Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Tulidhani ni mpira' - Mabomu yanayowaua na kuwajeruhi watoto
- Author, Soutik Biswas, Nupur Sonar & Tanushree Pandey
- Nafasi, BBC World Service
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 9
Katika miongo mitatu iliyopita, angalau watoto 565 katika jimbo la West Bengal, nchini India, wamejeruhiwa au kuuawa na mabomu ya kutengenezwa nyumbani, kulingana na uchunguzi wa BBC Eye.
Tunauliza ni vifaa gani hatari hivi na vimehusianaje na vurugu za kisiasa katika eneo hili?
Na kwa nini watoto wengi wa Bengal wanadhulumika kutokana na kadhia hii?
Asubuhi ya mwezi Mei 1996, wavulana sita kutoka mtaa wa mabanda wa Kolkata, mji mkuu wa jimbo la West Bengal, walikuwa wakicheza mchezo wa kriketi uwanja ulio karibu na makaazi yao.
Shughuli za kawaida zilikuwa zikinoga katika mtaa huu wa mabanda uliokuwa umepakana na mtaa wa walio na kipato cha juu katika bustani ya Jodhpur.
Ilikuwa ni likizo- siku ambayo uchaguzi mkuu ulikuwa unafanyika.
Puchu Sardar, mvulana wa miaka tisa, aliyekuwa miongoni mwa wavulana hao alichukua gongo la kriketi na kuondoka pole pole asimuamshe babake aliyekuwa amelala chumbani.
Dakika chache tu, mchezo wa kriketi ukaanza.
Mpira wa kriketi ulianguka na kutoka nje ya mipaka ya uwanja wao wa mpira na wavulana hao wakaamua kwenda kuutafuta katika bustani iliyokuwa karibu na makaazi yao.
Katika pilka pilka za kusakanya mpira ili waendelee na mchezo wao, waliona mfuko wa plastiki wa rangi nyeusi uliokuwa na vipira vya mviringo visita.
Vipira hivyo vilikuwa na muundo sawia na mpira wa kriketi wakadhani wamepata bahati na kurejea kuendelea kucheza.
Puchu alichukua mpira mmoja kutoka kwa waliookota na kuupiga na gongo la kriketi.
Punde si punde mlipuko wa kishindo ulisikika katika eneo waliokuwa wakichezea. Liikuwa ni bomu.
Wakati moshi ulipofuka majirani walikimbia nje kubaini kilichotokea, walikuta Puchu na wenzake watano wakiwa wamezimia , ngozi zao zimebadilika rangi na kuwa za buluu, mavazi yao yameteketea, na miili yao imepata majeraha makubwa.
Hali ya simanzi iligubika mtaa huo wa mabanda .
Watoto wawili, Raju Das mwenye umri wa miaka saba, ambaye alikuwa yatima na kulelewa na shangazi yake, na Gopal Biswas mwenye umri wa miaka saba, walifariki kutokana na majeraha yao.
Wavulana wanne walijeruhiwa.
Puchu alinusurika kifo, baada ya kupata majeraha makubwa ya moto kifuani, usoni na pia tumboni.
Puchu alihudumiwa hospitalini kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Aliporejea nyumbani, alilazimika kutumia kishikio cha jikoni na kuanza kutoa vipande vya bomu vilivyokuwa vimeingia mwilini mwake kwa sababu familia yake haikuwa na uwezo wa kumudu gharama ya matibabu.
Puchu na wenzake ni miongoni mwa watoto waliouwa au kujeruhiwa na mabomu , ambayo yamekuwa yakitumika katika jimbo la West Bengal kwa miongo kadhaa katika vita vikali vya kisiasa.
Kufikia sasa hakuna idadi kamili ya majeruhi wa mabomu hayo ya kutengenezwa nyumbani katika eneo la West Bengal.
Hivyobasi idhaa ya BBC Word service ililazimika kuchambua nakala zote za magazeti mawili maarufu ya jimbo hilo- Anandabazar Patrika na Bartaman Patrika - kutoka mwaka 1996 hadi 2024, kutafuta ripoti kuhusu watoto waliouawa au kujeruhiwa na mabomu haya.
Tumegundua kwamba watoto angalau 565 walikufa au kujeruhiwa - vifo 94 na majeraha 471 - hadi mwezi Novemba 10. Hii ina maana kwamba mtoto mmoja anakuwa mhasiriwa wa mlipuko wa mabomu kila baada ya siku 18.
