Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mgogoro wa Sudan: Mshtuko na hasira Khartoum, mji ambao haujazoea vita
Barabara za jiji la Khartoum mara nyingi hazikuwa na watu na msongamano wa magari siku ya Jumapili, huku pande zote zinazozozana zikiweka vizuizi barabarani.
Lakini misururu mirefu iliunda kwenye viwanda vya kuoka mikate na maduka machache ambayo yalisalia wazi, kwani baadhi ya watu walijitosa kwa muda mfupi kununua chakula kabla ya kurejea nyumbani kwa usalama.
Alasiri, kulisitishwa mapigano kwa kwa saa tatu baina ya wapiganaji ili kuruhusu maelfu ya watu waliofungiwa kuhama na kwa waliojeruhiwa kupata hospitali.
Miongoni mwa wakazi, kulikuwa na mshtuko - na pia hasira.
Tofauti na maeneo mengine ya nchi, kama vile eneo la magharibi la Darfur ambalo mara nyingi lina machafuko, Khartoum haijazoea vita. Hii ni mara ya kwanza kwa watu katika mji mkuu kuona mapigano kama haya.
Mapema Jumapili, muungano wa madaktari wa Sudan ulisema takriban raia 17 wameuawa katika mji huo, lakini baada ya siku mbili za mapigano, idadi halisi ya waathiriwa huenda ikawa kubwa zaidi.
Mkazi wa Khartoum Kholood Khair aliambia BBC kwamba wakaazi hawawezi kuwa na uhakika wa usalama popote pale.
"Raia wote wamehimizwa kukaa nyumbani, lakini hiyo haijaweka kila mtu salama," alisema.
"Kuna watu wengi aidha wakiwa majumbani mwao au wakiwa ndani na karibu na nyumba zao, juu ya paa, kwenye bustani na kadhalika, ambao wamejeruhiwa au kuuawa kwa risasi iliyopotea."
Waathiriwa hao ni pamoja na raia wa India, Albert Augestine, ambaye alikuwa akifanya kazi nchini Sudan na alipigwa na risasi iliyopotea njia siku ya Jumamosi, ubalozi wa India ulisema.
Mapigano makali na milipuko iliendelea kulitikisa jiji hilo, ikiwa ni pamoja na katika maeneo yanayoshikiliwa na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), ikidokeza kwamba madai yao ya kudhibiti 90% ya Khartoum hayana msaada wowote.
Hamid Khalafallah, mtafiti na mchambuzi wa sera katika Taasisi ya Tahrir ya Sera ya Mashariki ya Kati mjini Khartoum, aliiambia BBC kwamba wanajeshi wa Sudan wanaonekana kulenga shabaha za mabomu ndani ya mji huo.
"Tuliamshwa na milio mikubwa ya risasi na milipuko ya mabomu, katika baadhi ya matukio hata zaidi ya jana," alisema, akiongeza kuwa ndege za kivita zimesikika angani.
"Kimsingi, wanajeshi wa Sudan wanajaribu kulenga maeneo ambayo wanamgambo wa Rapid Support Forces wanapatikana."
Bi Khair alisema jeshi la Sudan liliwaambia wakazi kwamba watakuwa wakifagia vitongoji kwa ajili ya vikosi vya RSF, ambao alisema walikuwa wamejikita katika maeneo yenye watu wengi.
Alisema anahofia hii inaweza kusababisha "mauaji ya kiholela".
Katharina von Schroeder kutoka Save the Children alikuwa amenaswa katika shule katika mji mkuu Khartoum tangu mapigano yalipoanza Jumamosi asubuhi.
"Kila mara tulipofikiri kwamba inatulia basi ghafla kuna kelele nyingine," aliambia BBC. "Milipuko mikali zaidi ilikuwa asubuhi ya leo tulipoona pia baadhi ya jeshi la anga likitumwa, au ndege za kivita, na tukaamua kushuka kwenye orofa kwa takriban saa moja."
Mapigano yamekuwa yakifanyika kote nchini, kuanzia Darfur magharibi, ambako wafanyakazi watatu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) waliuawa, hadi Bandari ya Sudan kwenye pwani ya Bahari Nyekundu mashariki mwa nchi hiyo.
Huko Bandari ya Sudan, wakaazi waliamka na milipuko, lakini baadaye mchana walisema mambo yalionekana kuwa tulivu.
"Niliamshwa na sauti ya ndege za kivita zikiruka juu ya mtaa wangu. Kuona ndege zikiwa angani RSF ilianza kuwalenga kwa makombora ya kutungulia ndege. Ardhi ilikuwa ikitetemeka. Tena familia yangu yote ilikusanyika katika chumba kimoja. Tulikuwa tunaogopa sana,” Othman Abu Bakr alisema.
Lakini sauti ya mapigano ilipungua baadaye na Bw Abu Bakr akasema alitoka nje na kuwaona wanajeshi wa jeshi wakisherehekea mitaani.
Hospitali mjini Khartoum zimekuwa zikijitahidi kukabiliana na ongezeko la idadi ya majeruhi, wakilalamikia ukosefu wa madaktari na miundombinu.
Huku Ijumaa ijayo ikiwa ni mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuanza kwa sikukuu ya Eid al-Fitr, raia wa Khartoum wanashangaa kama watakuwa na chochote cha kusherehekea.
Hata kabla ya ghasia kuzuka, kumekuwa na siku za mvutano huku wanachama wa RSF wakisambazwa tena nchini kote, katika hatua ambayo jeshi liliona kama tishio.
Mivutano hiyo ilivuruga utaratibu wa kawaida wa kujumuika wakati wa Ramadhani, huku watu wakishindwa kufuata desturi zao za kawaida za kusherehekea na kusali kila mwisho wa mfungo mrefu wa kila siku.
Wakati wa sikukuu ya Eid, watu huzunguka sana, wakiwatembelea wanafamilia, majirani na marafiki wa karibu, lakini yote hayo yana shaka mwaka huu.
Wanaposubiri matokeo, hasira za watu zimewalenga wanajeshi wawili katikati mwa mzozo - mkuu wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na kiongozi wa RSF Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo.
Ugomvi wao ulizuka juu ya mipango ya mabadiliko kutoka kwa jeshi hadi utawala wa kiraia.
Lakini hivi sasa, Wasudan wengi wanataka amani na utulivu zaidi kuliko kutamani demokrasia.