Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Msichana wa Wales aliyelazimishwa kupima ubikira kabla ya ndoa
Farah hakua anapinga kuolewa tu bali pia hakutaka kufanyiwa kipimo cha kubaini ubikira wake.
Alilazimishwa kufanyiwa kipimo cha ubikira "unaodhalilisha" kabla ya kulazimishwa kuolewa akiwa na umri wa miaka 18.
"Sikujua ni aina ya unyanyasaji" alisema Farah. "Niliona aibu kwa kile walichonifanyia na tukio hilo la kufedhehesha limesalia akilini mwangu."
Kupima ubikira ni kinyume cha sheria nchini Uingereza lakini mashirika ya misaada yanayosaidia wanawake walioathiriwa na unyanyasaji wa aina hiyo na bado yanapokea visa kama hivyo.
Farah - si jina lake halisi - alisema mama yake alimpeleka kwa "daktari katika jamii ili kubaini kama nilikuwa bikira".
"Nililazimishwa kufunga ndoa nilipokuwa na umri wa miaka 18, nikitarajiwa kuishi na familia ya mume wangu," alikumbuka.
"Hiki sio kile nilichotaka na walijua hilo. Nilipinga hili hadi dakika ya mwisho lakini haikuleta tofauti.
"Kama ningejua kuna msaada labda ningezungumza na mtu anayeelewa."
Farah alisema pia "alifedheheshwa" usiku wa harusi yake wakati shuka zake zenye damu zilipoonyeshwa mama mkwe wake "kuthibitisha kuwa mimi ni bikira".
Kipimo cha ubikira ni nini?
Kipimo cha ubikira ni utaratibu usio halali unaohusisha ukaguzi wa kizinda(sehemu ya ndani ya uke), unaokusudiwa kubaini iwapo mwanamke au msichana ni bikira.
Lakini Shirika la Afya Duniani (WHO) na Chuo cha Royal cha Madaktari wa Uzazi na Wanajinakolojia (RCOG) wamesema vipimo vya ubikira havina sifa za kisayansi au dalili za kimatibabu.
Wanasema hakuna uchunguzi unaojulikana ambao unaweza kuthibitisha kama mwanamke amefanya ngono kwa sababu kizinda kinaweza kuvunjika kwa sababu kama vile kutumia kisodo na mazoezi.
Uchunguzi wa BBC mnamo 2020 uligundua wanawake walikuwa wakifanyiwa "vipimo vya ubikira" katika kliniki za matibabu za Uingereza, huku wengine wakitangaza kile kinachoitwa "kurekebisha ubikira" - utaratibu unaoitwa hymenoplasty.
Je kupima ubikira ni kinyume cha sheria?
Imekuwa kinyume cha sheria kufanya, kutoa au kusaidia na kupima ubikira nchini Uingereza tangu 2022 na yeyote atakayepatikana na hatia anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka mitano jela na uwezekano wa kutozwa faini isiyo na kikomo.
Sheria ya Afya na Utunzaji ya 2022 pia ilifanya kuwa haramu kwa raia wa Uingereza na wakaazi kusaidia kupima ubikira nje ya Uingereza.
Shirka la Afya Duniani WHO, imesema upimaji wa ubikira unasadikiwa kufanywa katika angalau mataifa 20.
Utaratibu huo wa kufedhehesha anachukuliwa kuwa ukiukaji wa haki za binadamu na WHO na Umoja wa Mataifa - na mashirika yote mawili yanashinikiza upigwe marufuku kote duniani.
'Wanawake hawajui pa kwenda kutafuta msaada'
Farah sasa yuko salama baada ya kutoroka mazingira yake ya unyanyasaji na amehamia mbali na Wales.
Lakini utaratibu aliofanyiwa umemuacha na athari ya kudumu, na alitaka kushiriki kisa chake ili kuongeza ufahamu na kusaidia wasichana wengine ambao wanaweza kukabiliwa na unyanyasaji sawa na wake.
"Si jamii nyingi zitazungumza kuhusu hili lakini najua wasichana wachache wamepitia haya lakini hawajui pa kwenda kupata msaada," alisema.
Idadi ya wanawake walioathiriwa na utaratibu wa upimaji ubikira nchini Uingereza haijabainika, kwani masuala yanayohusiana na ngono yanaweza kuwa mwiko katika jamii hizi.
Watu wengine pia hawatambui kama unyanyasaji au kujua kuwa ni kinyume cha sheria - kwa hivyo wengi hawajitokezi kuripoti.
'Utamaduni ni ngumu kumaliza'
Shirika moja linalowasaidia wanawake kutoka wa wenye asili ya kiafrika limewaokoa wanawake saba ambao wamepitia upimaji wa ubikira kati ya Aprili na Desemba 2022 na wengine watatu ambao walikuwa na hymenoplasty.
Bawso alisema wanawake hao ni pamoja na watu kutoka Misri, Afrika Kusini, Pakistan, India na Saudi Arabia.
"Ni suala lililoenea kwani Wales ina watu wengi ambao wamehama kutoka nchi hizo ambazo zinafanya utaratibu wa kupima ubikira," alisema mtendaji mkuu wake wa muda Wanjiku Ngotho-Mbugua.
"Tunajua watu wanadumisha tamaduni zao na utamaduni ni vigumu sana kukomesha. Wasichana ambao wamefanyiwa utaratibu huo wanaona haya kuzungumzia.
"Haina madhara ya kisaikolojia tu, lakini athari ya kimwili kwa wasichana hawa kwa sababu ni shambulio la utu wao. Na ukaguzi wa aina hiyo- ni unyanyasaji wa kijinsia.
"Mila hizi zimepitwa na wakati na tunastahili kuzitokomeza. Tunahitaji kupinga utamaduni ikiwa madhara yake ni uchungu."
Karma Nirvana, shirika la usaidizi ambalo linasaidia waathirika wa unyanyasaji wa heshima, pia limesaidia wanawake 19 walioathiriwa na upimaji wa ubikira tangu 2021 na wanataka kuongeza ufahamu kwamba utaratibu huo ni kinyume cha sheria.
Mkurugenzi Natasha Ratu alisema anaelewa kuwa utaratibu huo unaweza kusababisha "maumivu ya kisaikolojia na kiwewe" na wanawake wanapaswa kujua vipimo vya ubikira "si vya msingi wa ushahidi".
Alisema jamii inapaswa "kuondoa wazo la ubikira na sio watambulisha wanawake kwa hali yao ya kijinsia".
Taarifa na mwongozo kwa taaluma za matibabu zimeundwa na serikali ya Wales ili kuwasaidia kutambua ishara za aina hii ya unyanyasaji.
"Nadhani hili ni jambo ambalo huenda halijaangaziwa vya kutosha," Afisa Muuguzi Mkuu wa Wales Sue Tranka alisema.
"Haya si mazungumzo rahisi, ni nyeti sana na unataka kuhakikisha kuwa unasaidia wanawake na wasichana kuzungumza juu ya mada hii.
"Tunahitaji kuikemea. Tunahitaji kufanya hivyo kwa njia salama zaidi, na tunahitaji kuwaangalia waathirika wetu."