Kwa nini muziki wa Kenya unazidiwa na sauti za Kinaijeria

TH

Chanzo cha picha, AFP

Iliyochapishwa

Matatu mashuhuri, au teksi za basi dogo, za mji mkuu wa Kenya, mara nyingi hupitia msongamano wa magari kwa mipigo ya sauti ya muziki wa Afrobeat wa Nigeria, Bongo Flava ya Tanzania au Amapiano ya Afrika Kusini.

Ondoka kwenye gari na nyimbo za kigeni zinavuma kupitia spika za wachuuzi wa mitaani.

Na vivyo hivyo kwenye redio, nyimbo zinazochezwa zaidi ni nadra sana kutoka Kenya.

Kuongezeka kwa tasnia ya muziki wa pop barani Afrika kumekuwa jambo la fahari kwa bara hilo, lakini nchini Kenya pia kumezua wasiwasi kwamba wanamuziki wa humu nchini wanabanwa.

Baadhi katika tasnia hiyo wanasema talanta mpya za Wakenya hazipewi nafasi ya kupenya.

Suluhu moja kubwa ni kuongeza kiwango cha muziki wa Kenya kwenye vituo vya redio kutoka asilimia 40 ya sasa, iliyokubaliwa mwaka wa 2014, hadi 75% ya nyimbo zilizopeperushwa.

TH
Maelezo ya picha, Mcheshi Eric Omondi aliketi kwenye kisanduku cha vioo nje ya bunge ili kutangaza harakati zake za kutaka muziki zaidi wa humu nchini kwenye redio

Shughuli hiyo inaongozwa na mcheshi maarufu nchini, Eric Omondi, ambaye hivi majuzi alifanya maandamano nje ya bunge huku akiwa amefungiwa kwenye kisanduku cha kioo kilichoandikwa maneno "cheza 75% ya Kenya".

Wabunge kadhaa walionyesha kuunga mkono msukumo wake, akiwemo John Kiarie, mcheshi wa zamani, ambaye baadaye alilitaka bunge "kufungua" uwezo wa sekta ya Uchumi wa sanaa wa Kenya kwa kuidhinisha pendekezo hilo.

"Ninasukuma vipaji zaidi vijavyo kuonyeshwa kwenye redio na TV. Ninataka kuhakikisha vijana wetu wanapata nafasi hewani na kujenga chapa zao na kujitegemea," Omondi aliambia BBC Swahili.

Lakini idadi ya sasa ya 40% tayari ni kiasi kikubwa na kuna maswali ni kwa nini, kutokana na fursa hii , wanamuziki wa Kenya wanaendelea kutatizika.

Moja ya ugumu ni kwamba uchezaji zaidi wa muziki hewani haujaleta mapato zaidi kwa wasanii.

Ukosefu wa mirabaha

Tatizo ni kwamba vituo vya redio Kenya, huku vikizingatia mgao huo, vimekuwa vikisita kulipa mirabaha.

Kesi za mahakama za kupinga kutolipa huku zimeendelea kwa miaka mingi.

"Tunakusanya takriban 20% tu ya mirahaba," alisema Peter Inyenze, mkuu wa Jumuiya ya Hakimiliki ya Muziki ya Kenya - chombo kinachowakilisha wamiliki wa hakimiliki za muziki.

"Hili limekuwa tatizo nchini Kenya kwa miaka mingi. Vituo vya redio vimekuwa vikisema kwamba havina pesa na biashara haikuwa nzuri."

Amri ya rais mwaka jana ilijumuisha malipo ya mirabaha kama sharti la kuongezwa kwa leseni za utangazaji - ili mambo yabadilike.

Bw Inyenze alisema kwa sasa amekuwa akipata mawasiliano kutoka kwa vituo hivyo kuhusu kulipa mirahaba yao ambayo haijasalia.

Lakini, labda kwa sababu ya ukosefu wa pesa, pia kuna swali la kama kuna muziki mpya wa ubora wa kutosha wa Kenya unaotayarishwa kujaza kiwango kilichopendekezwa.

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwanamuziki wa Nigeria Burna Boy ni mtumbuizaji wa kila mara nchini Kenya

Ili kukabiliana na changamoto ya Afrobeats na Bongo Flava, baadhi ya wanamuziki wa hapa nchini wametumia lafudhi za Afrika Magharibi kwa Kiingereza, au jinsi Watanzania wanavyozungumza Kiswahili. Ishara ya wasiwasi kwa baadhi ya kupoteza kujiamini na uhalisi.

Lakini wana chaguo gani ikiwa wanataka kushindana?

Tamasha za mara kwa mara zinazoonekana nchini Kenya za mastaa wa Nigeria kama Davido, Burna Boy na Omah Lay, na Diamond Platnumz wa Tanzania, Rayvanny na Harmonize huzua tafrani miongoni mwa mashabiki wao wa hapa nchini.

Ikiwa na idadi ya watu milioni 54, Kenya inapaswa kuwa na nguvu za kiuchumi na kitamaduni ili kuzalisha nyota wa nyumbani ambao wanaweza kufika kusini na magharibi katika bara zima.

Lakini ingawa muongo au zaidi uliopita muziki wa Kenya - kupitia aina ya hip-hop ya Kapuka - ulikuwa ukivutia kimataifa, hii sasa imeshuka.

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Sauti Sol ni mojawapo ya wasanii wachache Wakenya kujitokeza katika bara zima

Mtendaji mkuu wa muziki Agnes Nonsizi anaamini kwamba ilipobadilika na kuwa Gengetone, ambayo iliathiriwa na dancehall na reggaeton, utambulisho wa kipekee wa pop uliondolewa - kuruhusu kuingia kwa sauti kutoka Nigeria na Tanzania.

Kumekuwa na baadhi ya mastaa kama Sauti Sol, Khaligraph Jones na Nameless. Lakini hadithi za mafanikio zimekuwa chache na wengi wamejitahidi kupata pesa kutoka kwa talanta yao.

Mtangazaji wa muziki Bilha Nguraiya ana maneno makali kwa wanamuziki wengi wa Kenya ambao anadhani "hawataki kushindana na kujipima" na nyota hao wa bara.

"Muziki ulikuwa njia ya baadhi yao kuondokana na umaskini. Na sasa wanaogopa sana kutoka katika eneo lao la starehe kwa sababu inaweza kukasirisha mlinganyo - hawajui bora na wanaogopa kuhatarisha," aliambia BBC.

Maneno machafu

Pamoja na ukosefu ari ya kutaka kuafikia makubwa na ujuzi wa kibiashara miongoni mwa wanamuziki, pia kuna swali la utambulisho na jinsi mashabiki wa ndani wanavyopata muziki.

Mwanafunzi wa chuo kikuu Priscilla Awino anaeleza kuwa anapendelea zaidi muziki wa Bongo wa Tanzania kwa sababu ya Kiswahili cha "mashairi".

"Siwezi kuhusiana na ujumbe katika Afrobeats lakini ni ya kuburudisha, napenda mdundo, lafudhi ya pijini na ninazipata kuwa za kitamaduni - unaweza kusema kuwa hii ni ya Kiafrika kabisa."

Wengine wanasema kuwa sababu moja ya Wakenya kutokuwa na uhusiano mkubwa na muziki wa humu nchini ni kwa sababu hauna msingi thabiti wa kitamaduni, lakini Nguraiya hakubaliani na hilo.

"Muziki wetu una utambulisho, ni kweli. Lakini ni watumiaji wa Kenya ambao wana shida na utambulisho. Wasanii ni kioo cha jamii, lakini hatupendi tu tunachokiona kwenye kioo," alisema.

Pia kuna mwelekeo unaokua miongoni mwa wanamuziki wajao wa usherati, hadithi za uzushi za vurugu za magenge na mabishano ambayo huwaweka ghafla katika uangalizi kabla ya kuyumba na kutoweka hivi karibuni.

Haishangazi baadhi ya vilabu vya humu nchini havichezi muziki wa Kenya na ni nadra kupata wageni wao wakiomba muziki wa Kenya, kulingana na DJ Sashi Diva.

"Nyimbo zinatazamwa na mamilioni ya watu kwenye YouTube lakini huwezi kuzicheza kwenye klabu kwa sababu si kila jambo lenye utata litatumika. Hapo ndipo Wanigeria na Watanzania walipotushinda," alisema.

Na hii yote inarejelea ni vituo gani vya redio vimetayarishwa kucheza na kama vinaweza kujaza nafasi ya 75%.

Vyombo vya habari tayari vimetoa wasiwasi kuhusu pendekezo hilo. Wanasema kuwa vituo vya redio vinapaswa kutangaza kile watazamaji wanataka ili kuendelea kuishi.

Ingawa vituo vya redio vya lugha za asili za Kenya hucheza zaidi muziki wa humu nchini, stesheni za kitaifa ambazo huvutia hadhira kubwa zaidi hustawi kutokana na maudhui ya kigeni.

Gazeti la The Star - linalomilikiwa na Kundi la Radio Africa ambalo lina vituo sita vya redio za kitaifa - lilibishana katika tahariri ya hivi majuzi dhidi ya hitaji la sheria mpya kwani "itapunguza aina mbalimbali za pato la TV na redio za Kenya".

"Wacha TV na redio zishindane kwa watazamaji kwa kutoa maudhui ya ndani na kimataifa katika vibali tofauti," ilisema.

Tamaa ya kuunga mkono wasanii wa humu nchini inaweza kuwashawishi baadhi ya wabunge kuunga mkono mabadiliko ya mgao, lakini hatimaye inaweza kufaulu kidogo ikiwa Wakenya wataendelea kupendelea sauti za kigeni.

Nchini kote, wasikilizaji wanapiga kura kwa masikio yao, na kwa sasa Afrobeat na Bongo Flava ni vipendwa vya wazi.