Kutoka Ghana hadi Ujerumani:Kufuatilia mmiliki wa pochi iliyopotea

th
Iliyochapishwa

Pochi hiyo nyeusi ya plastiki iliyopatikana katika kisiwa cha Italia cha Lampedusa ilikuwa imebebwa kilomita 3,500 (maili 2,200) kutoka Ghana na kisha kuenekana kutupwa.

Kuifungua, uso wa Richard Opoku ulinitazama kutoka kwenye kona ya leseni yake ya udereva.

Ilikuwa ni moja ya nyaraka za kibinafsi, za watu mbalimbali, ambazo zilikusanywa kwa muda kutoka kwenye tovuti ambapo boti ndogo zinazotumiwa na wahamiaji kuvuka Mediterania zilikuwa zimetupwa.

Ilikuwa imepatikana miaka kadhaa iliyopita na udadisi wangu ulichochewa - nilitaka kujua hadithi ya leseni.

Ni nini kilikuwa kimempata Richard Opoku?

Pochi hiyo ilikuwa sehemu ya mkusanyiko wa vitu vilivyopotea ambavyo hutumika kama makumbusho kwa kumbukumbu ya makumi ya maelfu ambao wamehatarisha maisha yao kuvuka Mediterania kutoka Afrika Kaskazini hadi Lampedusa.

Jaketi za kuokoa maisha, vyungu vya kupikia, chupa za maji, taa na kanda za kaseti zimepangwa vizuri kwenye rafu na kando ya kuta za chumba hiki karibu na bandari ya kisiwa.

Vitu hivi vya kila siku vimekusanywa na kikundi cha watu wa kujitolea tangu 2009.

"Wengine wanaleta udongo. Wanauleta kutoka nchi yao," anasema Giacomo Sferlazzo, mmoja wa wale walio nyuma ya mkusanyiko huo, huku akishikilia pakiti ndogo nyeupe ya nailoni.

"Tumepata idadi ya vifurushi hivi vidogo vinavyoonyesha uhusiano na nchi ya mtu barani Afrika."

Kisha anatoa folda kubwa iliyojaa picha, pasi za kusafiria, leseni za udereva na barua, ikiwa ni pamoja na hati ya Bw Opoku.

th
Maelezo ya picha, Wasamaria wema wa Lampedusa wamekuwa wakikusanya na kuonyesha vitu vya kibinafsi vyaa baadhi ya wahamiaji tangu 2009.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Karibu na Afrika kuliko Ulaya, Lampedusa - kisiwa kidogo cha uvuvi na kitalii chenye watu wapatao 6,000 - kwa muda mrefu imekuwa sehemu ya kuwasili kwa wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta maisha mapya.

Kila mwaka, maelfu ya watu huhatarisha maisha yao wakijaribu kuelekea Ulaya.

Mnamo Machi pekee, zaidi ya watu 3,000 walifika Lampedusa, zaidi ya mara mbili ya waliofika katika mwezi huo huo mwaka jana.

Huku kukiwa na zaidi ya vifo 20,000 vilivyorekodiwa na kupotea tangu 2014, eneo hili la Mediterania limekuwa njia hatari zaidi ya uhamiaji duniani.

Lakini Bw Opoku anaweza kuwa miongoni mwa walionusurika na nitarudi Ghana kujaribu kuchukua mkondo.

Ninasafiri hadi eneo la kati la Brong Ahafo, ambako idadi kubwa ya watu hhama.

Labda mtu hapa alikuwa amekutana na Bw Opoku walipokuwa wakisafiri kuelekea kaskazini.

Baadhi ya familia bado zinasubiri kusikia kutoka kwa jamaa zao tangu walipoondoka miaka mingi iliyopita.

Rita Ohenewaah anatarajia habari kutoka kwa mumewe ambaye alijaribu kuvuka bahari ya Mediterania kutoka Libya hadi Lampedusa mnamo 2016.

Alisikia kutoka kwake mara ya mwisho alipopiga simu kutoka Libya mnamo Desemba mwaka huo.

"Aliniambia angetuma pesa kupitia kwa mtu ambaye alikuwa akisafiri kwenda Ghana. Pia aliahidi kuongeza simu ya mkononi na nguo za Krismasi kwa watoto. Alipiga simu asubuhi na jioni siku hiyo. Sikumsikia tena."

Kama yeye, iliwezekana kwamba kulikuwa na mke au jamaa aliyekuwa akingoja habari za Bw Opoku.

Kwenye mji mkuu wa Ghana, Accra, kuna mfululizo wa kufadhaika kwani sheria za ulinzi wa data na vikwazo vya urasimu vinanizuia kujua zaidi kuhusu mtu huyu.

Lakini baada ya miezi ya kutafuta – mafanikio yanakuja

Frank Apronti wa Kituo cha Utaalamu wa Ulaghai wa Hati cha Huduma ya Uhamiaji ya Ghana anafanikiwa kupata nambari ya simu ya jamaa wa mmiliki wa leseni ya kuendesha gari.