Hata hivyo, BBC imebaini kuwa kuna visa vya watoto walioumizwa katika mlipuko wa mabomu ambayo havikujumuishwa katika magazeti haya, ikiwa na maana kuwa idadi ya majeruhi wa mabomu haya ni ya juu zaidi kuliko tunachokijua.
Zaidi ya asilimia 60% ya visa hivi vilihusisha watoto wakicheza nje ya makaazi yao- ima katika bustani, mtaani, mashambani, au hata karibu na shule - ambapo mabomu, ambayo hutumika mara nyingi wakati wa uchaguzi kutisha wapinzani, yalifichwa.
Wengi wa wahanga ambao BBC ilizungumza nao walikuwa kutoka familia za kimaskini, watoto wa wafanyakazi wa nyumba, vibarua, au wafanyakazi wa mashamba.
Historia ya mapinduzi ya mabomu huko West Bengal
West Bengal,ni jimbo la nne kwa ukubwa nchini India lenye idadi ya watu zaidi ya milioni 100, limekuwa likikumbwa na vurugu za kisiasa kwa muda mrefu.
Kwa miaka mingi, tangu uhuru wa India mwaka 1947, jimbo hili limepitia viongozi mbalimbali - chama cha Congress kwa miongo miwili, Chama cha Kikomunisti kilichokuwa kikiungana na upande wa kushoto kwa miaka mitatu, na sasa Chama cha Trinamool Congress tangu mwaka 2011.
Mwisho wa miaka ya 1960, jimbo hili lilikumbwa na mapigano makali kati ya waasi wa Maoist – pia wanajulikana kama Naxalites – na vikosi vya serikali.
Ukimya wa kisiasa na mapigano ya waasi tangu wakati huo umehusisha matumizi ya mabomu kama zana za kutisha wapinzani kuacha domo la kisiasa, hasa wakati wa uchaguzi.
"Mabomu yamekuwa yakitumika kulipana visasi vya kisiasa. Hii imekuwa ikitokea Bengal kwa muda mrefu, zaidi ya miaka 100," alisema Pankaj Dutta, aliyekuwa Mkuu wa Polisi wa West Bengal.
Utengenezaji wa mabomu nyumbani huko Benga ulikita mizizi wakati wa upinzani dhidi ya utawala wa Waingereza miaka ya 1900.
Juhudi za awali bomu haikuwa inaafiki viwango na ajali zilitokea kila mara:muasi mmoja alipoteza mkono na mwingine akafariki alipokuwa akijaribu bomu aliyokuwa ameitengeneza.
Kisha muasi mmoja alirejea India kutoka Ufaransa akiwa na maarifa zaidi kuhusu utengenezaji wa bomu.
Kitabu chake kilicho na taarifa kuhusu bomu- kitabu cha kisheria kilichojazwa na milipuko kilichofichwa kwenye kikebe cha kakao - kingeliua mlengwa, hakimu wa Kiingereza, kama angefungua kitabu hicho.
Mlipuko wa kwanza ulitikisa wilaya ya Midnapore mwaka 1907, wakati wanamapinduzi walipolipua treni iliyokuwa imebeba afisa wa serikali ya waingereza kwa kutega bomu kwenye reli.
Miezi michache baadaye, jaribio ambalo halikufua dafu la kumuua hakimu huko Muzaffarpur kwa kutupa bomu kwenye gari la farasi lilisababisha vifo vya wanawake wawili raia wa Uingereza.
Kisa hicho, ambacho kilielezewa na gazeti kama "mlipuko mkubwa ulioacha mji ukiwa na mshtuko," kilimgeuza Khudiram Bose, mzalendo mchanga, kuwa shahidi na kuwa mpiganiaji uhuru wa kwanza katika orodha ya wanamapinduzi wa India.
Bal Gangadhar Tilak, kiongozi wa kitaifa, aliandika mwaka 1908 kwamba mabomu hayakuwa tu silaha bali ni aina mpya ya "maarifa mengi," aina ya "uchawi" unaosambaa kutoka Bengal hadi sehemu nyingine za India.
Leo hii, mabomu ya kizamani ya Bengal yanajulikana kama peto.
Yamefungwa kwa nyuzi za pamba na kujazwa na vipande vya marisau ya misumari kioo na nati.
Tofauti zake ni pamoja na milipuko inayozungushwa kwenye vyombo vya chuma au chupa za kioo.
Mabomu haya hutumika hasa katika mapigano ya kikatili kati ya vyama vya kisiasa pinzani.
Wanaharakati wa kisiasa, hasa katika maeneo ya vijijini, hutumia mabomu haya kuwafedhehesha wapinzani, kuvuruga vituo vya kupigia kura, au kulipiza kisasi dhidi ya mahasimu wa kisiasa.
Mara nyingi hutumika wakati wa uchaguzi ili kuharibu vituo vya kupigia kura au kudhibiti maeneo fulani.
Watoto kama vile Poulami Halder wanamakovu ya vita hivyo vya kisiasa vya kutumia mabomu.
Alfajiri ya mwezi Aprili mwaka 2018 , akiwa na miaka saba wakati huo alikuwa akichuna maua ya kutumika katika ibada za asubuhi huko Gopalpur, kijiji kiliko kaskazini mwa 24 Parganas kilichojaa vidimbwi na minazi.
Uchaguzi wa baraza la kijiji ulikuwa unatarajiwa kufanyika ndani ya mwezi mmoja.
Poulami aliona mpira ukiwa umeachwa karibu na mfereji wa jirani.
"Niliuchukua na kurudi nao nyumbani," anakumbuka.
Alipofika nyumbani, babu yake, akila staftahi, alisimama kwa mshangao alipoona kitu hicho mikononi mwake.
"Alisema, 'Huu si mpira - ni bomu! tupa mbali sana!' Kabla sijajua nini cha kufanya, lililipuka mikononi mwangu."
Mlipuko wa bomu uligeuza utulivu wa kijiji kuwa purukushani.
Poulami aligongwa kwenye "macho, uso, na mikono" na kuzimia, huku athari za bomu hilo zikiendelea.
"Nakumbuka watu wakikimbia wakinifuata nilipokuwa nimeanguka, lakini sikuona vizuri. Nilikuwa nimejeruhiwa kila mahali."
Wakazi wa kijiji walimkimbiza hospitalini.
Majeraha yake yalikuwa makubwa – mkono wake wa kushoto ulitolewa na alikaa hospitalini kwa karibu mwezi mmoja.
Mazoea yake ya kila asubuhi yaligeuka kuwa ndoto mbaya, ikibadilisha maisha ya Poulami milele kwa tukio moja la kushtua.
Poulami sio yeye peke yake.
Sabina Khatun akiwa na miaka kumi alilipukiwa na bomu la kutengenezea nyumbani mikononi mwake mwezi Aprili mwaka 2020 huko Jitpur,kijiji kinacholima mchele katika wilaya ya Murshidabad.
Alikuwa ameenda malishoni ambapo alikuta bomu lilikuwa limetegwa ardhini.Akitaka kujua zaidi na kuanza kuchezea.
Dakika chache baadaye,ililipukia mikononi mwake.
" Niliposkia mlipuko,nilifikiria ni nani atajeruhiwa tena? Je Sabina amelemazwa? ''mamake , Ameena Bibi, akiongea akiwa na maumivu makali.
''Nilipotoka nje niliona Sabina akiwa amebebwa na wasamaria wema. Kidonda kilikuwa dhahiri mkononi.''
Madaktari walilazimika kumkata Sabina mkono.
Tangu arejee nyumbani,amehangaika kuendelea na maisha yake ya kawaida, huku wazazi wake wakiwa na wasiwasi kuhusu maisha yake ya usoni.
Hofu yao inakubalika:nchini India, wanawake ambao wanauwezo maalum hukabiliwa na unyanyapaa hasa katika masuala ya ndoa na kazi .
''Mtoto wangu alikuwa akilia kila mara,akisema hatawahi kuwa na mkono tena,''anasema Ameena.
''Nilikuwa namliwaza,nikimwambia,mkono na vidole vyake vitamea tena.''
Sasa Sabina anang'ang'ana baada ya kukatwa mkono ambao unamnyima kutekeleza majukumu ya msingi. ''Nateseka kujinywisha maji ,kula ,kuoga,kuvaa nguo na pia kwenda msalani.''
Watoto hawa, ambao wamejeruhiwa na mabomu lakini ni wenye bahati kuwa hai, maisha yao yamebadilika milele.
Poulami, ambaye sasa ana umri wa miaka 13, alipokea mkono bandia lakini hakuweza kuutumia – ulikuwa mzito na haukuchukua muda mrefu kabla ya kujaa na kuwa mkubwa kupita kiasi.
