miili 100 - wakati mwingine miili 150 - ambayo ilihitaji kukusanywa siku hiyo," alisema. "Zilikuwa nyingi sana ambazo hatukuweza kuzikusanya zote.
"Siku moja kombora liliruka kuelekea kwangu na ilinibidi kuruka ndani ya kaburi la pamoja ili kujificha. Nilijikuta karibu na maiti, lakini nilifurahi kuwa hai," alisema Vaagn.
Namtafuta mwanangu
Tatyana, ambaye alipoteza mtoto wake katika mapigano, alikuwa akitamani sana kumpata na msimu huu wa joto alitembelea eneo la mazishi la watu wengi huko Vynohradne karibu na Mariupol akimtafuta.
Anasema hajui kilichompata Yaroslav mwenye umri wa miaka 26, ambaye alipenda magari na alikuwa na ndoto ya kumiliki biashara yake mwenyewe.
"Tulihesabu zaidi ya makaburi mapya 800 [huko Vynohradne]," alisema Tatyana, ambaye anapendelea kutotumia jina lake la pili. Watu wengi kutoka mji unaodhibitiwa na Urusi hawataki kusema wazi juu ya mazishi ya watu wengi, kwa kuogopa kulipizwa kisasi na mamlaka zinazodhibiti mji huo.
Alichukua picha ya eneo moja huko Vynohradne. Makaburi mengi kwenye eneo hilo yamewekwa alama na mabango madogo yenye nambari na jinsia, lakini sio majina. "Miili mingi haijatambuliwa," alisema.
Wengine ambao BBC ilizungumza nao na kutembelea vyumba vya kuhifadhia maiti vya muda huko Mariupol ili kujaribu kutafuta wapendwa wao msimu huu wa joto, na ilibidi wachunguze miili mingi iliyokuwa nje -chini bila bia kuhifadhiwa ndani ya friji.
"Watu wanapaswa kujua ukweli kuhusu mambo haya ya kutisha," Tatyana alisema, "ili isitokee tena".












