Kushuka kwa thamani ya fedha ya Kenya kuna athari gani?

    • Author, Beatrice Kimaro
    • Nafasi, Mchambuzi wa uchumi
  • Iliyochapishwa

Mwaka huu, 2023 umekuwa mwaka mchungu kwa shilingi ya Kenya.Bei ya kununua dola katika kumbi za benki na duka za ubadilishanaji fedha za kigeni imefikia Sh145 kwa dola ya Kimarekani, na kuchangia kupanuka kwa pengo kati ya viwango rasmi na vya soko huria, na kuunda soko lisilofaa kwa sarafu ya Marekani kutokana na uhaba wake.

Kulingana na Gazeti la Business Daily ukaguzi wa moja kwa moja uliofanywa Jumatano iliopita katika baadhi ya mabenki ulionyesha kuwa zilikuwa zikiwauza wateja dola kwa kati ya Sh140.55 na Sh144.50 huku wakinunua sarafu hiyo yakwa kati ya Sh128.20 na Sh131.40 kwa kila moja.

Wateja wananunua dola kwa kati ya Sh141 na Sh146 kwa kila dola moja katika duka za ubadilishanaji fedha za kigeni, ambazo zinapata sarafu ya Marekani kwa kati ya Sh135 na Sh138.

Ingawa jitihada za kiuchumi za kuinusuru shilingi ya Kenya zinaendelea kufanywa na serikali ya Rais William Ruto, bado wasiwasi zaidi unaongezeka kutokana na kuendelea kwa athari za mabadiliko ya tabia nchi zinazoambatana na ukame pamoja na uhaba wa mvua katika baadhi ya maeneo, lakini pia hali ya kisiasa na maandamano yanayotishiwa kufanywa na upande wa upinzani.

Lakini ni nini na kwa nini pesa ya taifa hilo la Kenya inazidi kshuka thamani?

Kwanini pesa ya Kenya inazidi kuporomoka?

Kawaida thamani ya pesa inapatikana kwa njia zile zile za kawaida kama ilivyo kwa bidhaa zingine kwenye soko la uchumi zinavyothaminishwa. Ni kupitia Mahitaji na usambazaji au kwa lugha ya kiuchumi ‘Demand and Supply’.

Kuongezeka ama kupungua kwa mahitaji na usambazaji kunachochewa kiuchumi na sababu kadhaa ikiwemo mzunguko wa fedha (money supply), mfumuko wa bei (Inflation), viwango vya riba (interest rates) na suala la mitaji (capital flow).

Na mara nyingi sababu hizi zinazoathiri mahitaji na usambazaji kiuchumi zinaratibiwa na sera ya fedha ya nchi husika.

Sasa kwa Kenya kufuatia hatua ya Serikali kuendelea kulipa madeni hasa ya nje, mapato madogo kutokana na kuuza nje (low export earnings), ulipaji wa magawio kwa makampuni yenye wamiliki wa kigeni ambapo husababisha mabilioni ya dolla kupelekwa nje kwa wanahisa wa makampuni haya.

Benki kuu ya Kenya inasisitiza kuyumba kwa akiba ya fedha za kigeni kama sababu muhimu, ikishuka mpaka dola $6.56 billion karibu Sh849 billion za Kenya kutoka $6.61 (Sh854.7 billion) kaika mabadiliko ya ndani ya wiki mbili zilizopita za mwanzoni mwa mwezi Machi, kiwango kinachoweza kutumika katika miezi isiyozidi 3.67.

Athari za kuporomoka kwa Shilingi ya Kenya

Athari za wazi kwa upande wa Kenya kwa sasa zinazoletwa na kuporomoka kwa shilingi ya nchi hiyo ni pamoja na mfumuko wa bei na kupanda kwa gharama za maisha.

Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi Dkt. Barnos William anaongeza ‘Kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola kunaongeza zaidi mahitaji ya dola, ni rahisi kuwa na soko haramu la fedha za kigeni (black market), na hii ni mbaya kwa ukuaji wa biashara na uchumi wa nchi’.

Kwa Kenya mahitaji ya dola ni makubwa hasa kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa kama machine, bidhaa na malighafi za viwandani pamoja na mafuta. Lakini kupungua kwake kwenye mzunguko kutokana na kupanda zaidi kwa thamani yake ukilinganisha na uwiano wa thamani ya shilingi ya Kenya, kunatikisa uagizaji wa bidhaa kutoka nje kama ikiwemo mafuta ya kupikia na ngano zinazoingizwaga kwa wingi nchini humo.

‘Unapoagiza kwa mfano malighafi na bidhaa zingine kutoka nje, kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi, inaongeza gharama za uagizaji, gharama hizi zikiongezeka tegemea bei ya bidhaa hiyo kwa mlaji wa mwisho itakuwa juu zaidi ili mfanyabiashara atengeneze faida ama kurudisha gharama zake’, anasema Dkt. William.

