Kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara Tanzania na Kenya kunamaanisha nini?
Na Yusuph Mazimu, BBC Swahili

Chanzo cha picha, IKULU
Wiki hii Tanzania na Kenya zimekubaliana kuondoa vikwazo vyote 14 vilivyosalia vya kibiashara baina ya nchi hizo mbili. Hii ni hatua kubwa kuelekea kuwa na uhuru wa kibiashara na uhuru wa wafanyabiashara wanaoendesha shughuli zao katika mataifa haya ya Afrika Mashariki.
Kwa miaka mingi kumekuwa na makelele ya kuwepo kwa vikwazo vingi vinavyoyumbisha biashara kupunguza kasi ya ukuaji wa kibiashara baina ya nchi hizi.
Kufuatia maagizo ya rais aliyepita wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Rais Samia Suluhu pamoja na vikao vya mawaziri na wawakilishi wa pande zote mbili, yalisaidia kushugulikiwa kwa vikwazo 56 pekee na kuchangia ukuaji wa biashara baina ya mataifa haya kwa asilimia 38% kufikia dola milioni 765 kwa mwaka 2021 pekee.
Pengine faida hii na nyingine zitakazobainishwa kwenye Makala hii, zinawasukuma Rais wa sasa wa Kenya na Rais Samia kutoa maagizo kwa mawaziri husika wa nchi hizi kukutana na kujadili namna ya kumalizia kuviondoa vikwazo 14 vilivyosalia.
Vikwazo 14 vinavyotajwa ni vipi?

Katika kikao cha mwezi Machi, 2022 huko Zanzibar, Ujumbe wa Kenya ukiongozwa na waziri wake wa zamani wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Betty Maina na Asha Kijaji, waziri wa Uwekezaji, viwanda na biashara akiongoza ujumbe kutoka Tanzania, walijadili vikwazo 30 na kufanikiwa kuvishughulikia baadhi.
Vikwazo vilivyosalia kwenye mjadala vilikuwa kwenye umoja wa forodha, ushuru wa bidhaa za bia za TBL kuingia Kenya, ushuru wa stempu na kushikiliwa kwa makontena 50 ya saruji na mamlaka za KPA/TRA.
Vikwazo vingine ni kutokulipwa kwa wafanyabishara wa Tanzania waliokuwa wanasambaza bidhaa zao katika maduka makubwa ya Nakumatt na Uchumi. Deni la Tzs 8.6 bil kwa biashara 283 zilizosambazwa katika maduka ya Uchumi aliyofungwa mwaka 2015, na TZS 5.6bil kwa biashara 122 kwenye maduka ya Nakumatt yaliyofungwa mwaka 2016.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Vingine ni vikwazo kwenye tumbaku ya Kenya, tozo zinazolalamikiwa kwa bidhaa zitokanazo na wanyama Kenya zinazoingia Tanzania, changamoto ya usafirishaji wa mbegu kuingia Tanzania kutokana na kanuni mbalimbali, zikiwemo za GMO.
Uwepo wa ulazima wa vibali vinavyoruhusu uingizaji wa vyanzo vya mionzi na bidhaa za vyakula nchini Tanzania na ushuru wake wa 0.4%, ushuru wa barabarani, uwepo wa sheria ya wageni the Non-citizens (Employment Regulation) Act 2015 inayoathiri masuala ya kazi na biashara.
Vingine ni Bima ya COMESA ya kiwango cha Ksh 30,000 ambapo inapotokea madhara ya mtu wa tatu kuwa na gharama ya juu zaidi itampasa msafirishaji agharamie kiasi cha ziada.
Changamoto zinazowakumba jamii zinazoishi mpakani huku kuzuiwa kwa nyama ya Uturuki kutokea Kenya kwa sababu ya hofu ya maambukizi ya Influenza na ulazima wa Cheti cha chanjo ya Covid-19 ya Kenya kwa wasafiri wa anga kutoka Tanzania ni vikwazo vipya vilivyojitokeza kwenye mkutano uliopita wa mawaziri.

Kwanini nchi zinaweka vikwazo wakati ikiviondoa inafadika?

Si rahisi kukuta taifa likajitosheleza kwa kila kitu, kupitia viwanda vyake na shughuli zake zingine za uzalishaji. Kuna wakati itahitaji aina fulani ya bidhaa, huduma, utaalamu na watalaamu kutoka nje ya nchi.
David Osiany, naibu waziri wa viwanda na biashara wa wakati huo wa Kenya aliwahi kusema kuhusu mafanikio ya uondoaji wa vikwazo vya biashara, kwamba biashara imekuwa mara 6 baina ya nchi hizo kwa muda wa miezi minne ya mwaka jana.
‘hatuwezi kuongea kuhusu soko huru la Afrika, kama hatuwezi kufanya biashara kama Afrika Mashariki, lazima tuaminiane tuhakikishe tumesingesha biashara yetu’, alisema Osiany.
Unaweza kujiuliza kama mahitaji yapo na faida ipo, kwa nini nchi iamue kuweka vikwazo kwenye bidhaa ama biashara ambayo inajua kuna faida itapata kupitia kodi, ushuru, tozo na hata kurahisisha upatikanaji wake kwa wananchi wake?
Wataalam wa uchumi na biashara wanazitaja sababu zifuatazo; kulinda ajira za ndani, kupunguza na kuzuia ajira holela wa ajira, kuongeza mapato ya nchi kupitia kodi na ushuru wa bidhaa kutoka nje, kuongeza matumizi ya bidhaa zinazozalishwa ndani, kumlinda mlaji wa ndani, na kulinda usalama wa watu wake kwa ujumla.
‘Usalama ni jambo kubwa sana, kuliko yote, sishangai kuona ili upitishe bidhaa za mionzi lazima uwe na kibali kutoka kwa mamlaka za nishati za Atomiki, kwa sababu ni rahisi kupitishwa hata silaha za nyukilia usipoweka utaratibu’, anasema Beatrice Kimaro, mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika.
‘Cheti cha Covid ili mtanzania aingie Kenya, ni katika kulinda usalama wa afya za wakenya, kwa hivyo kila kitu kimewekwa kwa maslahi ya taifa husika’, aliongeza.
Athari za utekelezaji wake Kisheria?

Safari ya kuondoa vikwazo si kama kuondoa chakula mezani ama kusuuza sahani ya ukoko wa wali. Iwe vikwazo vya kiushuru ama visivyo vya kiushuru (Non-tarrif barriers) mchakato wake unahitaji majadiliano, maridhiano na kwenye utekelezaji kuna baadhi unagusa sera, kanuni, miongozi na sheria zilizoweka na nchi.
Kwa mfano tozo, ushuru ama kodi zinawekwa kwa misingi ya kisheria na kikanuni, hivyo kuondolewa kwakwe kunahitaji kufuatwa kwa misingi hiyo hiyo. Hivyo utekelezaji wake lazima uchukue muda kiasi.
‘vikwazo vya ucheleweshaji wa ukaguzi wa mizigo ama utoaji wa vibali vya kawaida, unaweza kutekeleza, lakini kodi kwenye bidhaa fulani inayoingia, ama usalama wa bidhaa yenyewe, ni lazima, mamlaka za juu, wakati mwingine sheria zihusike, sio jambo la kukimbia’, alisema Beatrice.
Anachokisema Beatrice kinajionesha kwenye uwekezaji wa USD 130mil wa Taifa Gas nchini Kenya, uliwezekana kuondolewa kikwazo, kwa sababu haukuhitaji sheria. Walikaa pamoja Taifa Gas na Mamlaka inayosimamia ukanda wa uwekezaji (SEZA) wakakubaliana.
Kwa mfano suala la Tanzania kupunguza kibali cha biashara kutoka dola 500$ mpaka dola 100$ kwa wafanyabiashara wa Afrika mashariki, liko chini ya sheria inayoitwa Non- Citizens (Employment Regulations) Act ya mwaka 2015. Kenya ilifuata misingi ya soko la pamoja la Afrika Mashariki wakati Tanzania iliendelea kuwatoza dola 100$ kwa wafanyabiashara wa Kenya.
Uamuzi wa kuviondoa vikwazo unamaanisha nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
‘uhuru upo wa biashara na suluhu ya kuondoa vikwazo vya biashara’, hii ilikuwa kauli ya Rais Samia Suluhu wa Tanzania mwaka jana akiwahimiza wakenya kwenda kuwekeza Tanzania.
Uhuru anaousema Rais Samia, utakamilika kwa kuondolewa vikwazo vyote vilivyosalia. Na hilo ndilo msingi wa kushughulikia vikwazo 14 vilivyosalia.
Wachumi na wataalam wa biashara wanasema, uamuzi wa sasa ni kuimarisha zaidi biashara baina ya nchi hizo, lakini pia kuweka uhuru kamili wa shughuli za kibiashara kwa faida ya pande zote mbili.
Lakini wanaonya “ uhuru huu ni muhimu sana, lakini uwe na tahadhari, lazima kuandaliwe mazingira ya pamoja, kwenye kushughulikia vikwazo vinavyogusa usalama wa watu, mali na afya zao, anasema Raphael Kugesha, mchumi wa maendeleo ya jamii, aliyejikita kwenye eneo la utalii Tanzania kwa miaka zaidi ya 10 sasa.
Pengine hatua ya sasa, ni muendelezo wa ndoto za kufikia uhuru wa kibiashara kwa nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Inawezekana, lakini mjadala je nchi hizi zimejiandaa kwa matokeo ya upande wa pili wa athari za uhuru huo?














