Kwanini wapigaji kura wanavipa kisogo vyama tawala barani Afrika?

gg

Chanzo cha picha, AFP

    • Author, Nic Cheeseman
    • Nafasi, Mchambuzi Afrika
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Chama tawala cha Namibia, Swapo, kimeendelea kuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 30, hata hivyo ushawishi wake umepungua mno-ikiwa ni nchi ya hivi punde zaidi ya Afrika ambapo viongozi walio madarakani wamekuwa na wakati mgumu mwaka huu.

Kulingana na matokeo rasmi, Netumbo Nandi-Ndaitwah, mgombea wa chama cha Swapo, alishinda uchaguzi wa urais kwa asilimia 57 ya kura, na kuwa kiongozi wa kwanza mwanamke nchini.

Vyama vya upinzani vimepinga matokeo ya uchaguzi vikidai uchaguzi huo ulikumbwa na dosari.

Maswala ibuka ambayo hayajapata ufumbuzi ni pamoja na jinsi chama cha Swapo ilivyoweza kuongeza hesabu ya kura za urais na umaarufu wake wakati katika uchaguzi wa wabunge ilirekodi matokeo duni kuwahi kutokea, ikipoteza viti 12 kati ya 63 na kushikilia tu kuwa na wabunge walio wengi bungeni.

Sio chama cha Swapo pekee kilichokumbwa na upinzani mkubwa katika uchaguzi.

Mwaka huu umekuwa wa "majanga" kwa serikali hizo za Afrika zilizo katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Katika kila uchaguzi uliofanyika katika eneo hili mwaka huu chini ya hali ya kidemokrasia, chama tawala kilipoteza idadi kubwa ya viti au kuondolewa mamlaka kabisa.

Taifa la Namibia limetawalia na chama cha Swapo tangu lipate uhuru 1990

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Taifa la Namibia limetawalia na chama cha Swapo tangu lipate uhuru 1990

Moja ya mambo ya kushangaza zaidi ya chaguzi zilizofanyika mwaka huu ni kwamba nyingi zimesababisha kushindwa kwa serikali ambazo hapo awali zilionekana kuwa na nguvu kubwa ya madaraka - ikiwa ni pamoja na katika nchi ambazo hazijawahi kupata mabadiliko ya juu.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Chama cha Botswana Democratic Party (BDP) ambacho kilikuwa kimetawala nchi hiyo tangu uhuru mwaka 1966 kilisambaratsihwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Pamoja na kupoteza mamlaka, chama cha BDP kilishindwa kufikia idadi ya wabunge 38 kama ilivyokuwa awali katika bunge lenye wabunge 69, na kikakaribia kufutwa kabisa.

Baada ya kushinda viti vinne pekee, BDP sasa ni moja ya vyama vidogo zaidi bungeni na kinakutana na changamoto kubwa ya kubaki na uhusiano wa kisiasa.

Pia, chama tawala cha Mauritius kilipata kipigo kikubwa mwezi Novemba, ambapo muungano wa Alliance Lepep, unaoongozwa na Pravind Jugnauth wa Vuguvugu la Wanamgambo wa Kisoshalisti, kilipata asilimia 27 pekee ya kura na kupunguzwa hadi viti viwili bungeni.

Chama cha upinzani cha Alliance du Changement, kilichoshinda viti 60 kati ya 66 vilivyopo, kilileta mageuzi makubwa ya kisiasa nchini Mauritius.

Senegal na Somaliland pia ziliona ushindi wa upinzani.

Kwa upande wa Senegal, mabadiliko ya kisiasa yalikuwa ya kushangaza kama ilivyokuwa nchini Botswana, ingawa kwa njia tofauti.

Wiki chache kabla ya uchaguzi, viongozi wa upinzani Bassirou Diomaye Faye na Ousmane Sonko walikuwa wakiteswa gerezani, huku serikali ya rais Macky Sall ikitumia vibaya mamlaka yake ili kuepuka kushindwa.

Shinikizo la ndani na kimataifa lililosababisha Faye na Sonko kuachiliwa huru, lilimsaidia Faye kushinda urais katika duru ya kwanza, huku mgombea wa serikali akishinda asilimia 36% pekee ya kura.

Mbwembwe zilianikiza Senegal baada ya upinzani kushinda uchaguzi

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Mbwembwe zilianikiza Senegal baada ya upinzani kushinda uchaguzi

Hata katika hali ambapo serikali tawala hazijashindwa katika uchaguzi,sifa na udhibiti wao wa kisiasa umesuasua sana.

Kama ilivyokuwa kwa chama cha SWAPO hivi punde, chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini kiliendelea kuwa madarakani, lakini kutokana na kampeni mbaya, kilishuka chini ya asilimia 50 ya kura katika uchaguzi wa kitaifa kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa utawala wa wazungu wachache mwaka 1994.

Hali hii ilimlazimu Rais Cyril Ramaphosa kuunda serikali ya mseto na kugawa nyadhifa 12 za baraza la mawaziri kwa vyama vingine, ikiwa ni pamoja na nyadhifa muhimu kama ile ya Mambo ya Ndani.

Kwa matokeo hayo, eneo ambalo limekuwa maarufu kwa serikali zinazoshikilia madaraka kwa miongo kadhaa sasa linaona mwaka mmoja wa siasa za vyama vingi na ushindani mkali.