Ni dada yake ambaye ananiunganisha na kaka yake ambaye ananiambia kuwa bado yuko hai na anaishi Ujerumani.

Ninapompigia simu Bw Opoku, anashtuka ninapomwambia kwamba nilikuwa nimepata leseni yake ya udereva huko Lampedusa.

Inageuka kuwa alikuwa ameipoteza mnamo 2011 na hakutarajia kuipata tena. Kwa kweli, haamini kuwa ninayo hadi nishiriki picha yake.

Hatimaye nasafiri kwenda Ujerumani kukutana naye.

th
Maelezo ya picha, Richard Opoku alirejeshewa leseni yake ya udereva miaka 11 baada ya kuipoteza kwenye boti

Asubuhi ya majira ya baridi kali, ananikaribisha katika nyumba yake ndogo ya chumba kimoja cha kulala, nje kidogo ya jiji la kaskazini mwa Ujerumani la Bremen.

Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 40 sasa anafanya kazi huko kama dereva wa lori la forklift.

Alipokuwa Ghana alifanya kazi kwa muda kama mchimba dhahabu haramu, au galamsey kama wanavyojulikana, ili kutafuta pesa kwa ajili ya safari yake.

Mwaka 2009, alipoamua kuelekea Ulaya, anasema alijua hatari ambazo safari hiyo ingehusisha, lakini alihisi haikuwa hatari zaidi kuliko kazi aliyokuwa akifanya nchini Ghana.

Safari zalifanya azurure eneo lote alipokuwa akijaribu kupata pesa ili kuendelea.

Kwanza alikwenda Cotonou katika Benin iliyo karibu, na kisha Lagos katika nchi jirani ya Nigeria, ambako alipata pesa kwa kuendesha pikipiki iliyobeba abiria kuzunguka jiji hilo kubwa.

Kutoka huko alirudi Cotonou na kuelekea kaskazini hadi nchi jirani ya Niger na kufanya kazi katika mkahawa wa ndani kwa miezi miwili zaidi.

Lakini safari ya gari kuvuka jangwa kutoka Niger hadi Libya ilikuwa mtihani mkubwa zaidi bado. Alitumia pesa alizopata kufanya kazi Nigeria na Niger kulipa nauli.

Alistaajabu jinsi dereva alijua pa kwenda mahali pasipokuwa na barabara.

"Wakati mwingine utakutana na kikundi, watu wote 35 na dereva ... wote wamekufa."

Labda walikufa kwa kiu - hana uhakika.

"Maji ni kitu kama dhahabu au almasi katika safari. Labda siku nzima unakunywa mara moja au mbili tu."

Katika mpaka wa Chad, gari hilo lilisimamishwa na wahalifu na abiria kuvuliwa nguo na pesa.

Bw Opoku alifaulu kuzuia pesa zake zisichukuliwe kwa kuzificha kwenye mwili wake.

Lakini shida zake hazijaisha mara tu alipofika Libya. Alitekwa nyara kwa ajili ya fidia na kupigwa kwa sababu hakuweza kufikia jamaa yake kulipa. Hatimaye, mwanamke aliyekuwa akitafuta mfanyakazi wa ndani alilipa ili aachiliwe.

th

Kisha mwaka wa 2011, miaka miwili baada ya kuondoka Ghana na katikati ya maasi dhidi ya kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi, Bw Opoku alipanda mashua mjini Tripoli kuvuka hadi Lampedusa.

Lakini katikati ya Bahari ya Mediterania, injini ya mashua hiyo ilizima. Bw Opoku na wasafiri wenzake walilazimika kutegemea rehema ya upepo hadi walipookolewa na walinzi wa pwani ya Italia.

Alipoteza leseni yake walipotia nanga kwenye ufuo wa Lampedusa.

Hapo awali waliwekwa kwenye kambi na kisha kuhamishiwa katika kituo cha wahamiaji huko Sicily. Mpango wake ulikuwa kuelekea Ujerumani, kwani alikuwa amesikia kutoka kwa Waghana wengine kwamba ilikuwa mahali pazuri kuishi.

Akiwa Italia, hata hivyo, aliomba hifadhi.

Ombi lake lilikataliwa awali, lakini anasema alifanikiwa kupata kibali cha kuwa Ulaya kama Umoja wa Mataifa ulipendekeza kwa Italia kwamba mtu yeyote aliyekimbia Libya wakati wa machafuko ya 2011 apate kibali cha kukaa kwa mwaka mmoja.

"Safari ilikuwa ngumu sana. Ilikuwa kuzimu," anasema.

"Lakini hakuna matumaini nyumbani kwa hivyo utavumilia maumivu na kuendelea."

Bw Opoku alikuwa amewazia maisha rahisi Ulaya, lakini anasema mambo hayakuwa hivyo.

“Nilipokuwa Afrika nilifikiri ulaya utapata pesa kirahisi lakini sio hivyo lazima ufanye kazi kwa bidii.

"Lakini nyumbani, hakukuwa na mpango wa mimi kuishi, kwa hivyo nitasema kuwa nashukuru kuwa hapa."