Mabadiliko ya mawaziri: Rais Ruto 'apima anga ya 2027' au aboresha utendakazi?

Iliyochapishwa

Na Yusuf Jumah

BBC Swahili, Nairobi

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais Ruto anasema mabadiliko hayo yanalenga "kuboresha utendakazi na kuimarisha utoaji wa huduma kama ilivyoainishwa katika manifesto ya utawala".

Rais wa Kenya William Ruto ametangaza mabadiliko makubwa ya baraza la mawaziri na kuiweka wizara ya mashauri ya nchi za kigeni chini ya ofisi ya waziri mkuu na kuwahamisha mawaziri wengine saba.

Haya yanajiri baada ya rais kuwakosoa mawaziri wake hadharani hivi majuzi, akiwashutumu baadhi yao kwa kutokuwa na ufahamu kuhusu nyadhifa zao.

Rais Ruto anasema mabadiliko hayo yanalenga "kuboresha utendakazi na kuimarisha utoaji wa huduma kama ilivyoainishwa katika manifesto ya utawala".

Je wachambuzi wametafsiri vipi mabadiliko hayo?

Maelezo ya sauti, Mabadiliko katika baraza la mawaziri:Rais Ruto alitaka kuafikia kipi?

Kwanza rais Ruto hajamfuta kazi Waziri yeyote katika mabadiliko yake ya kwanza tangu kutwaa madaraka mwaka mmoja uliopita . Calvin Muga ,mchambuzi wa siasa nchini Kenya anasema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kwamba rais anapata muhula wa pili kwa kutoanza mafarakano na wafuasi wa mawaziri ambao utendakazi wao umetiliwa doa na hivyo basi kuamua kuwahamisha hadi wizara zinazoonekana kutokuwa na majukumu mengi ama mazito .

Hata hivyo Stella Agara ambaye ni mtaalam wa masuala ya utawala na serikali anasema Wakenya wengi walimtaraji rais kuwafuta kazi mawaziri ambao mienendo yao haijaambatana na hadhi walizopewa kama mawaziri .

Wizara ya mashauri ya nchi za kigeni sasa itaongozwa na Waziri Mkuu Musalia Mudavadi, huku waziri wa awali Alfred Mutua akiongoza wizara ya utalii.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Bw Mutua mnamo Mei alisema kwamba Kenya ilikuwa imeingia mkataba wa kisheria kwa ajili ya kuwapeleka wafanyakazi nchini Kanada lakini taifa hilo la Amerika Kaskazini baadaye lilikanusha makubaliano hayo na kuonya dhidi ya njama za udanganyifu za uhamiaji.

Katika wiki za hivi majuzi, Bw Mutua amekuwa sura ya kampeni ya Kenya kupeleka polisi 1,000 nchini Haiti.

Pia walioathirika ni aliyekuwa waziri wa biashara Moses Kuria, ambaye sasa ataongoza wizara ya utumishi wa umma.

Bw Kuria siku za hivi majuzi amekuwa akikosolewa kwa kile ambacho kimeonekana kuwa mbinu yake ya kiburi wakati wa kushughulikia gharama ya juu ya maisha nchini Kenya.

Pia hapo awali amezua utata kuhusu matamshi yake dhidi ya duka linalomilikiwa na Wachina linalouza bidhaa za bei nafuu za nyumbani nchini Kenya. Hivi karibuni pia alipuuzwa na Mwakilishi wa Biashara wa Marekani wakati wa ziara yake ya hivi majuzi nchini Kenya.

Hivi majuzi Kenya imeshuhudia msururu wa maandamano ya upinzani dhidi ya kupanda kwa gharama ya maisha na nyongeza ya kodi iliyowekwa na serikali.

Mudavadi na siasa za 2027

TH

Chanzo cha picha, MUDAVADI/FACEBOOK

Kulinga na mchambuzi Calvin Muga ,rais ametumia mabadiliko hayo kuanza kufanya ‘majaribio’ ya mkakati wake wa kuchaguliwa tena mwaka wa 2027.

‘Kwa kumpa Musalia Mudavadi wizara ya mashauri ya kigeni,rais anajaribu kumsongesha karibu naye,kuna uwezekano kwamba rais anajaribu kutathmini iwapo Mudavadi anaweza kuwa naibu wake katika tiketi ya 2027-Hilo huenda lisimfurahishe naibu wake wa sasa Rigathi Gachagua’ anasema Muga .

Wizara ya Mashauri ya kigeni itampa Mudavadi jukumu jingine muhimu la kuiwakilisha Kenya kimataifa ,hatua ambayo ni fursa nzuri kwake kujitangaza pia kisiasa na kujenga mtandao wake wa washirika wa kimataifa wanaoweza kumpiga jeki katika siku zijazo .

Muga anasema kwa sasa huenda Naibu wa rais Rigathi Gachagua asijitokeze wazi kunung’unikia hilo lakini baadaye ukweli wa nia ya rais kumpa Mudavadi nafasi hiyo utadhihirika .

Utendakazi serikalini utaboreka?

Swali la iwapo mabadiliko hayo yataboresha utendakazi ndio zito zaidi ,lakini kulingana na mchambuzi Calvin Muga ,rais alitaka kwanza kumaliza aibu,migogoro na matumizi ya lugha chafu miongoni mwa baadhi ya mawaziri wake na maafisa wakuu serikalini .

Stella Agara anahisi kwamba mageuzi hayo ya rais ni kama ujumbe wa tahadhari kwamba rais atachukua hatua kwa mawaziri wasiotekeleza vyema majukumu yao na huenda waliopewa fursa ya pili katika mabadiliko hayo wakarekebisha mienendo yao na kuboresha uchapakazi wao .

Kuhusu iwapo kutakuwa na mabadiliko katika utendakazi,Muga anasema itakuwa vigumu kuona mabadiliko kwa sababu jambo tofauti lingekuwa kuwaondoa kabisa mawaziri ambao utendakazi wao haujaridhisha .

Kumekuwa na hisia kwamba rais Ruto aliwapa wanasiasa kazi za uwaziri kwa sababu walimuunga mkono katika uchaguzi uliopita na inakuwa vigumu kuwachukulia hatua za moja kwa moja bila kulemaza uhusiano wake na wapiga kura katika maeneo wanakotoka baadhi ya mawaziri hao.

Matumaini ya wadadisi wengi ni kwamba iwapo Ruto atashinda uchaguzi kuhudumu muhula wa pili mwaka wa 2027 ,atakuwa na uwezo zaidi kuwateua mawaziri wenye uwezo mkubwa kufanikisha ajenda yake ya maendeleo kuliko ilivyo sasa .