Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Ukraine: Mapigano yaendelea licha ya mapatano ya upande mmoja ya Putin kusitisha vita kwa muda
Usitishaji vita wa upande mmoja ulioitishwa na Vladimir Putin unaonekana kuwa na athari ndogo katika uwanja wa vita, huku maafisa wa Ukraine wakiwashutumu Warusi kwa kufyatua risasi katika maeneo kadhaa.
Mfanyakazi wa uokoaji wa Ukraine aliuawa katika mashambulizi hayo ya Urusi, wakati TV ya serikali ya Urusi ilisema mji wa Donetsk ulishambuliwa.
Urusi iliamuru kusitishwa kwa mapigano kwa saa 36, ili kusheherekea Krismasi ya Orthodox. Ukraine iliikataa ikisema huenda Moscow ikatumia ujanja huo kujiimarisha kijeshi.
Wizara ya ulinzi ya Urusi ilisisitiza kuwa ilikuwa inazingatia usitishaji wa amani kuanzia saa 12:00 saa za Moscow (09:00 GMT) siku ya Ijumaa. Ilisema vikosi vyake vilirudi kupambana baada ya jeshi la Ukraine kushambulia maeneo ya Urusi.
Tahadhari za anga ziliripotiwa kote Ukraine muda mfupi baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kuanza, na kisha gavana wa eneo la Kherson akasema mashambulizi kwenye kituo cha zimamoto uliwaacha yaliua maafisa kadhaa wa zimamoto huku watu wengine wanne wakijruhiwa katika mji mkuu, uliokombolewa mnamo Novemba na vikosi vya Ukraine.
Mji wa mashariki wa Kramatorsk pia ulishambuliwa na zaidi ya majengo kumi na mbili yaliharibiwa, maafisa wa Ukraine walisema.
Kiongozi wa eneo la Luhansk Serhiy Haidai alionya kwamba mapatano ya Krismasi ya Urusi ni "uongo na mtego", na kuwashauri wakaazi wasihudhurie ibada za Kanisa la Kiorthodoksi au kukusanyika katika maeneo yenye watu wengi kwani Warusi wanaweza kupanga "mashambulizi ya kigaidi".
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema mapatano hayo ni jaribio la kusitisha maendeleo ya kijeshi ya nchi yake mashariki mwa nchi hiyo, na kuongeza wapiganaji na vifaa zaidi.
Milio ya risasi ilisikika pande zote mbili za mstari wa mbele wa vita katika mji wa mashariki wa Bakhmut, ambapo vikosi vya Urusi vimewekeza sehemu kubwa ya nguvu zake huko katika jaribio la kuelekea Kramatorsk.
Kiongozi wa kundi la mamluki la Wagner wa Urusi, Yevgeny Prigozhin, alisema wiki hii kwamba raia wa Ukraine wamegeuza kila nyumba katika jiji hilo kuwa ngome. Picha za satelaiti zilizotolewa Ijumaa zilifichua athari za vita tangu Agosti mwaka jana.
Ingawa maafisa wa Urusi walisisitiza kuwa makubaliano hayo yataendelea, hakukuwa na dalili yoyote ya utulivu katika mapigano.
"Tuko saa mbili na nusu katika usitishaji vita uliotangazwa, na kwa hakika eneo lote la Ukraine liko chini ya tahadhari ya mashambulizi ya anga. Kwa hivyo nadhani hilo linajieleza lenyewe," Mbunge wa Ukraine, Inna Sovsun aliiambia BBC. "Kimsingi usitishaji mapigano, ni mbinu tu za Warusi."
Kanisa la Orthodox la Urusi - kubwa zaidi la Makanisa ya Orthodox ya Mashariki - huadhimisha Siku ya Krismasi mnamo Januari 7, kulingana na kalenda ya Julian.
Baadhi ya watu nchini Ukraine husherehekea Krismasi tarehe 25 Disemba, wengine 7 Januari. Siku zote mbili ni likizo ya umma nchini humo. Mwaka huu, kwa mara ya kwanza, Kanisa la Kiorthodoksi la Ukraine lilisema lingeruhusu makutaniko yake kusherehekea Krismasi mnamo tarehe 25 Desemba, kama yanavyofanya madhehebu mengine magharibi mwa Ukraine.