Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Atiq Ahmed: Maisha ya mwanasiasa 'mhalifu' wa India aliyeuawa mubashara kwenye TV
Mwezi uliopita, Atiq Ahmed, mmoja wa wanasiasa wenye utata wa kuogopwa zaidi nchini India, aliuawa kwa kupigwa risasi mubashara kwenye TV pamoja na kaka yake.
Mauaji hayo ya kushtua yaliashiria mwisho wa utawala wake wa miongo minne ya ugaidi huko Prayagraj, jiji lililojulikana kwa utamaduni wake tajiri. Soutik Biswas huko New Delhi na Vikas Pandey huko Prayagraj huunganisha maisha ya Ahmed yenye misukosuko, ambapo mipaka kati ya uhalifu na siasa ilikuwa membamba mno.
Januari 2005, Raju Pal, mbunge aliyetoka kuchaguliwa hivi karibuni, aliuawa kwa risasi wakati akisafiri katika mji wa kaskazini mwa India wa Prayagraj (zamani ulijulikana kama Allahabad) wakati magari mawili yalipotokea ghafla, na kusimama mbele ya gari lake aina ya Toyota SUV.
Wanaume zaidi ya nusu-dazeni waliruka na kuanza kufyatua risasi kwenye gari kwa Pal.
Madaktari walikuta risasi 19 mwilini mwake. Mbunge huyo, ambaye inadaiwa alikuwa na uhusiano wa karibu na watu wa chini, alikuwa ametoka kufunga ndoa siku tisa tu zilizopita.
Wakati huo, Atiq Ahmed alikuwa tayari ni mhalifu mtata anayeogopwa sana aliyegeuka kuwa mwanasiasa wa Prayagraj. Mwaka mmoja kabla ya mauaji hayo, alikuwa mbunge baada ya mihula mitano mfululizo kama mbunge kutoka mji katika jimbo la Uttar Pradesh.
Pal alidaiwa kuuawa kwa sababu alithubutu kumpinga Ahmed kwenye siasa. Ahmed alikuwa amemwacha kaka yake na gwiji mwenzake, Ashraf kiti chake cha jimbo la Allahabad Magharibi katika uchaguzi wa jimbo - na yeye kushinda - uchaguzi wa ubunge huko Phulpur jirani (jimbo lililomtoa waziri mkuu wa kwanza wa India, Jawaharlal Nehru).
Hata hivyo, Ashraf alishindwa uchaguzi kwa kura 4,000 dhidi ya Pal. Ikadaiwa Atiq na watu wake waliripotiwa kulipiza kisasi kwa kumuua Pal, na walitajwa kuwa washtakiwa wakuu katika kesi hiyo.
Mji wa Prayagraj ni maarufu kwa kuwa na watu mahiri kama wa mashairi, waimbaji, waandishi, wanasheria na wasanii wa filamu (Amitabh Bachchan gwiji wa filamu duniani kazaliwa hapa). NI sehemu tulivu iliyoficha mchanganyiko wa uhalifu na siasa.
Hakuna mtu aliyechangia umaarufu huu zaidi ya Atiq Ahmed. Nyumbani, alikuwa baba wa watoto watano, alifanya karamu za kifahari na kuandaa kwa marafiki zake.
Nje, inasemekana alipora mali na biashara, aliiba pesa kutoka kwa wafanyabiashara, alitoa hundi ghushi kununua vitu na kuwafanya wapinzani wake wateswe gerezani. Maafisa wengi wa polisi na wanasiasa waliripotiwa kumuunga mkono na kumsaidia. Hata mahakama zilionekana kuwa na tahadhari: mwaka 2012, majaji 10 wa mahakama kuu walijitoa kwenye kusikilizwa kwa kesi yake hasa kama apewe dhamana ama la.
Haishangazi kuona Ahmed Atiq alikuwa na rekodi ndefu za uhalifu Polisi. Alikuwa kiongozi wa kundi lililoitwa "Inter-State Gang 227" na alikuwa ana kesi karibu kesi 100, zikiwemo za mauaji na utekaji nyara. Hata hivyo muda mwingi alikuwa hawekwi kwenye mikono ya Polisi na alikuwa huru mtaani.
Idadi halisi ya uhalifu wa Ahmed ni kubwa zaidi kwa sababu "watu walimwogopa na hawakuripoti mamia ya kesi", anasema Lalji Shukla, afisa mkuu wa zamani wa polisi huko Prayagraj.
Hata hivyo, ilikuwa mwezi wa Machi mwaka huu ambapo Ahmed alipatikana na hatia katika kesi ya utekaji nyara na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela - kwa mara ya kwanza alikutwa na hatia.
Bw Shukla anahusisha kuchelewa huku kutiwa hatiani kwa Ahmed ni kwa sababu "aliuweka mfumo mfukoni".
"Mara kwa mara alikuwa akikosa kuhudhuria kesi mahakamani na kuwatisha mashahidi. Hata baadhi ya mashahidi ambao hawakumuogopa walichoka baada ya miaka mingi ya kuhairishwa kwa kesi na mahakama," alisema.
Lakini siku chache baada ya kuhukumiwa, usiku wa April 15, zama zake ziliisha kwa namna isiyofaa.
Ahmed na kaka yake waliuawa kwa kupigwa risasi huku tukio likishuhudiwa moja kwa moja. Ilikuwa nje ya hospitali ya Prayagraj mbele ya polisi zaidi ya kumi waliokuwa na silaha kumlinda.
Ndugu hao walikuwa wanashikiliwa na polisi na walikuwa wakizungumza na waandishi wa habari walipokuwa wakienda kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.
Polisi waliwakamata wanaume watatu ambao, walisema, waliamua kuwaua ndugu hao kwa sababu walitaka “kujipatia umaarufu katika ulimwengu wa uhalifu”. Mauaji hayo yalishtua nchi na serikali iliamuru uchunguzi ufanyike haraka.
"Hakuna mafia wanaweza kueneza ugaidi huko Uttar Pradesh tena," Yogi Adityanath, kiongozi wa Chama cha Bharatiya Janata (BJP) kinachoongoza Uttar Pradesh, alisema siku chache baada ya mauaji hayo. Ingawa hakumtaja moja kwa moja Ahmed Atiq.
Atiq Ahmed alizaliwa katika kitongoji chenye Waislam wengi huko Prayagraj mnamo 1962.
Hakuna mengi yanayojulikana kuhusu maisha yake ya awali mbali na ukweli kwamba aliacha shule akiwa sekondari na kujihusisha na uhalifu mdogo.
Kufikia mwaka 1979, hata hivyo, tayari Ahmed alionekana kuwa amekomaa. Alishtakiwa katika kesi ya mauaji, lakini mashtaka hayakuweza kuthibitishwa.
Katika muongo uliofuata, alikuwa tayari na sifa za uhalifu ukiwemo wizi, polisi wanasema. Aliiba vyuma kwenye yadi za reli, alijipatia kandarasi za serikali baada ya kuwatishia wakandarasi wenzie waliokuwa wanawania kazi pamoja. Alipora ardhi na mali za watu wengine. Pia alijiunga na genge lililoongozwa na jambazi aliyegeuka kuwa diwani wa manispaa aitwaye Shauq Ilahi, maarufu kwa jina la Chand Baba.
Kufikia mwaka 1989, Ahmed alikuwa anakodolea macho kazi ya siasa. Mshauri na mfuasi wake walitofautiana wakati wote wawili walipoijitosa kuwania ubunge katika jimbo lao mwaka huo. (IIahi alimtaka Ahmed asigombee; lakini alikataa.)
Wakati wa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, au pengine wakati wa mchakato wa kuhesabu kura (kukawa na ripoti za matokeo zinazokinzana), hapo kukazuka machafuko na vita vikali vya magenge katika mitaa ya jiji kati ya wafuasi wa wahalifu hao wenyewe kwa wenyewe ambao walikuwa wameshindikana.
Katika ghasia hizi, Ilahi, ambaye alikuwa mlengwa mkuu, aliuawa. Kwa kuuawa mpinzani wake ambaye alikuwa rafiki yake na mshauri wake, alijipatia ushindi mkubwa katika uchaguzi wake wa kwanza, na hapo ndipo umaarufu na ubabe wa Ahmed ulipojisimika rasmi.
Katika miongo mitatu iliyofuata, Ahmed alikua mhalifu mwanasiasa wa kuogopwa zaidi huko Prayagraj. Bw Shukla anakumbuka alimkamata mara tatu, kwa makosa mbalimbali ikiwemo ya mauaji, lakini kila mara Ahmed alikuwa huru kwa dhamana. "Alikuwa na watu kila mahali. Kila mtu alimuogopa," anasema.