Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Ukraine: Raia waukimbia mji wa Kherson huku Urusi ikiongeza mashambulizi zaidi
Nika Selivanova mwenye umri wa miaka kumi na tatu alitengeneza umbo la moyo kwa mikono yake yote miwili, akimuaga rafiki yake mkubwa Inna ambaye alikuwa upande wa pili wa uzio wa kiooo uliotenganisha eneo la kuingia kwenye kituo cha treni cha Kherson na eneo la kusubiria ama kungojea abiria.
Muda mfupi kabla, walikuwa wamekumbatiana, machozi yakiwatoka machoni mwao. Inna alikuwa amembusu Asia, mbwa aliyefunikwa kwenye blanketi yenye joto, iliyekuwa amebebwa na Nika. Wasichana hawa hawakujua ni lini wangeonana tena. Familia ya Nika ilikuwa ikiondoka Kherson, bila uhakika wa hatima yao.
Kwa sasa, walikuwa wakielekea katika jiji la magharibi la Khmelnytskyi, wakitumaini kwamba wangepata msaada huko.
Siku chache zilizopita huko Kherson zilikuwa siku ngumu kwa mama yake Nika anayeitwa Elena.
"Hapo awali, [vikosi vya Urusi] vilitupiga kwa makombora mara saba hadi 10 kwa siku, sasa ni mara 70-80, kwa siku moja. Inatisha sana." Elena alisema.
"Ninaipenda Ukraine na mji wangu pendwa. Lakini inabidi tuondoke." Elena na binti zake watatu ni miongoni mwa zaidi ya watu mia nne ambao wameondoka Kherson tangu Siku ya Krismasi, baada ya kuongezeka kwa kasi ya mashambulizi ya mabomu katika jiji hilo kutoka jeshi la Urusi. Elena aliondoka kwa treni, katika uokoaji uliowezeshwa na serikali ya Ukraine.
Mamia ya watu wanakimbia wenyewe, foleni ya magari kwenye kituo cha ukaguzi kinachotoka Kherson, yakiwa yamejaa raia waliojawa na hofu.
Iryna Antonenko alitokwa na machozi tulipokaribia gari lake ili kuzungumza naye. 'Hatuwezi kuivumilia tena. Mashambulizi ni makali sana. Tulikaa muda huu wote na tukadhani itapita na kwamba tungekuwa na bahati. Lakini kombora lilipiga nyumba iliyo karibu na yetu, na nyumba ya baba yangu pia ilipigwa makombora, "alisema. Alipanga kusafiri hadi Kryvyi Rih, jiji lililo katikati mwa Ukraine ambako ana ndugu huko.
Mwezi uliopita tu, kumekuwa na matukio ya kadhaa huko Kherson. Mji huo ulitekwa na vikosi vya Urusi siku ya pili ya uvamizi, mwezi Februari, 2022 lakini ulikombolewa mnamo Novemba 11.
Karibu na mahali ambapo umati wa watu walikuwa wamekusanyika wakipeperusha bendera za Ukraine kusherehekea kukombolewa kwa mji huo kutoka kwenye udhibiti wa Urusi, shambulio la usiku wa mkesha wa Krismasi lilisababisha vifo vya watu kumi na mmoja, na kadhaa kujeruhiwa.
Miongoni mwa waliofariki ni mfanyakazi wa kijamii, mchinjaji na mwanamke anayeuza kadi za simu za mkononi - watu wa kawaida wanaofanya kazi au kutembelea mara kwa mara kwenye soko kuu la jiji hilo.
Siku hiyo, mji wa Kherson ulishambuliwa mara 41 na makombora, kwa mujibu wa serikali ya Ukraine. Warusi wanashambulia kutoka upande wa kushoto (mashariki) wa mto Dnipro, ambako walikimbilia huko; njia ya maji imekuwa muhimu kusini mwa Ukraine.
Kherson ni eneo muhimu la kimkakati, ambalo mara nyingi huitwa lango la Crimea. Wachambuzi wengi wanasema kwamba Urusi sasa imelazimishwa kuongeza nguvu ya kulinda eneo hilo. Ni vigumu kuona inachotarajia kupata kutokana na kushambuliwa kwa Kherson.
Mbali na makombora, tumeona pia risasi za moto zikitumika - cheche za moto zinasambaa kila kona ya jiji. Haijulikani pia ikiwa wanajeshi wa Ukraine wanajaribu kurudisha udhibiti wa maeneo ya ukingo wa kushoto wa mto.
Hapa jijini, hakuna muda wa kupumzika kutokana na sauti ya mara kwa mara za mashambulizi ya makombora. Serhii Breshun, 56, aliuawa alipokuwa amelala. Aliangukiwa na nyumba yake baada ya bomu kutua.
Siku moja baada ya kifo chake, tulikutana na mama yake, Tamara, mwenye umri wa miaka 82, ambaye alikuja kutafuta pasipoti yake kwenye vifusi. Alihitaji hati hiyo ili mwili wake utolewe katika chumba cha kuhifadhia maiti.
"Nilikuwa na hisia kwamba kuna kitu kingeenda vibaya siku hiyo. Kwa sababu nilizungumza naye [kwa simu] na kumsihi aondoke nyumbani. Hakutoka na ikawa hivyo. Maisha yetu yameharibiwa," alisema huku akilia. Hatukuwa tumemaliza kuzungumza naye, na kulikuwa na milipuko mikubwa zaidi. Harakati za pekee za mama huyo mzee kumzika mwanae kwa heshima ni hatari, kwa sababu hakuna sehemu ya Kherson iliyo salama.
Kuishi hapa, iwe nje barabarani au ndani ya nyumba, ni suala la bahati nasibu. Mfanyakazi wa kujitolea wa Msalaba Mwekundu Viktoria Yaryshko mwenye umri wa miaka 39 aliuawa katika mlipuko wa bomu nje kidogo ya kituo cha shirika hilo huko Kherson, mita chache kutoka eneo salama.
Mama yake Liudmyla Berezhna alituonyesha medali ya heshima aliyopewa Viktoria. "Nimefurahi sana kuwa alisaidia watu wengi. Alikuwa mkarimu sana. Lakini pia inaniuma, lazima nipone na kuwalea watoto wake wawili, nawaambia wajivunie mama yao kwa sababu ni shujaa," alisema. " alisema.
Viktoria alikuwa akiishi chini ya ardhi, eneo maalumu la usalama la Msalaba Mwekundu akiwa na watoto wake wawili - Alyonushka mwenye umri wa miaka 17 na Sasha wa miaka 12 ambao wanaendelea kuishi huko, wakiwa na faraja na ulinzi kutoka kikundi cha watu waliojitolea ambao wamekuwa familia.
'Wakati mtu wa karibu sana anakufa, ni ngumu. Lakini ikiwa tutakata tamaa na kuacha, basi kifo chake kingekuwa bure. Tunafanya kazi ili kuhakikisha watu wanaishi. Vigine vitafuata, "Dmitro Rakitskyi, rafiki wa Viktoria na mfanyakazi mwingine wa kujitolea alisema.
Lakini ni vigumu kufanya hivyo kujua familia yako inaweza kuwa hatarini kila dakika. Muda mchache baadaye, mabomu zaidi yanaporushwa, Dmitro anapiga hatua huku na huko akijaribu kumwita mkewe, hali ya wasiwasi ikionekana usoni mwake. Ana watoto wawili.
"Hawataki kuondoka. Wananihangaikia, na mimi nina wasiwasi nao. Ndivyo tunavyoishi," alisema.
"Kinachonikera zaidi ni kwamba wao [vikosi vya Urusi] kila mara hushambulia miundombinu ya kiraia. Nyumba, nyumba za ghorofa. Ni ngumu kuelewa nini mantiki nyuma ya mashambulizi haya," Dmitro alisema.
"Hatuna umeme au maji kabisa. Hupatikana kwa muda mfupi wakati mwingine na hatupati kabisa kwa sababu ya makombora. Inatisha sana usiku. Hata hivyo tuna gesi, inatusaidia," mkazi mmoja, Larysa Revtova, alisema.
Makumi kwa maelfu ya raia bado wanaishi Kherson, lakini angalau mara mbili wiki hii utawala wa kikanda umewahimiza kuondoka. Ni jiji linaloandamwa na mashambulizi ya kiholela ya Urusi.