Uhamisho 11 wa wachezaji uliowahi kushangaza katika dirisha la usajili la Januari

Iliyochapishwa

Na Yusuph Mazimu

BBC Swahili

Soka

Chanzo cha picha, Getty Images

Dirisha la usajili la ajira ya baridi barani Ulaya linafungwa saa nane usiku wa kuamkia Jumatano kwa saa za Afrika Mashariki. Ni dirisha linalotoa nafasi kwa vilabu kurekebisha, kuziba ama kuongeza nguvu ya vikosi vyao.

Tayari dirisha la sasa lililofunguliwa Januari 1, 2023 limeonyesha makucha ya matumizi hasa kwa vilabu vya ligi kuu England, yaliyovunja rekodi ya matumizi tangu dirisha la majira ya baridi lilipoanzishwa.

Uchambuzi kutoka kampuni ya michezo ya Deloitte unaonyesha kuwa matumizi ya usajili katika ligi kuu ya England yamefikia £440m, ambayo ni £10m zaidi ya awali ya juu zaidi yaliyowekwa mnamo Januari 2018.

Mara kadhaa ni dirisha linaloonekana kuwa na sifa ya kuleta maajabu ya uhamisho wa kushangaza wa majina makubwa kuhama vilabu vyao isivyotarajiwa.

Mykhailo Mudryk ametua Chelsea akitokea Shakhtar Donetsk kwa kushangaza. Mosi dau lake la kushangaza la £88.5m lakini pia kukaribia kutua Arsenal kabla ya 'kubadili gia angani'.

Wakati macho yakielekezwa kwa kiungo Moises Caicedo wa Brighton na sakata lake la kutua Arsenal, katika saa chache zilizosalia huenda tukashuhudia uhamisho mwingine wa kushangaza. Lakini huko nyuma tumeshawahi kushuhudia uhamisho wa kushtusha uliofanywa katika ndirisha la Januari.

11. Juan Mata: Chelsea - Manchester United (2014)

Mata

Chanzo cha picha, Getty Images

Juan Mata alihama Chelsea akiwa nyota mkubwa kwenda Manchester United, mwaka 2014 kwa dau la £37.1m. Ni wachache sana waliofikiri David Moyes, kocha wa wakati huo wa Manchester United akifanya hivi. Licha ya kocha huyo kufukuzwa baadaye Mata akaweza kuisaidia United kushinda mataji manne,, akimpiku Andy Cole kwa kucheza mechi nytingi zaidi na United huku akilingana kwa mabao na gwiji Roy Keane.

10. Bruno Guimaraes: Lyon - Newcastle (2020)

Bruno

Chanzo cha picha, Getty Images

Mbrazil huyu alikuwa akisakwa na vilabu vikubwa vya Arsenal, Manchester United, Inter Milan na Juventus, lakini Januari 2022 dau la  £40m lilimtoa Lyon ya Ufaransa na kutua Newcastle ambao walimpa pia mshahara mnono ambao ilikuwa ngumu kuukataa. Eddie Howe kocha wa Newcastle United anaonekana kutengeneza timu kumzunguka kiungo huyu mahiri.

9. Ferran Torres: Manchester City - Barcelona (2022)

Torrees

Chanzo cha picha, Getty Images

Usingetegemea kuona mchezaji akitoka Manchester City yenye kila kitu na mataji juu akielekea Barcelona ambayo inaanza kujitengeneza upya baada ya kizazi chake cha dhabau kikiongozwa na Lionel Messi kutoweka. Lakini pia matatizo ya kifedha inayoyapitia.

Ferran Torres Januari 2022 akaondoka City na kutua Barcelona kwa dau la £54.7m . Ilishangaza.

8. Dusan Vlahovic: Fiorentina - Juventus (2022)

Dusan

Chanzo cha picha, Getty Images

Dunia ilikuwa na jina la Dusan Vlahovic katika ushambuliaji Januari 2022. Alisakwa na kila timu ikiwemo Arsenal iliyokuwa inasaka mshambuliaji baada ya kushindwana na Pierre Aubameyang. Wengi waliamini angetoka nje ya Italia lakini mshambuliaji huyu Muitalia akachagua kuikacha Firentina na kujiunga na wapinzani Juventus kwa ada ya £66.6m.

7. Pierre-Emerick Aubameyang: Borussia Dortmund -Arsenal (2018)

Auba

Chanzo cha picha, Getty Images

Ulikuwa uhamisho mwingine wa kushtua katikati mw amsimu, Borrusia Dortmund wakimuachia nyota wake huyu ambaye alikuwa kwenye ubora wa hali ya juu.

Akawasaidia kutwaa kombe la FA Cup na akafunga mabao yaliyomfanya kupitwa na wachezaji saba tu waliowahi kufunga mabao mengi wakiwa na jezi ya Arsenal. Alitua kwa ada ya £56m.

6. Paulinho: Barcelona - Guangzhou Evergrande (2019)

Paulinho

Chanzo cha picha, Getty Images

Wengi walishangazwa na mbrazil huyu gwiji la zamani la Spurs kusajiliwa na Barcelona akitokea Guangzhou Evergrande tena kwa ada kubwa ya £36m katika dirisha kubwa la Agosti 2017, lakini baadaye Januari iliyofuata walimrudisha kwa mkopo kwa wachina hao ambapo alifanya vyema kabla ya kununuliwa moja kwa moja na kwenda kuwasaidia kutwa taji la ligi.

5. Diego Costa: Chelsea - Atletico Madrid (2018)

costa

Chanzo cha picha, Getty Images

Moja ya wachezaji watukutu uwanjani na nje ya uwanja. Alikuwa mkali wa mabao lakini baadaye hakuonekana kuwa chaguo la kwanza chini ya Antonio Conte pale Chelsea. Kilichoshangazwa ni kuuzwa kwake kwenda Atletico Madrid kwa dau nono la £57m.

4. Fernando Torres: Liverpool - Chelsea

torres

Chanzo cha picha, Getty Images

Ni jambo la kushangaza ukifikiria Fernando Torres amecheza michezo nane zaidi ya ligi kuu England akiwa na Chelsea kuliko idadi ya michezo aliyochezea Liverpool.

Wengi wanamfahamu na alijitambulisha zaidi akiwa na Liverpool lakini miaka yake minne pale Stamford Bridge imempa taji la ligi ya mabingwa Ulaya na kombe la Yuropa. Alionekena mfalme pale Anfield akiwa na kina Steven Gerrard, uhamisho wa kushangaza wa kwa ada ya £50m kuhamia Chelsea tena katika dirisha la Januari unabaki jambo lisilokuwa likitarajiwa na wengi.

3. Virgil van Dijk: Southampton - Liverpool (2018)

Dijk

Chanzo cha picha, Getty Images

Ni beki mzuri, lakini uzuri wake ulifichwa na timu aliyokuwa akiichezea Southampton. Kwa macho ya kawaida usingeona uzuri huo mpaka kwa jicho la ufund. Lakini kuhamia Liverpool kumeoinyesha dunia uzuri wake akiisaidia kutwaa taji la ligi ya mabingwa Ulaya na ligi Kuu.

Akitajwa moja ya mabeki bora katika miaka 5 iliyopita. Kilichoshangaza wengi si yeye kuhamia Liverpool bali ada yake ya uhamisho ya £75m katika dirisha la Januari 2018, ilikuwa kubwa kufikirika kwa uhamisho wa beki. Mpaka wakati huu hiyo ndiyo asda kubwa zaidi kuwahi kutolewa kwa mlinzi katika dirisha la Januari.

2. Philippe Coutinho: Liverpool - Barcelona (2018)

Phillipe

Chanzo cha picha, Ronald Grant

Alikuwa kwenye kiwango bora Liverpool na moja ya viungo bora wakati huo katika ligi kuu England. Haikutarajiwa angehama tena katikati ya msimu, lakini ofa ya £142m ilikuwa ya rekodi na kubwa kwa Liverpool kuikataa . Aliwaliza mashabiki wa Liverpool kwa kuifuata ndoto yake ambayo hata hivyo haikutimia kwani amerejea England akiichezea Aston Villa kwa sasa.

1. Oscar : Chelsea - Shanghai SIPG (2017)

Oscar

Chanzo cha picha, Getty Images

Mpaka leo anasemwa na mpaka leo anajitetea. Oscar alikuwa anafanya vizuri Chelsea, usingedhani angeondoka. Lakini hata kama angeondoka asingeenda China, labda angehamia timu kubwa kubwa ama tiomu za ligi kubwa kubwa Ulaya.

Januari 2017 Chelsea ikapokea ofa yake ya £60m na kutua Shanghai. Wengi wanasema amepotea njia kwenda China na kuacha soka la usnindani ulaya akiwa bado kijana na ana kiwango kizuri. Yeye anasema amwetoka katika familia masikini, ana jukumu la kuingiza fedha kutunza famila yake huko kwao Brazil. Ameshangaza.