Kwa kauli za mchumi huyu haishangazi kusikia maandamano yakiaandaliwa kila uchawao na upande wa upinzani Kenya, wanaodai kuwepo kwa hali ngumu ya maisha kutokana na vitu kupanda bei zaidi.

‘Sababu ya vitu kupanda bei kupita kiasi na hali ngumu ya maisha, hiyo huwa sababu ya kwanza kuonekana, mara tu panapotokea pesa ya taifa husika kushuka thamani kwa kiwango kikubwa’, anasema Dkt. William.

Hali ikoje kwa shilingi za Tanzania na Uganda na namna gani zinaathiri biashara na Kenya?

Kwa sasa shilingi ya Tanzania imeendelea kuwa tulivu wastani wake wa 2309.36 dhidi ya dola katika kipindi kirefu cha mwaka huu. Katika maduka mengi ya kubadilishia fedha na mabenki dola kwa sasa inauzwa kati ya shilingi 2296 mpaka 2299.

Angalau shilingi ya Tanzania ina hauweni kwa sasa ukilinganishwa na mwaka 2019 ambapo dola moja ya Marekani iliuzwa kwa kati ya shilingi 2,415 hadi na shilingi 2,418 ya Tanzania, bei ambayo inatajwa ilikuwa ya kiwango cha chini zaidi kuwahi kutokea.

Siku chache ziliizopita benki kuu ya Tanzania ilikiri kushuka kwa thamani ya shilingi ikitaja sababu kama kuchelewa kwa ununuzi wa korosho, kutokuwa na msimu wa watalii na kupungua kwa fedha za wahisani.

Mara kadhaa amesikika Waziri wa fedha wa Tanzania, Mwigulu Mchemba akisema kuwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani kuendelea kuwa tulivu kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuwepo kwa akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, utulivu wa mfumuko wa bei nchini, mwendelezo wa nakisi ndogo katika urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamishaji mali nchi za nje, pamoja na utekelezaji wa sera thabiti za fedha na bajeti.

Kwa upande wa shilingi ya Uganda kati ya April 2022 mpaka sasa imekuwa ikishuka dhidi ya dola kwa asilimia 3%, kwa mujibu wa benki kuu ya Uganda.

Hii ni mara ya kwanza shilingi ya nchi hiyo kuporomoka kwa kiasi hicho dhidi ya dola katika kipindi cha miongo mwili iliyopita.

‘Inachopitia Kenya, pia kinapitiwa na nchi nyingi hasa za Afrika ikiwemo Tanzania, Uganda, Afrika Kusini, Sudan, DRC na nyingine za Ukanda wa kusini mwa Jangwa la Sahara’ anasema Mtaalamu wa maendeleo ya uchumi wa jamii, Raphael Kugesha kutoka Tanzania na kuongeza ‘ lazima kibiashara kuna athari kiasi kwa sababu zipo biashara nyingi baina ya nchi hizi zinatumia dola’.

Kwa mfano huu wa mchumi huyu, Kenya na Tanzania, kwa mfano, takriban asilimia 60 ya ununuzi wa nje hulipwa kwa Dola za Marekani, ingawa ni upande wa mafuta zaidi asilimia 100 ya malipo kutoka nje ya nchi inalipwa kwa Dola.

Upo wasiwasi kwamba shilingi ya Kenya itaendelea kusuasua kutokana na mengi yanaoendelea. Terry Karanja, mmoja wa wataalamu wa fedha kutoka AZA Finance, aliwahi kunukuliwa akitaja ukosefu wa mvua kutasababisha kupatikana kwa mazao duni na kuzidi kuongeza mfumuko wa bei, vitu ambavyo vitaendelea kushusha thamani ya shilingi ya nchi hiyo.

Lakini wengine wanataja mizozo ya kisiasa, ‘haya maandamano na kukosekana kwa utulivu kisiasa, kunatishia wawekezaji, tutatarajia msukosuko zaidi wa fedha za kigeni na uwekezaji, kwa hili usitarajie kushuhudia shilingi ikiimarika’, anasema Kugesha.

Kuna haja ya Kenya kama ilivyo kwa mataifa mengine ya Afrika Mashariki kuimarisha akiba yake ya fedha za kigeni, kuongeza uwekezaji wake kwenye viwanda vya ndani ili kuuuza zaidi nje ya nje.

‘Kwa kufanya hivi, unajaribu kuwa na urari mzuri wa mahitaji na usambazaji (Demand and Supply) ambao ni muhimu sana kwenye uchumi wa soko na uimara wa kuimarisha thamani ya fedha’, alisema Dkt. William, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.

Fikra za kiuchumi zinataka mwendelezo mzuri wa nakisi ndogo katika urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamishaji mali nchi za nje, pamoja na utekelezaji wa sera thabiti za fedha na bajeti. Pamoja na hili kufahamika; swali la kujiuliza ni kwanini kila leo tunashuhudia kushukakwa thamani ya shilingi za mataifa haya?