Hata hivyo, hali hii iliepukwa na nchi ambazo uchaguzi haukuwa huru wala wa haki, kama vile Chad na Rwanda, au zile ambapo serikali zilishutumiwa na upinzani na makundi ya haki za binadamu kwa kutumia mbinu za udanganyifu na ukandamizaji ili kuepuka kushindwa, kama ilivyokuwa nchini Msumbiji.

Mitindo mitatu hii imechangia katika kufanya mwaka huu kuwa mgumu kwa serikali zinazoshikilia madaraka.

Nchini Botswana, Mauritius na Senegal, ongezeko la wasiwasi wa raia kuhusu rushwa na matumizi mabaya ya madaraka lilisababisha kupungua kwa imani kwa serikali.

Viongozi wa upinzani walitumia hasira za wananchi dhidi ya upendeleo, usimamizi mbovu wa kiuchumi, na kushindwa kwa viongozi kuheshimu utawala wa sheria ili kupanua uungwaji mkono wao.

Hasa katika Mauritius na Senegal, chama kilicho madarakani kilipuuzilia mbali madai yake ya kuwa serikali iliyojitolea kuheshimu haki za kisiasa na uhuru wa kiraia – hatua hatari katika nchi ambazo raia wengi wamejitolea kwa demokrasia na ambazo hapo awali zilishuhudia ushindi wa upinzani.

Mtazamo kwamba serikali zilikuwa zikishughulikia vibaya uchumi ulikuwa na uzito mkubwa kwa sababu watu wengi walikabiliwa na mwaka mgumu kifedha.

Mfumko wa Bei ya vyakula na mafuta iliongeza gharama ya maisha kwa mamilioni ya wananchi, hali iliyochochea kuchanganyikiwa kwao.

Mbali na kushindwa kwa serikali katika maeneo mengine, hasira ya kiuchumi ilikuwa ni chanzo kikuu kilichosababisha maandamano ya vijana nchini Kenya yaliyotikisa serikali ya Rais William Ruto mnamo Julai na Agosti.

Uchungu wa kuongezwa kwa ushuru sambamba na ongezeko la gharama ya maisha ulichochea maandamano nchini Kenya

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Uchungu wa kuongezwa kwa ushuru sambamba na ongezeko la gharama ya maisha ulichochea maandamano nchini Kenya

Hili si suala la kipekee kwa Afrika pekee, bali ni changamoto ya kimataifa.

Kutoridhika na mfumuko wa bei kumekuwa na athari kubwa katika mabadiliko ya kisiasa duniani, kama ilivyoshuhudiwa katika kushindwa kwa Rishi Sunak na Chama cha Conservative nchini Uingereza, na ushindi wa Donald Trump na Chama cha Republican nchini Marekani.

Hata hivyo, kile kinachokuwa tofauti zaidi kuhusu mabadiliko ya madaraka barani Afrika mwaka huu ni jinsi vyama vya upinzani vilivyojifunza kutoka kwa makosa ya zamani.

Katika baadhi ya matukio, kama vile Mauritius, vyama vya upinzani vilibuni mbinu mpya za kulinda kura na kuhakikisha kila hatua ya mchakato wa uchaguzi inafuatiliwa kwa makini.

Katika matukio mengine, vyama vya upinzani vilijenga miungano mipya ili kuwasilisha ujumbe wa umoja kwa wapiga kura.

Nchini Botswana, kwa mfano, vyama vitatu vya upinzani pamoja na wagombea binafsi walikusanyika chini ya muungano wa Mwamvuli wa Mabadiliko ya Kidemokrasia kwa lengo la kung’oa chama cha BDP madarakani.

Mitindo hii inaweza kuleta changamoto kwa New Patriotic Party (NPP) ya Ghana katika uchaguzi wa Jumamosi, na pia inaweza kuleta matatizo makubwa kwa serikali ya Malawi chini ya Rais Lazarus Chakwera katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Ikiwa Ghana itashuhudia uhamishaji wa madaraka, hii itakuwa ni ushindi wa tano wa vyama vya upinzani katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ifikapo mwaka 2024 – jambo litakalokuwa ni rekodi ya kihistoria kwa mkoa huu.

Hata hivyo, ni jambo la kushangaza kuona kwamba licha ya kuporomoka kwa demokrasia duniani na kuongezeka kwa utawala wa kimabavu katika baadhi ya maeneo, serikali nyingi barani Afrika zinakutana na changamoto kubwa kutoka kwa wapiga kura katika uchaguzi.

Hii inaashiria kuwa Afrika ina viwango vya juu zaidi vya uthabiti wa kidemokrasia kuliko inavyotambulika mara nyingi, licha ya kuwepo kwa tawala za kimabavu zinazojitokeza.

Mashirika ya kiraia, vyama vya upinzani na wananchi wenyewe wamejizatiti kwa wingi kudai uwajibikaji kutoka kwa serikali, na kuwaadhibu wale ambao wamekuwa na utawala mbovu wa kiuchumi na kidemokrasia.

Serikali za kimataifa, mashirika, na wanaharakati wanaotafuta njia mpya za kulinda demokrasia duniani wanapaswa kuzingatia zaidi maeneo ya Afrika, ambayo mara nyingi huchukuliwa kuwa na changamoto kubwa katika siasa za vyama vingi, lakini pia yamekuwa na mifano mingi ya kurejea kwa demokrasia kuliko mikoa mingine duniani.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid