Fahamu jinsi mchakato mzima wa uchaguzi ulivyokuwa Kenya

Iliyochapishwa

Mamilioni ya Wakenya walijitokeza katika vituo mbalimbali vya kupiga kura Agosti 9, kushiriki katika shughuli ya upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu ambapo waliwachagua viongozi wao ikwemo rais mpya.

Hili ni zoezi linalofanyika kila baada ya miaka mitano kama ilivyo katika katiba.

Zoezi la uchaguzi la mwaka huu 2022, kulishuhudiwa raia wengi waliorauka alfajiri na mapema wakianza kupanga foleni wakiwa na lengo la kutimiza haki yao ya kikatiba.

Baadhi ya masuala yaliojadiliwa katika kipindi cha kampeni ilikuwa ni pamoja na Ukosefu wa ajira, gharama ya juu ya maisha na ufisadi.

Zaidi ya Wakenya milioni 22 walisajiliwa kushiriki katika shughuli hiyo katika zaidi ya vituo 40,000.

Na pia Rais anayeondoka madarakani alionekana kumpigia debe aliyekuwa mpinzani wake wa muda mrefu, Raila Odinga dhidi ya naibu wake William Ruto.

Raila Odinga alikuwa akitafuta uungwaji mkono kwa kushinikiza vita dhidi ya ufisadi katika kampeni yake huku naibu wake William Ruto naye akijihusisha zaidi na raia wa tabaka la chini akiwahakikishia kuinua hali yao ya maisha.

Hali ilivyokuwa katika baadhi ya maeneo

Vituo vya Kupiga kura katika maeneo mengi ya nchi vilifunguliwa mwendo wa saa kumi na mbili kamili asubuhi.

Ikawa ni pilkpilka za hapa na pale kila mmoja akijitahidi kutimiza ndoto yake kabla ya kukamilika kwa kuda uliowekwa.

Jijini Nairobi katika kituo kimoja huko Kibra, Mwandishi wa BBC Mercy Juma alipata picha ya mwanamke ambaye alikuwa amepanga foleni na mtoto wake wa miaka miwili kutoka saa kumi alfajiri saa za Kenya, licha ya baridi kali ya asubuhi kwa madai kwamba hakuwa na na mtu wa kumwachia mtoto wake nyumbani.

Hata hivyo hitalafu za hapa na pale hazikukosekena.

Kwenye kituo kimoja mjini Nairobi, raia walijawa na ghadhabu baada ya shughuli ya kupiga kura kukosa kuanza kwa wakati.

Baadhi ya wapiga kura walionya kuzua vurugu iwapo shughuli ya upigaji kura haitaanza.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu Dickens Olewe ulibani kwamba nyenzo za uchaguzi zilikuwa zimechelewa kuwasili.

Dosari nyingine iliyojitokeza ilikuwa ni vifaa vya kielektroniki vinavyokagua alama za vidole (vinavyojulikana kama vifaa vya Kiems) kuripotiwa kutofanya kazi vizuri katika maeneo tofauti.

Pia kuna wale walioambiwa kuwa majina yao yapo kwenye kituo kingine tofauti na walichokwenda kupiga kura.

Takriban wapiga kura 12,065,803 walikuwa wamejitokeza kupiga kura nchini Kenya sawa na asilimia 56.17 kufikia saa kumi jioni siku hiyo.

Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC ilisema idadi hiyo haijumuishi wale waliotambuliwa na sajili ya daftari.

Hata hivyo, siku ya kupiga kura kwa kiasi kikubwa ilikuwa ya amani.

 Tume ya uchaguzi ilikadiria waliojitokeza kupiga kura kuwa karibu 60%, ikiwa ni idadi ya chini ikilinganishwa na 80% iliyoonekana katika uchaguzi uliopita miaka mitano iliyopita.

Matokeo yalivyoanza kuhesabiwa

Punde tu baada ya muda wa kupiga kura kukamilika, shughuli ya kuhesabu kura ilianza.

Na ni wakati huo ambapo wakazi wa kaunti za Mombasa na Kakamega, walijua kuwa hawatakuwa na uchaguzi wa ugavana kwasababu ya mchanganyiko wa makaratasi ya kupiga kura ambao kwasasa umepangwa kufanyika Jumanne ijayo Agosti, 23.

IEBC ilijitetea kwa dosari hiyo ikisema halikuwa kosa lao na kuongeza kwamba, kampuni iliyopewa kandarasi ya kuchapisha makaratasi ya kupiga kura ndio iliochanganya makaratasi hayo.

Kilichojitokeza tangu awali kabisa, ilikuwa ni ushindani mkali kati ya mgombea wa Muungano wa Azimio Raila Odinga na naibu rais William Ruto wa muungano wa Kenya Kwanza.

Kwa zaidi ya 90% ya matokeo yaliyotumwa kutoka kwa maelfu ya vituo vya kupigia kura, hesabu za ndani zilionyesha pengo dogo sana kati ya wagombea hao wawili.

Ila kingine kilichotawala kwa haraka ilikuwa ni kuonekana kwa matokeo tofauti katika vituo mbali mbali vya utangazaji nchini Kenya.

Lakini tofauti na chaguzi zilizotangulia, wa mwaka huu Tume Huru ya Uchaguzi na mipaka ilikuwa imeweka fomu za matokeo ya 34A na 34B katika tovuti yake.

Vyombo vya habari, vyama vya kisiasa na hata raia waliweza kuzichukua fomu hizo na kuanza kujumlisha hesabu hizo wenyewe kwa wale ambao walitaka kujua au kukisia matokeo kabla hayajatangazwa.

Hiyo ndio sababu kubwa ya matokeo tofauti kwa sababu hakuna mpangilio maalum uliowekwa wa kufanana na kuzichukua fomu hizo.

Kila aliyefanya hesabu hizo anaanza na fomu alizochagua mwenyewe na kuzijumlisha na kisha kujitolea matokeo ya muda.

Na baada ya hapo raia walisalia kwa amani huku wakisubiri kutangazwa kwa matokeo rasmi ili kumjua mshindi hadi wafuasi wa Bw Odinga walipoingia katika eneo lililozuiliwa na kuwashambulia maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi, wakiwashutumu kwa kuvuruga kura.

Huku kukiwa na ghasia hizo, meneja mkuu wa kampeni za Bw Odinga aliweza kufika kwenye jukwaa lililotumiwa na maafisa wakuu wa tume ya uchaguzi, ambako alikosoa mchakato wa kuhakiki matokeo.

"Nataka kutangaza kwa taifa kwamba Bomas of Kenya ni eneo la uhalifu," alisema Saitabao Ole Kanchory, kabla ya kipaza sauti alichotumia kuzimwa na kuchukuliwa''.

Polisi wa kutuliza ghasia walitumwa ndani ya jengo hilo ili kuimarisha usalama.

Kutangazwa kwa mshindi

Muda mfupi tu kabla ya William Ruto kutangazwa kama rais mteule, palitokea jambo ambalo lilishtua raia.

Makamishna wanne wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) wakiongozwa na makamu mwenyekiti Juliana Cherera, walisema hawahusiki na uamuzi wa matokeo ya mwisho yaliyokuwa yakitangazwa na mwenyekiti wao Wafula Chebukati.

Wanne hao walipinga matokeo hayo ya uchaguzi wa tarehe 9, Agosti na kuahidi kutoa maelezo ya kina kuhusu ni nini haswa kilichotokea wakati wa kuhesabu kura hizo za urais.

Tume hiyo ina makamishna saba tu.

Akizungumza na vyombo vya Habari, makamu mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini Kenya Juliana Cherera alifafanua hoja zao zilizowafanya kufikia uamuzi huo.

Alidai kuwa ukiongeza asilimia kama ilivyotangazwa na mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati, jumla hiyo ilifika 100.01%.

Aliongeza kuwa matokeo ya kura za urais hayaakisi maoni ya makamishna, kwa sababu walipaswa kuyashughulikia kabla ya kutangazwa na hawakuweza kuyaona yote.

Aliongeza kuwa, majumuisho ya asilimia ya kura alizopewa kila mmoja wa wagombea urais wanne ilizidi asilimia 100.

"Hii inatupa jumla ya asilimia 100.01. Na inamaanisha takriban kura 142,000 ambazo zitafanya tofauti kubwa katika matokeo ya mwisho,'' Cherera alisema.

"Tulipotaka tuhakiki matokeo, mwenyekiti alikataa na kusisitiza kutangaza matokeo," Cherera aliongeza.

Hata hivyo licha ya madai hayo, sheria ya uchaguzi inampa mwenyekiti jukumu la kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais na Chebukati aliendelea kutekeleza jukumu hilo na kumtangaza mshindi.  

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini Kenya Wafula Chebukati aliyataja madai yaliotolewa na makamishna hao wanne wa tume hiyo kama ya uwongo.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Chebukati alisema kwamba makamishna hao walijaribu kulazimisha kufanyika kwa kura ya marudio kinyume na kiapo walichokula katika tume hiyo.

''Hiyo ni sawa na kupindua Katiba na mamlaka ya Wananchi wa Kenya'', alisema Chebukati akiongezea kwamba yeye kama mwenyekiti alikataa katakata ukiukaji wa katiba na akaendelea kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais kama yalivyopokelewa kutoka vituo mbalimbali vya kupigia kura.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja nchini Kenya Raila Odinga alipinga matokeo ya uchaguzi uliomtangaza naibu wa Rais William Ruto kuwa ndiye rais mteule.

Raila aliwataka wafuasi wake kudumisha amani na utulivu huku muungano huo ukifuata njia za kikatiba za kubatilisha matamshi ya Bw Chebukati.

''Jana, demokrasia yetu changa ilikumbwa na msukosuko mkubwa, kwa sababu hiyo, Kenya inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisheria na kisiasa kutokana na matendo ya Wafula Chebukati''.

Hadi kufikia sasa, wananchi wamekuwa wakisubiri kuona nini kitatokea na kuangazia zaidi Mahakama ya Juu Zaidi maana ndiyo yenye mamlaka ya kushughulikia kesi za aina hiyo kisheria, iwapo Raila Odinga atachukua mkondo huo.