Nchi ya Afrika iliyo na kiwango cha juu cha watu wanaojitoa uhai duniani

Nyumbani kwa Matlohang Moloi
    • Author, Andre Lombard
    • Nafasi, BBC Focus on Africa, Hlotse & Maseru
    • Akiripoti kutoka, Lesotho
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Kufika nyumbani kwa Matlohang Moloi mwenye umri wa miaka 79, unapitia miteremko kutoka barabara kuu hadi maeneo ya milima inayoifanya Lesotho kuwa miongoni mwa nchi zilizo katika maeneo ya juu zaidi duniani.

Mama wa watoto 10 ananikaribisha kwenye nyumba yake nadhifu, kunionyesha picha za familia yake. Niko hapa kuzungumza naye kuhusu mmoja wa watoto wake hasa - mwanawe wa kwanza, Tlohang.

Akiwa na umri wa miaka 38 alikua sehemu ya takwimu mbaya. Lesotho, taifa linaloongozwa na utawala wa kifalme, linaongoza kwa kuwa na kiwango cha juu zaidi cha watu wanaojitoa uhai.

"Tlohang alikuwa mtoto mzuri. Alikuwa ameniambia kuhusu matatizo yake ya afya ya akili," Bi Moloi anasema.

“Hata siku hiyo alijitoa uhai, alinijia na kuniambia ‘mama ipo siku utasikia nimejitoa uhai wangu’.

“Kifo chake kiliniuma sana, natamani angenieleza kwa undani zaidi kilichokuwa kinamsumbua akilini mwake, alikuwa na wasiwasi watu wakijua kinachomsumbua watafikiria yeye ni mtu dhaifu asiyeweza kutatua matatizo yake mwenyewe. "

Tlohang's ID card.
Maelezo ya picha, Tlohang, mwana wa kiume wa Matlohang, alijitoa uhai

Kulingana na Shirika la Afya Duniani, watu 87.5 kati ya 100,000 ya watu hujitoa uhai kila mwaka nchini Lesotho.

Nchi inayofuata kwenye orodha hiyo ni Guyana huko Amerika Kusini, ambapo idadi hiyo ni zaidi ya 40.

Pia ni karibu mara 10 ya wastani wa kimataifa, ambao unafikia watu tisa wanaojiua kwa kila watu 100,000.

Hii ni takwimu ambayo mashirika yasio ya kiserikali - kama vile HelpLesotho - zimedhamiria kubadilisha, kwa kuwapa vijana ujuzi wa kuimarisha afya zao za akili.

Katika mji wa Hlotse, uliopo mwendo wa kama saa mbili kwa gari kutoka mji mkuu, Maseru, mimi hushiriki kikao cha kawaida cha matibabu ya kikundi cha wanawake vijana, kinachoendeshwa na mhudumu wa kijamii Lineo Raphoka.

"Watu wanadhani tunaenda kinyume na desturi zetu za Kiafrika, mitazamo yetu ya kitamaduni, imani yetu ya kidini kama Waafrika, na kama jamii kwa ujumla," Patience mwenye umri wa miaka 24 anaambia kikundi.

"Lakini pia tunaepuka ukweli kwamba inafanyika. Ninazusema hivi kwa sababu nimepoteza marafiki watatu walioamua kujitoa uhai, binafsi nimejaribu."

Social worker Lineo Raphoka supports people with mental health struggles who have contemplated suicide.
Maelezo ya picha, Lineo Raphoka naendesha vikao vya tiba ya kikundi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kila mmoja hapa amewahi kuingiwa na mawazo ya kujitoa uhai ama wanajua watu waliofariki kutokana na visa kama hivyo.

Ntsoaki mwenye umri wa miaka 35 anajawa na hisia, anaposimulia kikundi kisa cha jinsi alivyobakwa hospitalini.

"Daktari aliniambia kuwa navutia sana. Kisha akatoa bunduki na kuniambia alitaka kujiburudisha nami, na nisipofanya hivyo angeniua.

"Kila wakati niliingiwa na mawazo ya kujiua, siku zote nilifikiri kuwa ndiyo suluhisho pekee. Sikuweza kufanya hivyo, sikuwa na nguvu ya kufanya hivyo. Kitu pekee ambacho kilinifanya niendelee na maisha au kuwa hai ni nyuso za ndugu zangu. Wanaamini mimi " nina uwezo, lakini mimi ni dhaifu."

Kikundi kinamhakikishia kuwaamefanya vyema kushiriki hisia zake.

Kipindi kinapoisha, wanawake wote wanapiga soga na kutabasamu, wakisema wanajisikia vizuri kushiriki hadithi zao.

Kinachowafanya watu kujitoa uhai ni vigumua kuelewa, sababu ni zaidi ya moja. Licha ya hayo, Bi Raphoka anasema anaona mifumo inayoeleza ni kwa nini Lesotho hasa ina kiwango cha juu cha watu wanaojitoa uhai.

"Kuna baadhi ya watu wanapitia msongo wa mawazo unaotokana na hali kama vile ubakaji, ukosefu wa ajira, na kupoteza wapendwa wao kupitia kifo. Hali hiizi zinawafanya kuingilia utumizi wa dawa za kulevya na pombe."

Kulingana na ripoti ya World Population Review mwaka 2022, 86% ya wanawake nchini Lesotho wamepitia ukatili wa kijinsia.

Wakati huo huo Benki ya Dunia inasema vijana wawili kati ya watano hawana ajira au elimu.

"Hawapati usaidizi wa kutosha kutoka kwa familia zao, marafiki au aina yoyote ya uhusiano walio nao," Bi Raphoka anaendelea kusema.

Ni jambo ambalo mara nyingi utasikia nchini Lesotho. Watu husema mara kwa mara kwamba hawajisikii vizuri kuzungumza juu ya afya yao ya akili - na kwamba wengine wanaweza kuwahukumu.

Nikiwa nimeketi katika baa moja huko Hlotse jioni moja, ambapo wateja wa kiume hunywa pombe ya kienyeji na kupiga gumzo wakifuatilia mpira wa miguu unachezwa kwenye TV, ninaanzisha mazungumzo kuhusu afya ya akili.

"Tunazungumzia hali hiyo, tunaambizana tufungue mioyo yetu," Khosi Mpiti ananiambia.

Khosi Mpiti na rafiki yake wakizungumza na BBC
Maelezo ya picha, Khosi Mpiti (kushoto) anasema wanaume wamepiga hatua katika juhudi za kusaidiana kimawazo

Wengine wanahofia kwamba wakifichua mengi wanaweza kusengenywa, licha ya hayo, anasema wamepiga hatua katika juhudi hizo na kwamba mambo yanakuwa mazuri.

"Kama kundi [la marafiki] tunasaidiana sana. Nikiwa na tatizo nawaambia wenzangu, na tunasaidiana."

Ingawa watu wanatafuta msaada, wanakabiliwa na changamoto nyingine - mfumo wa afya wa umma usiokidhi mahitaji.

Kitengo pekee cha magonjwa ya akili nchini humo mwaka jana kilishutumiwa na ombudsman - afisa ambaye kazi yake ni kuangalia maslahi ya umma - kwa kutokuwa na daktari wa magonjwa ya akili tangu 2017. Pia aliangazia dhuluma zilizoenea, ikiwa ni pamoja na "hali ya maisha ambayo inakiuka haki za binadamu" .

Hapo awali pia hakukuwa na sera ya kitaifa ya afya ya akili kushughulikia mzozo huo, ingawa serikali - iliyochaguliwa Oktoba 2022 - inasema kwa sasa iko katika mchakato wa kushughuliakia suala hilo.

"Afya ya akili imekuwa janga," anakubali Mokhothu Makhalanyane, mbunge anayeongoza kamati ya bunge inayoshughulikia masuala ya afya.

Mokhothu Makhalanyane
Maelezo ya picha, Mbunge Mokhothu Makhalanyane anasema kukomesha unyanyapaa kutaleta mabadiliko makubwa

"Tunahakikisha kwamba uhamasishaji umeimarishwa, kuanzia shule za msingi, shule za upili, hadi mahali ambapo vijana hukusanyika, kama vile mashindano ya kandanda," anaambia BBC.

"Sera hiyo pia itakuwa mahususi katika suala la matibabu, na kutoa nafasi kwa walioathirika kupata ushauri nasaha"

Pia anasema Lesotho inaweza kujifunza kutokana na vita vyake dhidi ya VVU/UKIMWI.

Mnamo mwaka wa 2016, ikawa nchi ya kwanza kuanzisha mkakati wa "kupima-na-kutibu", kumaanisha kuwa watu wanaweza kuanza matibabu mara tu wanapogunduliwa. Viwango vya maambukizi vimepungua mara kwa mara.

"Uzoefu tuliokuwa nao ni kwamba kuzungumza kwa uwazi, na bila kuwalaumu au kuwakosoa watu kwa hali zao, kulisaidia kubadilisha mitazamo."

Huku milimani, Bi Moloi akitembea mwendo mfupi ili kutunza kaburi la Tlohang.

Mahali pake pa kupumzika pana mandhari ya kuvutia.

Bi Moloi akiwa kwenye kaburi la mwanawe, Tlohang.
Maelezo ya picha, Mtoto wa Matlohang Moloi amezikwa mbali kidogo na nyumbani kwake

Bi Moloi ni mmoja wa watu wengi nchini Lesotho ambao wanakabiliana na huzuni baada ya wapendwa wao kujitoa uhai.

Tunapomaliza mazungumzo yetu ana ujumbe kwa wale wanajikuta katika hali kama yake.

"Ninawaambia watu kuwa kujitoa uhai sio suluhu kamwe. Unachotakiwa kufanya ni kuzungumza na watu walio karibu nawe ili wakusaidie."

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi