Wabunge Kenya wapitisha Mswada wa Fedha

Chanzo cha picha, Bunge la Kenya
Wabunge nchini Kenya wamepitisha mswada wa Fedha uliozua mgawanyiko nchini humo kwa mapendekezo kadhaa ya kuongeza kodi.Wabunge 176 waliidhinisha mswada huo ilhali 81 waliupinga.
Jumla ya wabunge waliopiga kura ni 257.
Rais William Ruto na kinara wa Azimio Raila Odinga walikuwa wamewatahadharisha wanachama wa Miungano yao kwamba watakuwa chini ya ulinzi ili kuona ni njia gani wangeupigia kura Mswada huo.
Siku ya Jumanne, Kamati ya Bunge ya Kitaifa ya Fedha na Mipango iliwasilisha Mswada wa Fedha wa 2023 uliorekebishwa baada ya umma kutoa maoni yao kuhusu Mswada wenyewe.
Kulikuwa na lalama kuhusu mapendekezo fulani katika Mswada huo, ambayo Wakenya waliyataja kuwa kandamizi.
Baadhi ya tozo zilizopendekezwa zilirekebishwa huku nyingine zikisalia zile zile.
Mswada huo, unapendekeza miongoni mwa mambo mengine ushuru wa nyumba kwa mishahara ya wafanyakazi na ongezeko la ushuru wa mafuta.
Rais Ruto alisema mswada huo ni muhimu kuongeza mapato ili kufadhili bajeti ya kwanza ya utawala wake ya Sh3.59 trilioni.
Kamati ya bunge kuhusu Fedha iliazimia kubakiza ushuru wa asilimia 16 wa VAT kwa bidhaa za petroli, ambayo itaongeza ushuru wa petroli kwa kiwango sawa na mafuta taa na dizeli.
Kodi iliyopendekezwa ya Ongezeko la Thamani (VAT) ilikuwa asilimia 16 na haijarekebishwa hadi kiwango cha chini.
Miongoni mwa marekebisho muhimu ya mswada huo, ni asilimia 15 iliyopendekezwa kwa Waundaji wa Maudhui ya Dijitali ambayo imepitiwa upya hadi asilimia 5.
Pia, asilimia tatu ya tozo ya nyumba inayopendekezwa imepunguzwa hadi asilimia 1.5 katika marekebisho mapya.












