Raila awasilisha masharti mapya huku Ruto akisisitiza hakutakuwa na 'handshake'

Iliyochapishwa

Na Abdalla Seif Dzungu

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga siku ya Jumapili alisitisha maandamano yaliokuwa yakifanyika siku ya Jumatatu na Alhamisi kila wiki dhidi ya serikali kufuatia ombi la Rais William Ruto la kumuita katika meza ya majadiliano.

Hatua ya rais Ruto inajiri baada ya shinikizo kutoka kwa viongozi wa dini pamoja na wale wa jamii ya kimataifa waliowataka wawili hao kukutana ili kuanza majadiliano ya kusuluhisha mzozo uliopo

Hii ni baada ya maandamano hayo kulemaza biashara nchini mbali na kulionesha taifa hili kama lililokumbwa na machafuko mbele ya jamii ya kimataifa.

Akizungumza katika hotuba yake kwa taifa, rais William Ruto alimuomba bwana Raila Odinga kusitisha maandamano hayo kwa lengo la kutafuta suluhu mbali na kuwaunganisha pamoja Wakenya.

Masharti mapya ya Raila Odinga

Hatahivyo akimjibu muda mchache baadaye kiongozi wa upinzani Raila Odinga aliitikia wito huo lakini akatoa masharti ambayo yangezunguka ajenda ya mazungumzo hayo.

Katika masharti hayo Kiongozi huyo wa upinzani alimtaka bwana Ruto kusitisha ukatamataji na uchunguzi ambao umekuwa ukiendelea dhidi ya waandamanaji nchini.

Vilevile bwana Raila alimtaka kiongozi huyo wa taifa kuwarudisha kazini makamishna wanne wa tume ya uchaguzi wa IEBC walioshinikizwa kuondoka katika tume hiyo hivi karibu kwa madai ya utendakazi mbaya wakati wa uchaguzi uliopita.

Bwana Raila alisema kwamba uundaji wa kamati ya bunge isioegemea upande wowote itakayofanya kazi nje ya bungee ndio njia pekee ambayo itaweza kusuluhisha mgogoro uliopo .

Vilevile aliitaka serikali ichukue hatua za haraka kupunguza gharama ya maisha na Rais Ruto kupanua mazungumzo yao zaidi ya bunge.

Aliongezea kwamba mchakato wa bunge hauwezi kushughulikia matatizo yao na kupendekeza kuundwa kwa timu sawa na ile ya mkataba wa Kitaifa wa 2008, ambao ulisimamiwa naaliyekuwa mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo Koffi Annan.

Mkuu huyo wa upinzani pia alidai kuwa kulikuwa na majaribio ya kuvuruga seva za uchaguzi, ambazo anataka zikaguliwe tena.

Rais Ruto: Kamwe hakutakuwa na handshake

Hatahivyo akizungumza nchini Rwanda, rais William Ruto alisisitiza kwamba hakutakuwa na makubaliano ya handshake kati yake na kiongozi wa Azimio Raila Odinga.

Akizungumza na vyombo vya habari mjini Kigali Rwanda siku ya Jumanne, kiongozi huyo wa taifa alisema hatua yake ya hivi karibuni kuanzisha mazungumzo na Muungano wa upinzani haikuwa njia ya serikali kuuleta upinzani ndani yake.

Wakati akijibu swali la mmoja wa waandishi wa habari wakati akizungumza na mwenyeji wake Rais Paul Kagame, Rais Ruto alisema: “Nataka niwaambieni hakutakuwa na kupeana mkono, bali kutakuwa na mazungumzo Bungeni kuhusu masuala ambayo wameinuliwa. Yale ambayo Bunge linaweza kuyatatua, yatasuluhishwa.”

Alibainisha kuwa Kenya ilikuwa taifa la kidemokrasia, ambapo ukaguzi na usawa unaimarishwa huku upande wa upinzani ukitekeleza jukumu lake la kuweka serikali kwenye vidole vyake.

Aliongezea: “Historia tuliyonayo ya kupeana mkono ni pale ambapo kulikuwa na muunganiko wa serikali na upinzani na matokeo yalikuwa mabaya. Hakukuwa na uwajibikaji wowote, mfumo mzima uliharibika, na watu wa Kenya hawataki hali ambapo demokrasia inahujumiwa," aliongeza.