Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Gaza-Israel zakabiliana vikali kufuatia shambulio baya katika ukingo wa magharibi
Jeshi la Israel limefanya mashambulizi ya anga katika Ukanda wa Gaza baada ya wanamgambo wa Kipalestina katika eneo hilo kurusha makombora kusini mwa Israel.
Roketi sita zilirushwa kutoka Gaza alfajiri, tano kati ya hizo zilinaswa, jeshi lilisema. Muda mfupi baadaye, ndege za kivita za Israel zilishambulia kile ilichokitaja kuwa maeneo mawili ya wanamgambo wa Hamas.
Hakuna aliyeripotiwa kuumia.
Makabiliano hayo yanafuatia uvamizi wa Israel huko Nablus katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu siku ya Jumatano na kuua Wapalestina 11.
Hamas, ambayo inadhibiti Gaza, na kundi jingine la wanamgambo, Palestinian Islamic Jihad, walikuwa wamtishia kulipiza kisasi.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika Mashariki ya Kati Tor Wennesland, ambaye anajaribu kuondoa hali hiyo, alisafiri hadi Gaza siku ya Alhamisi kukutana na viongozi wa Hamas, kulingana na shirika la habari la Reuters.
"Nimesikitishwa sana na msururu wa vurugu na kushangazwa na vifo vya raia," alisema kabla ya safari iliyoripotiwa. "Ninaziomba pande zote kujiepusha na hatua ambazo zinaweza kuzidisha hali ambayo tayari ni tete."
Mpaka sasa hakuna kundi lolote la wanamgambo lililodai kuhusika na shambulio hilo la roketi la Alhamisi, ambalo lilisababisha ving'ora katika miji ya kusimwa Israel karibu na Gaza, ikiwemo Ashkelon na Sderot kulia.
Kulikuwa na milipuko midogo angani kwani mingi ilinaswa na mfumo wa ulinzi wa Iron Dome wa Israeli, kulingana na jeshi la Israeli. Roketi moja ilianguka katika eneo wazi.
Jeshi lilisema saa mbili baadaye kwamba ndege zake za kivita zilishambulia eneo la utengenezaji wa silaha na kambi ya kijeshi ya Hamas katikati na kaskazini mwa Gaza kujibu.
Picha za video zilizochapishwa mtandaoni zimeripotiwa kuonyesha milipuko katika kambi za wakimbizi za al-Bureij na al-Shati.
Jumatano asubuhi, wanajeshi wa Israel waliingia katika mji mkongwe wenye shughuli nyingi wa Nablus, kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, kwa kile walichokisema kuwa ni operesheni ya kuwakamata wanamgambo watatu wa Kipalestina waliokuwa wanatafutwa. Lakini, walikamatwa haraka katika makabiliano ya risasi na wapiganaji wenye silaha.
Wanajeshi wa Israel hatimaye walirusha vilipuzi kwenye handaki ambayo wanamgambo hao watatu walikuwa wamejichimbia, baada ya kusema kwamba hawatajisalimisha. Jeshi la Israel lilisema watu hao walihusika katika mauaji ya mwanajeshi wa Israel mwaka jana na walikuwa wakipanga mashambulizi ya mengine.
Raia kadhaa pia walikuwa miongoni mwa waliouawa katika uvamizi huo, wakiwemo wazee watatu.
Video pia ilionyesha vijana, ambao inaonekana hawakuwa na silaha, wakikimbia huku milio ya risasi ikisikika kabla ya mmoja kuanguka chini. Jeshi la Israel limesema linakagua picha hizo.
Hospitali za eneo hilo zimekuwa zikihangaika kuwatibu makumi ya watu waliojeruhiwa, wengi wakiwa na majeraha ya risasi.
Daktari mmoja aliambia mwandishi wa BBC Tom Bateman kwamba hilo lilikuwa mojawapo ya matukio mabaya zaidi ya aina hii ambayo amewahi kuona katika miaka ya hivi majuzi.
Mvulana mwenye umri wa miaka 15 aliyekuwa na jeraha mguuni alisema alikuwa amesimama karibu na wanamgambo wakati alipopigwa na milio ya risasi ya Israel.