Unajua makelele yanavyokuua polepole?

.
Maelezo ya picha, James Gallagher akirekodi viwango vya sauti karibu na mji wa Barcelona
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Tumezungukwa na muuaji asiyeonekana. Moja ya vitu vya kawaida vinavyotufanya tusitambue kwamba vinafupisha maisha yetu.

Vinasababisha mshtuko wa moyo, kisukari cha aina ya 2 na tafiti sasa zinaihusisha na shida ya akili.

Je unafikiri inaweza kuwa nini?

Jibu ni kelele - na athari zake kwa mwili wa binadamu huenda mbali zaidi ya kuharibu kusikia.

"Ni janga la afya ya umma, kuna idadi kubwa ya watu wanaoathiriwa katika maisha yao ya kila siku," anasema Prof Charlotte Clark, kutoka St George's, Chuo Kikuu cha London.

Ni tatizo tusilolizungumzia.

Kwa hivyo nimekuwa nikichunguza wakati kelele inakuwa hatari, nikiongea na watu ambao afya zao zinaathiriwa ili kuona ikiwa kuna njia yoyote ya kukabiliana na ulimwengu wetu wenye kelele.

Nilianza kwa kukutana na Prof Clark katika maabara ya sauti ya kutisha. Tutaona jinsi mwili wangu unavyoitikia kelele na nimepewa kifaa kinachofanana na saa na kitapima mapigo yangu ya moyo na jinsi ngozi yangu inavyotoka jasho.

Unaweza kujiunga pia ikiwa una vipokea sauti vya masikioni. Fikiria jinsi sauti hizi tano zinakufanya uhisi.

Maelezo ya video, Sikiliza sauti tofauti za kelele katika chini ya dakika moja. Je, zinakufanya uhisi vipi?

Sauti kali zaidi ninayosikia ni ile ya kelele za trafiki kutoka Dhaka, Bangladesh, Mji ulio na jina la jiji lenye kelele zaidi ulimwenguni. Mara moja ninahisi kama niko kwenye msongamano mkubwa wa magari.

Na vitambuzi vinachukua msukosuko wangu - mapigo ya moyo wangu yanapanda na ngozi yangu inatoka jasho zaidi.

"Kuna ushahidi mzuri kwamba kelele za msongamano huathiri afya ya moyo wako," asema Prof Clark, huku sauti inayofuata ikiandaliwa

Ni sauti za furaha tu za uwanja wa michezo ambazo zina athari ya kutuliza mwili wangu. Lakini mbwa wakibweka na sauti za karamu ya jirani katika masaa ya alfajiri husababisha majibu hasi.

Lakini kwa nini sauti inabadilisha mwili wangu?

"Una jibu la kihisia kwa sauti," anasema Prof Clark.

Sauti hugunduliwa na sikio na kupitishwa kwenye ubongo na eneo moja kwa jina - amygdala - hufanya tathmini ya kihisia.

Hii ni sehemu ya majibu ya mwili unapopigana na hisia fulani ili kutusaidia kuitikia kwa haraka sauti.

"Kwa hivyo wakati mapigo ya moyo wako yanapoongezeka, mfumo wako wa fahamu huanza kutoa homoni za mfadhaiko," Prof Clark ananiambia.

Jinsi kelele zinavyoathiri mwili wa mwanadamu

Yote haya ni mazuri katika dharura, lakini baada ya muda huanza kusababisha uharibifu.

"Iwapo utaathiriwa kwa miaka kadhaa, mwili wako unafanya hivyo kila wakati, huongeza hatari yako ya kupata magonjwa kama vile mshtuko wa moyo, shinikizo la damu, kiharusi na kisukari cha aina ya 2," Prof Clark alisema.

Hali hii hutokea hata tukiwa tumelala usingizi mzito. Unaweza kufikiria unazoea kelele. Nilifikiri nilifanya hivyo nilipoishi katika nyumba ya kukodisha karibu na uwanja wa ndege. Lakini biolojia inasimulia hadithi tofauti.

"Huwezi kufunga masikio yako; unapolala, bado unasikiliza. Kwa hivyo majibu hayo, kama vile mapigo ya moyo wako kupanda, hutokea ukiwa umelala," anaongeza Prof Clark.

.
Maelezo ya picha, Afya ya Coco inaathiriwa na kelele anakoishi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kelele ni sauti isiyohitajika. Usafiri - trafiki, treni na ndege - ni chanzo kikuu, lakini pia kuna sauti zinazofanywa na binadamu wakati wa sherehe. Kelele ya sauti za sherehe kwa mtu mmoja ni kelele isiyoweza kuvumilika kwa mtu mwingine.

Ninakutana na Coco katika ghorofa yake ya nne ya jumba analoishi katika eneo la kihistoria la Vila de Gracia huko Barcelona, Uhispania.

Kuna mfuko wa ndimu zilizovunwa hivi karibuni umefungwa kwenye mlango wake zikiwa ni zawadi ya jirani mmoja, friji yake ina tortilla iliyopikwa na mwingine na ananipa keki za kupendeza zilizotengenezwa na jirani wa tatu anayefundisha upishi wa keki.

Kutoka kwenye roshani unaweza kuona kanisa kuu maarufu la jiji, Sagrada Familia. Ni rahisi kuona kwa nini Coco alipenda kuishi hapa, lakini hatua yake inakuja na gharama kubwa na anafikiri kuwa atalazimika kuondoka.

"Kuna kelele sana ... ni kelele ya saa 24," ananiambia. Kuna bustani ya mbwa kwa ajili ya wamiliki "hubweka saa 2, 3, 4, 5 asubuhi" na huwa sehemu ya umma ambayo hutumiwa kwa kila kitu kutoka kwa sherehe za kuzaliwa kwa watoto hadi tamasha za siku nzima zinazokamilika na fataki.

Anatoa simu yake na kucheza rekodi za muziki unaopigwa kwa sauti kubwa sana hivyo kufanya kioo kwenye madirisha yake kutetemeka.

Nyumba yake inapaswa kuwa kimbilio kutoka kwa mafadhaiko ya kazi, lakini kelele "huleta kufadhaika, nahisi kulia".

"Amelazwa hospitalini mara mbili kwa maumivu ya kifua" na "kabisa" anadhani kelele husababisha mkazo, ambao unaharibu afya yake. "Kuna mabadiliko ya kimwili ambayo ninahisi, hufanya kitu kwa mwili wako, kwa hakika," anasema.

Huko Barcelona kunakadiriwa kuwa na mishtuko 300 ya moyo na vifo 30 kwa mwaka kutokana na kelele za trafiki, kulingana na mtafiti Dkt. Maria Foraster, ambaye amepitia ushahidi kuhusu kelele kwa Shirika la Afya Ulimwenguni.

.
Maelezo ya picha, Dk Maria Foraster anasema kelele za trafiki zina athari kubwa kwa afya kwani ni za kawaida

Kelele kote Ulaya zinahusishwa na vifo vya mapema 12,000 kwa mwaka pamoja na mamilioni ya visa vya kukosa usingizi pamoja na kero kubwa ya kelele ambayo inaweza kuathiri afya ya akili.

Ninakutana na Dk Foraster kwenye mkahawa ambao umetenganishwa na mojawapo ya barabara zenye shughuli nyingi zaidi za Barcelona na bustani ndogo. Kipimo changu cha sauti kinasema kelele kutoka kwa trafiki ya mbali ni zaidi ya desibeli 60 hapa.

Tunaweza kuzungumza kwa urahisi juu ya kelele bila kupaza sauti zetu, lakini hii tayari ni sauti isiyofaa.

Nambari muhimu kwa afya ya moyo ni desibeli 53, ananiambia, na kadiri unavyozidi kwenda ndivyo hatari za kiafya zinavyoongezeka.

"Hii 53 ina maana kwamba tunahitaji kuwa katika mazingira tulivu," anasema Dk Foraster.

Kelele za kawaida ni kubwa kiasi gani

Na hiyo ni wakati wa mchana tu, tunahitaji viwango vya chini zaidi vya kulala. "Usiku tunahitaji utulivu," anasema.

Ingawa sio tu kuhusu sauti, jinsi sauti inavyosumbua na jinsi unavyoweza kuidhibiti huathiri hisia zetu kwa kelele.

Dkt Foraster anasema athari za kiafya za kelele ziko "katika kiwango cha uchafuzi wa hewa" lakini ni ngumu zaidi kuelewa.

"Tumezoea kuelewa kuwa kemikali zinaweza kuathiri afya na ni sumu, lakini sio rahisi kuelewa kwamba kelele, huathiri afya zetu zaidi ya kusikia," anasema.

Sherehe kubwa inaweza kuwa furaha inayofanya maisha kuwa ya thamani na vilevile kuwa kelele isiyovumilika kwa mtu mwingine.

Sauti ya trafiki ina athari kubwa zaidi kwa afya kwa sababu watu wengi wanakabiliana nayo. Lakini trafiki pia ni sauti ya kufika kazini, kufanya ununuzi na kuwapeleka watoto shuleni. Kukabiliana na kelele kunamaanisha kuwaomba watu waishi maisha yao kwa njia tofauti - Suala ambalo huzua matatizo ya aina yake.

Dkt Natalie Mueller, kutoka Taasisi ya Barcelona ya Afya Ulimwenguni, ananipeleka kwa matembezi katikati ya jiji. Tunaanzia kwenye barabara yenye shughuli nyingi - mita yangu ya sauti inasoma kuwa kuna kelele zaidi ya desibeli 80 - na tunaelekea kwenye barabara tulivu iliyo na miti ambapo kelele iko chini hadi desibeli 50.

.
Maelezo ya picha, Natalie Mueller kwenye barabara tulivu yenye msongamano wa magari

Lakini kuna kitu tofauti kuhusu barabara hii - zamani ilikuwa barabara yenye shughuli nyingi, lakini nafasi ilitolewa kwa watembea kwa miguu, mikahawa na bustani. Ninaweza kuona barabara kuu ya zamani. Magari bado yanaweza kushuka hapa, polepole tu.

Kumbuka hapo awali kwenye maabara, tuligundua kuwa sauti zingine zinaweza kutuliza mwili.

"Sio kimya kabisa, lakini ni mtazamo tofauti wa sauti na kelele," Dkt Mueller anasema.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Watu hutembea katika eneo la watembea kwa miguu kama sehemu ya mpango wa Super block huko Barcelona.

Ukuaji wa miji

Hatari za kelele ingawa zinaendelea kukua. Ukuaji wa miji unawaweka watu wengi katika miji yenye kelele.

Dhaka, Bangladesh, ni mojawapo ya miji mikuu inayokua kwa kasi zaidi duniani. Hili limeleta msongamano zaidi wa magari na kulipa jiji hilo sauti za ajabu za honi. za magari

Msanii Momina Raman Royal alipata jina la "shujaa wa pekee" kwani maandamano yake ya kimya yalilenga shida za kelele za jiji.

Kwa takriban dakika 10 kila siku, anasimama kwenye makutano ya barabara kadhaa zenye shughuli nyingi akiwa na bango kubwa la manjano akiwashutumu madereva wanaopiga honi kwa sauti kubwa kwa kusababisha kero kubwa.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla