Simu iliyoibiwa kwenye treni yapatikana baada ya saa tatu kwa usaidizi wa 'Ramani ya Google'

Iliyochapishwa

Palani Swami, ni mfanyakazi aliyestaafu wa kutoka wilaya ya Kanyakumari, India - alikuwa amepanda treni ya Kanchipuram kutoka Nagercoil kwenda Trichy mapema asubuhi Jumapili, Februari 4.

Treni ilipopita kituo cha Nellie, aliamka na kugundua mkoba wake na simu yake ya mkononi vimeibiwa.

Mwanawe alimkamata mwizi huyo kwa kutumia teknolojia ya Google ya kufuatilia ramani na kupata vitu hivyo ikiwa ni pamoja na simu yake ya mkononi iliyoibiwa.

Akizungumza na BBC kuhusu tukio hilo, Raj Bhagat anasema alimwacha babake asubuhi mnamo Februari 4 na kurudi nyumbani baada ya kupanda treni ya Kanchipuram Express katika kituo cha Nagercoil kwenda Trichy.

“Asubuhi na mapema hakuna umati mkubwa kwenye kituo cha treni. Nilipigiwa simu na baba asubuhi ya saa tatu kutoka nambari nyingine.

Akasema simu yake ya mkononi na mkoba wake vimeibiwa na hakuweza kuvipata ndani ya treni. Pia, alisema mtu aliyekuwa amekaa naye kwenye treni hakuwepo.

Baba huyo alieleza wasiwasi wake, simu hiyo ya mkononi imeunganishwa na akaunti za benki na kuna uwezekano wa fedha kuibiwa.

Ramani za Google

''Kwa bahati nzuri, simu ya baba ilikuwa imeunganishwa na huduma ya ramani ya google ya kuonyesha simu ilipo na huduma hiyo ilikuwa iko wazi. Ikimaanisha naweza kujua sehemu ambapo simu iko,'' anaelezea Raj Bhagat.

“Simu ya baba ilionyesha iko kwenye njia ya reli. Nilifikiri huenda imeanguka, lakini baada ya muda mawimbi ya simu yalianza kutembea kwenye njia ya reli kuelekea hekalu la Nagar,” anasema.

“Tulitoa taarifa kwa polisi wa reli wa Nagercoil baada ya kugundua kuwa mtu ambaye aliiba simu, amepanda treni nyingine na alikuwa akirejea Nagercoil.

Polisi wa reli walituambia treni inakuja. Rafiki yangu na mimi tulikwenda kwenye kituo cha treni na kungojea iwasili.

''Treni ilipofika kituo cha Nagercoil, idadi kubwa ya abiria walishuka. Nilisimama kwenye lango kuu la kituo na kulitafuta begi ambalo baba alikuwa nalo, huku nikiangalia ramani ya google." alisema.

Mwizi alikamatwa vipi?

Raj Bhagat anasema abiria wote walitoka nje ya kituo cha treni, lakini hakuweza kumpata mwizi huyo.

“Baada ya treni kuwasili, basi liliondoka kwenye kituo hicho likiwa limebeba abiria. Tulilifuata basi baada ya kuthibitisha kuwa mwizi amepanda,” alisema.

"Tulifika kituo cha basi karibu saa tano asubuhi. Kulikuwa na karibu watu 200 kwenye kituo hicho, hivyo kumtafuta tena ikawa kazi ngumu. Rafiki yangu na mimi tulitafuta kila upande,” Raj Bhagwat anasema.

"Ramani ya Google ilionyesha simu ilikuwa umbali wa mita 2 kutoka pale nilipokuwa. Kulikuwa na madereva wa mabasi na makondakta wamesimama. Kulikuwa na mtu niliyemtilia shaka. Nilipomkaribia nililiona begi la baba mkononi mwake.

''Mimi na rafiki yangu tulimkamata mwizi. Baadaye watu walipokusanyika tuliichukua simu ya baba yangu kutoka kwenye begi lake," alisema.

Polisi walikuja kituo cha mabasi na kumhoji na kumkuta na simu ya mkononi, pesa taslimu rupia 1,000, funguo za gari na hedifoni za bluetooth. Tulimkabidhi mwizi kwa polisi na kurudi nyumbani."

Rajbhagat anasema yeye ni mtaalamu wa masuala ya kijiografia katika kampuni binafsi, aliweza kuelewa kwa urahisi ramani iliyoonyeshwa kwenye programu ya Ramani ya Google.

Inaweza kuwa vigumu kwa mtu wa kawaida kuitumia. Lakini mara tu unapoizoea, inakusaidia katika nyakati kama hizi," alisema.

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla