Huyu ndiye ''Kizz Daniel'' msanii nyota aliyeshindwa kutumbuiza Tanzania
Na David Nkya
BBC Swahili Dar es Salaam

Chanzo cha picha, KIZZ DANIEL/TWITTER
Katika mitandao ya kijamii mambo mengi sana yalitokea mwishoni mwa juma lililopita katika eneo la Afrika Mashariki.
Pamoja na kwamba uchaguzi mkuu wa Kenya ndio suala linalojadiliwa kwa upana zaidi katika Eneo zima la Afrika Mashariki na maeneo mengine duniani, katika suala la burudani pia yalikuwepo mengi ikiwemo tamasha kubwa la Yanga, baadae likafuata la Simba.
Lakini bila shaka kuna kitu ambacho unatamani nikigusie mbali na hayo niliyoyataja hapo juu, eheee! Hicho hicho. Wengi wanamfahamu kama Kizz Daniel ama Vado, lakini kama yalivyo majina mengine ya kinijeria, jina lake halisi ni refu kidogo alizaliwa Mei 1, 1994 na kupewa jina la Oluwatobiloba Daniel Anidugbe.
Oluwatobiloba ni jina la Kiyoruba analopewa mtoto wa kiume likiwa na maana ya ‘’ Mungu ni mfalme mkuu’’.
Maisha ya muziki

Chanzo cha picha, KIZZ DANIEL/INSTAGRAM
Akiwa amesainiwa na G-Worldwide Entertainment chini ya jina la kisanii Kiss Daniel, alitoa wimbo wake wa kwanza, "Shoye," Mei 2014 kabla ya kujizolea umaarufu nchini Nigeria kwa kuachia wimbo wake wa pili "Woju." Alitoa remix ya wimbo huo hivi karibuni akiwashirikisha nyota wengine kama Tiwa Savage na Davido.
Mwaka 2018, kulikuwa na uvumi kwamba mwimbaji wa YEBA, Oluwatobiloba Anidugbe hatimaye amekubali shinikizo kutoka kwa lebo yake ya zamani ya G-worldwide kuachia jina lake la stejini. Kufuatia ugomvi huo, Tobi ambaye alikua maarufu kwa jina la Kiss Daniel akabadilisha jina la kisanii kwenye majukwaa yote baada ya lebo yake ya zamani kusisitiza kuwa lazima aache kutumia jina hilo, na hapo ndipo ‘’Kizz Daniel’’ ilizaliwa na kutamba zaidi kimataifa.
Kufikia 2022, alikadiriwa kuwa na utajiri unaofikia dola milioni 4.5.
Ameshinda tuzo mbalimbali ikiwemo City People Music Award, Nigeria Entertainment Awards for Afropop, The Hedies Award for Hiphop na nyinginezo nyingi.
Novemba 2017, Kizz Daniel alitangaza kutengana na lebo yake ya rekodi, G-Worldwide na kuunda lebo yake iitwayo FLYBOY I.N.C. Alishtakiwa kortini na lebo yake ya zamani ya rekodi lakini hakupatikana na hatia.
Maisha binafsi

Chanzo cha picha, KIZZ DANIEL/FACEBOOK
Machi 27, 2022, mwimbaji huyo alimtambulisha mama wa watoto wake ambaye hata hivyo hakutaja jina lake. Aliweka picha wakiwa wawili na kumtakia siku njema ya kina mama duniani.
Hii ilikua mara ya kwanza kwa Kizz Daniel kumuonyesha mpenzi wake ambaye hata hivyo alijifunika kwa barakoa hivyo sura yake haikuonekana vizuri. Baadhi ya wafuasi wake wa kike walionyesha hysia tofauti kwa kuwa miongoni mwao wamekua wakimtaka kimapenzi mara kwa mara, linasema jarida la ``The Will’’ la nchini Nigeria.
Nyota huyo wa muziki alifanikiwa kupata mapacha watatu mwezi Mei 2021, lakini mmoja alifariki siku nne baadaye kama ilivyofichuliwa na mwimbaji huyo alipoweka picha ya kwanza kabisa na Jelani na Jalil kwenye Instagram. “Mungu alinibariki na wavulana 3 kitambo Jamal, Jalil na Jelani’’ hii ikiwa ni Siku 4 baada ya kumpoteza mwanae Jamal.
Buga
Kwa sasa Kizz Daniel anatamba zaidi na wimbo wa ``Buga’’ aliouachia May 4, 2022 ambapo video yake aliyomshirikisha msanii mwingine nyota Tekno imefikisha watazamani milioni 44 katika mtandao wa Youtube baada ya kuwekwa kwa June 22, 2022.
Katika mahojiano na blogu moja iitwayo Sunday Scoop, Kizz alisema neno ``Buga’’ maana yake ni kuonyesha mafanikio baada ya kupambana kwa muda mrefu. ``Wengi hawafahamu nilipotoka, namna nilivyopambana kimuziki’’ alisema Kizz Daniel.
Kizz anasema wimbo huu umemtambulisha zaidi kimataifa na kumfanya kupanda katika majukwaa mbalimbali nje ya Nigeria ili kuweza kutoa burudani.
Mikasa

Chanzo cha picha, KIZZ DANIEL/TWITTER
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Vyombo vingi vya habari barani Afrika na sehemu nyingine duniani viliripoti kukamatwa na Polisi nchini Tanzania kwa msanii Kizz Daniel, kosa kubwa likiwa ni kutoonekana ama kushindwa kuburudisha watu waliojitokeza usiku wa Agosti 8 jijini Dar es Salaam. Matokeo ya yeye kushindwa kupanda stejini yalisababisha vurugu na watu kurusha chupa na kuharibu vifaa mbalimbali katika ukumbi wa ``Next Door Arena’’ uliopo Dar es Salaa. Yeye Kizz anasema sababu kubwa ya kushindwa kupanda stejini ni kutokana na kukosa nguo za kutumbuiza baada ya begi lake la nguo kushushwa kimakosa nchini Kenya badala ya Tanzania.
"Nilipofika Nairobi kutoka Kampala ndege niliyotakiwa kuunganisha nayo ilikua imeshaondoka, nilikaa Nairobi kwa saa nane, nikapata ndege nyingine saa mbili na nusu Usiku, Nilipofika Dar tuligundua kwamba vitu vyangu vimesahaulika, wakasema watanitumia’’ alisema Kizz Daniel alipokua akiomba radhi kwa mashabiki zake.
"Waandaaji wa onyesho langu walinihakikishia kwamba ningepata vifaa vingine, nilijaribu kuwasiliana na wabunifu wa mavazi wa hapa ili kupata nguo, lakini haikufanikiwa, tukakubaliana na waandaaji kwamba tutaandaa onyesho jingine’’ aliongeza Kizz Daniel.
Kizz Daniel anasema kwamba alikwenda kuhojiwa na polisi na wala hakukamatwa na hiyo ilikua salama kwake kwani mashabiki walikua na hasira kali juu yake.
Hii ni baada ya video yake akiwa amejifunika usoni chini ya uangalizi wa polisi kusambaa sehemu mbalimbali duniani.
Katika video hiyo, Kizz Daniel anasindikizwa na polisi wa Tanzania kwenye gazi la wazi, huku mtu mmoja akisema, "Kizz Daniel, utaingia gharama kwa hilo. Utaingia gharama kwa kweli. Umesababisha uharibifu katika nchi hii. Lazima uingie gharama kwa ajili yake."
Mratibu wa SUMMER AMPLIFED pia aliomba radhi kwa umma katika taarifa yake. Ilisema, "Big Step Consultancy inapenda kuomba radhi kwa umma kwa kile kilichotokea kwenye tamasha la SUMMER AMPLIFIED linalotarajiwa kufanyika Jumapili, Agosti 7, 2022, ambapo msanii maarufu Kizz Daniel (aliyelipwa fedha zake zote) alishindwa kutumbuiza kama ilivyopangwa."
Hata hivyo tiyari ameahidi kuburudisha mashabiki zake bure siku ya Ijumaa Agosti 12, ili kuweza kufidia hasara walizopata na kusema ataanza kwa kuomba radhi kabla ya kutumbuiza.
Hii ni mara ya pili kwa mwimbaji huyo kushindwa kutumbuiza kwenye tamasha ambalo lililua likisubiriwa kwa hamu na mamia ya mashabiki zake.
Mwezi uliopita aliwafanya mashabiki kusubiri kwa saa nyingi kwenye tamasha lake la DMV huko New York lakini baadaye alilaumu kutoshiriki kwake kwamba kulisababishwa na changamoto za uhamiaji.















