EPL:Klabu mwiba kwa Liverpool na Manchester City msimu huu

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa

Manchester City na Liverpool zimetoa upinzani mkali katika miaka ya hivi karibuni hatua ambayo imepandisha kiwango cha soka ya Uingereza hadi ngazi ya juu.

Katika misimu mitano iliyopita, City inayonolewa na mkufunzi Pep Guardiola imetwaa taji la ligi kuu mara nne, huku Reds ya Jurgen Klopp ikishinda mara moja.

Inaonekana timu hizi mbili ndizo zitakazoshika nafasi mbili za kwanza kwa msimu wa  pili wa 2022-23, baada ya City kuimarisha kikosi chao kwa kumsajili mshambuliaji wa Norway Erling Haaland na kiungo wa kati wa Uingereza Kalvin Phillips, huku Liverpool wakimleta Darwin Nunez kuchukua nafasi ya Sadio Mane.

Timu hizo mbili zilikutana kwenye kombe la Community Shield siku ya Jumamosi - Nunez akifunga huku Liverpool ikishinda 3-1.

Huku kundi la klabu zilizosalia zikiwa na lengo la kuziba pengo hilo, ni klabu gani kati ya zilizomaliza nyuma yao ambazo zina uwezekano mkubwa wa kuzipa changamoto timu hizo mbili ?

Chelsea

Raheem Sterling alijiunga na Chelsea kutoka Man City

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Raheem Sterling alijiunga na Chelsea kutoka Man City

Nafasi msimu uliopita: 3

Wachezaji wapya: Raheem Sterling (£50m), Kalidou Koulibaly (£33m)

Wachezaji walioondoka: Antonio Rudiger (bila malipo), Andreas Christensen (bila malipo), Danny Drinkwater (bila malipo), Romelu Lukaku (loan)

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kumekuwa na msukosuko mkubwa katika klabu ya Chelsea baada ya Mmarekani Todd Boehly kuinunua klabu hiyo ili kumaliza enzi yenye mafanikio makubwa ilioachwa na Roman Abramovich.

Boehly ana kibarua kigumu kufuata nyayo hizo lakini alionyesha nia ya kumsajili Raheem Sterling kutoka kwa mabingwa Manchester City.

Ingawa sio mchezaji mbadala, mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza anachukua nafasi ya Romelu Lukaku, ambaye alirejea Inter Milan baada ya msimu wa mapambano Stamford Bridge ambapo alitofautiana na kocha Thomas Tuchel.

Chelsea walikuwa kileleni mwa jedwali katika hatua moja muhula uliopita lakini kiwango chao kilishuka katika kipindi cha pili cha kampeni, na sasa bila mshambulizi mkuu katika kikosi chao Tuchel anapeleka kikosi cha kwanza cha wachezaji watatu akiwemo Kai Havertz, Timo Werner na Christian Pulisic ambao wanapatikana  msimu huu.

Beki muhimu wa Ujerumani Antonio Rudiger aliondoka bila malipo na kujiunga na Real Madrid na nahodha wa Senegal Kalidou Koulibaly hatimaye amehamia Ligi ya Premia kama mbadala wake.

Tottenham

Richarlison

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Richarlison ndiye mchezaji mpya wa Tottenham kutoka Everton

Nafasi msimu uliopita: 4

Wachezaji waliojiunga: Ivan Perisic (bila malipo), Fraser Forster (bila malipo), Yves Bissouma (£35m), Richarlison (£60m), Clement Lenglet (kwa mkopo), Djed Spence (£20m)

Wachezaji walioondoka: Steven Bergwijn (£26m), Jack Clarke (£10m)

Spurs walipata nafuu chini ya Antonio Conte baada ya kuanza vibaya msimu uliopita na kutwaa nafasi ambayo haikutarajiwa ya Ligi ya Mabingwa na Muitaliano huyo ameungwa mkono kikamilifu katika dirisha hili la usajili.

Pauni milioni 60 zimelipwa kwa Everton kwa ajili ya huduma ya Richarlison, ingawa mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil hana uhakika wa kuanza moja kwa moja, jambo ambalo linaonyesha nguvu waliyonayo sasa.

Yves Bissouma anaongeza udhabiti katika safu ya kati . Huku usajili wa bila malipo wa Ivan Perisic ukionekana kuwa wa busara kwani Mcroatia huyo alifunga mabao manane na kutoa pasi saba za mabao kwa Inter Milan kwenye Serie A msimu uliopita.

Conte ameshinda mataji ya ligi kuu akiwa na Juventus, Chelsea na Inter Milan na huku timu hiyo ya kaskazini mwa London ikiongeza kikosi cha msimu uliopita, huenda wakaonekana na baadhi ya watu kama wanaopewa nafasi kubwa ya kuingia katika nafasi mbili za juu.

Spurs pia wanaingia kwenye msimu mpya wakiwa na hisia shwari zaidi kuliko mwaka jana wakati mustakabali wa mshambuliaji Harry Kane ulikuwa mashakani huku tetesi za kuhamia Manchester City zikiibuka lakini hazikutimia.

Arsenal

Jesus ndiye atakayeiongoza safu ya mbele ya Arsenalk msimu huu

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Jesus ndiye atakayeiongoza safu ya mbele ya Arsenalk msimu huu

Nafasi msimu uliopita: 5

Wachezaji waliojiunga: Marquinhos (£3m), Fabio Vieira (£30m), Matt Turner (£8m), Gabriel Jesus (£45m), Oleksandr Zinchenko (£30m)

Wachezaji walioondoka: Konstantinos Mavropanos (dau lisilojulikana), Alexandre Lacazette (uhamisho wa bila malipo), Matteo Guendouzi (£9m)

Mashabiki wa Arsenal wanatumai kuwa wachezaji wao wapya wanaovutia macho wanaweza kuongeza umahiri kwenye kikosi kilichofeli mwishoni mwa msimu uliopita, baada ya kuonekana kuchujwa kwenye nafasi ya nne bora.

Mikel Arteta alifanikiwa kumnunua mshambuliaji Gabriel Jesus kwa dau la £45m kutoka Manchester City na Mbrazil huyo ataongoza safu ya mbele ya The Gunners msimu huu. Wakati huo huo, mchezaji wa kimataifa wa Ukraine Oleksandr Zinchenko alimfuata Jesus na kujiunga na Arsenal kutoka Manchester.

Kiungo wa kati wa Ureno Fabio Vieira pia amejiunga kutoka Porto, wakati Alexandre Lacazette akirejea Lyon, hivyo mchezaji wa kimataifa wa Norway Martin Odegaard ameteuliwa kuwa nahodha wa timu hiyo.

Bosi Arteta aliweka imani yake kwa vijana msimu uliopita, Arsenal ikiwa timu yenye wachezaji wenye umri mdogo zaidi, kwa hivyo mwaka mwingine wa uzoefu unapaswa kuwaweka katika nafasi nzuri.

Manchester United

Cristiano Ronaldo na Maguire

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Cristiano Ronaldo na Maguire

Nafasi msimu uliopita: 6

Wachezaji waliojiunga: Tyrell Malacia (13m), Christian Eriksen (uhamisho wa bila malipo), Lisandro Martinez (£55m)

Wachezaji walioondoka : Dean Henderson (kwa mkopo), Edinson Cavani (bila malipo), Juan Mata (bila malipo), Paul Pogba (bila malipo), Jesse Lingard (bila malipo), Lee Grant (alistaafu), Nemanja Matic (bila malipo), Andreas Pereira (£10m)

Msimu huu utaadhimisha miaka 10 tangu Manchester United ilipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza mara ya mwisho na sasa jukumu hilo linamwangukia meneja wa zamani wa Ajax Erik ten Hag ambaye atajairibu kurejesha hadhi ya mabingwa hao walioanguka .

Mashetani Wekundu walichechemea hadi kumaliza katika nafasi ya sita msimu uliopita chini ya bosi wa muda Ralf Rangnick, na kuandikisha pointi zao za chini zaidi katika Ligi ya Premia na kulikuwa na ripoti za ghasia katika vyumba vya kubadilishia nguo.

Wachezaji wa kikosi cha kwanza wenye majina makubwa akiwemo Paul Pogba, Jesse Lingard na Edinson Cavani wote wameondoka, huku kusajiliwa bila malipo kwa Christian Eriksen kukitarajiwa kuwa kazi kubwa.

Bado kuna masuala ya kusuluhishwa - nahodha Harry Maguire, ambaye alikuwa na mchezo mbaya, alizomewa na wafuasi wake nyakati fulani msimu uliopita na alidhihakiwa kwa mara nyingine kwenye mechi ya kabla ya msimu mpya dhidi ya Crystal Palace kwenye Uwanja wa Kriketi wa Melbourne.

Na swali kubwa linabaki, je Cristiano Ronaldo atasalia au atakwenda? Aliichezea United katika mechi ya kirafiki Jumapili dhidi ya Rayo Vallecano kwenye Uwanja wa Old Trafford - lakini mustakabali wake wa muda mrefu bado unatakiwa kutatuliwa.

Je, kuna timu zingine?

Je, Newcastle inaweza kuvuruga timu kuu sita msimu huu? The Magpies walionekana kama watu wasio na uwezo mwanzoni mwa kampeni lakini walifanya mabadiliko ya kushangaza chini ya Eddie Howe.

Katika kipindi cha pili cha msimu huu, Newcastle ilivuna pointi 38 ambazo ziliboreshwa pekee na Liverpool (48), waliomaliza nafasi ya pili, na hatimaye mabingwa Manchester City (46).

Usajili wa pesa nyingi wa kiungo wa kati wa Uholanzi Sven Botman utaongeza utulivu zaidi kwenye safu ya nyuma, wakati kipa wa England Nick Pope hatimaye akiweza kuwa nambari moja nyuma yake.