Sabina, mwenye umri wa miaka 14, ana matatizo ya macho.
Familia yake inasema inahitaji upasuaji mwingine wa kuondoa mabaki ya bomu kwenye macho yake, lakini hawawezi kumudu gharama hiyo.
Puchu, ambaye sasa ana miaka 37, alikola masomo baada ya wazazi wake kujawa na hofu alipokataa kutoka nje kwa miaka mingi, mara nyingi akijificha chini ya kitanda chake kila aliposikia kelele kidogo.
Hajarejelea mchezo alioupenda wa Kriketi.
Hakufurahia utoto wake na sasa anajikimu na kazi za ujenzi zisizo na uhakika na anabeba makovu ya maisha yake ya nyuma.
Lakini bado wana matumaini.
Poulami na Sabina wamejifunza kuendesha baiskeli kwa mkono mmoja na wanaendelea kwenda shuleni.
Wote wanatamani kuwa walimu.
Puchu anatumaini maisha bora kwa mtoto wake, Rudra, mwenye umri wa miaka 5, – maisha ya baadaye akimtakia awe afisa wa polisi.
Licha ya madhara makubwa yanayotokana na matumizi ya mabomu ya kizamani,hakuna dalili za kumalizika kwa vurugu za mabomu huko West Bengal.
Hakuna chama chochote cha kisiasa kinachokubali kutumia mabomu kwa faida za kisiasa.
Wakati BBC ilipouliza vyama vikuu vinne vya kisiasa huko West Bengal ikiwa vimehusika, moja kwa moja au kupitia wasaidizi, katika utengenezaji au matumizi ya mabomu ya kizamani, chama cha Trinamool Congress (TMC) kilichoko madarakani na chama cha upinzani cha Bharatiya Janata Party (BJP) hakikujibu.
Chama cha Communist Party of India (Marxist) (CPI-M) kilikanusha vikali kuhusika, na kusema kuwa "kimejizatiti kudumisha utawala wa sheria… na kwamba linapohusiana na kulinda haki na maisha, watoto ndio kipaumbele kikuu."
Chama cha Indian National Congress (INC) pia kilikanusha vikali kutumia mabomu ya kizamani kwa faida ya uchaguzi, na kusema hakijawahi kujihusisha na vurugu za kisiasa au za kibinafsi.
Ingawa hakuna chama chochote cha kisiasa kinachokubali kuwajibika, hakuna mtaalamu mmoja aliyezungumza na BBC ambaye anashuku kuwa mauaji haya yana mizizi katika utamaduni wa vurugu za kisiasa za Bengal.
"Wakati wowote wa uchaguzi mkuu hapa, utaona matumizi ya mabomu yakikithiri," alisema Pankaj Dutta. "Uonevu wa watoto unafanyika. Ni ukosefu wa utunzaji kutoka kwa jamii." Bwana Dutta alifariki mwezi Novemba.
Poulami anasema: "Wale waliotega mabomu bado wako huru. Hakuna mtu anapaswa kuacha mabomu yakitapakaa kila mahali. Ikiwa hivi hakuna mtoto anayeweza kujeruhiwa tena kama hivi."
'Angalia walivyomfanya mtoto wangu'
Lakini visa kama hivi vya kikatili vinaendelea.
Mwezi Mei mwaka huu, katika wilaya ya Hooghly, wavulana watatu waliokuwa wakicheza karibu na dimbwi la maji walikutana na hifadhi ya mabomu bila kujua.
Mlipuko ulimuua Raj Biswas, mwenye umri wa miaka tisa, na kumjeruhi rafiki yake, ambaye alikatwa mkono wake baada ya kujeruhiwa vibaya.
Mvulana mwingine alidanganya kifo lakini alijeruhiwa miguuni.
"Angalia walivyomfanya mtoto wangu," baba wa Raj aliomboleza kwa huzuni huku akigusisha kipaji cha mtoto wake aliyekufa.
Wakati mwili wa Raj uliposhushwa kaburini, matangazo ya kisiasa yaliguswa hewani kutoka kwa mkutano wa uchaguzi ulio karibu: "Heri Bengal!" watu walikuwa wakisema kwa sauti, "Heri Bengal!"
Ilikuwa ni wakati wa uchaguzi. Na tena, watoto walikuwa wakiendelea kudhurika na yanayoendelea ya uhasama wa kisiasa.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid