Fahamu mambo matano ya kipekee katika jamii ya wapemba nchini Kenya

    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

Ni hivi majuzi ambapo Jamii ya Wapemba wanaoishi nchini Kenya walitambuliwa rasmi kuwa kati ya makabila zaidi ya arubaini yalioko nchini humo, na pia kujumuishwa kati ya jamii 16 za waswahili wa pwani nchini kenya.

Kwa hatua hio jamii hi imeendelea kusherehekea na kutumai kwamba siku zijazo na vizazi vijavyo watapata haki za kimsingi za kurasimishwa kwao.

Kikosi cha wanahabari wa shirika la BBC kutoka Kenya kilifunga safari kuelekea kijiji cha Kichaka Mkwaju Eneo hili lililopo Kaunti ya Kwale wanasema ni sehemu ambao iliteuliwa na wazee wa kipemba wa kijadi kuwa makao makuu yao , kwani asilimia 99 ya watu wanaoishi huko ni wapemba.

Kwa mujibu wa Mwalimu Ali mkasha ambaye ni katibu Mwenezi wa jamii ya wapemba waliopo Kenya ni kwamba wamepambana kuimarisha mila na desturi za kale za jamii hio, zinazowatofautisha na jamii nyengine za uswahilini zinazoishi Pwani ya Kenya. Katibu huyo alitupataia mambo 5 tusiyoyafahamu kuhusu jamii ya wapemba nchini Kenya.

Matumizi ya lahaja za lugha ya mama katika lugha ya kiswahili

Japo wanakiri wanazungumza Kiswahili , wanasisistiza kwamba wameingiza lahaja za lugha ya mama katika matamshi yao , ambayo ikiwa mtu ni mgeni huenda akakosa kuelewa mdahalo kati ya wapemba wenyewe ,ila tu awe na mkalimani. Kwa mfano majina kama Mchele wanatamka ‘chele’ , Mama wanatamka ‘mamengwa’ , chakula cha mchana kinaitwa ,vishuka’, chakula cha jioni ni ‘kijio’ , kutafuta wanasema ‘kuzinga’ , kuzungumza ni ‘kutongoa’ na kadhalika wanasema kwa kutumia lahaja katika matumizi ya lugha ya kiswahili chao kinakuwa tofauti na jamii nyengine za waswahili .

Matumizi ya viungo katika mapisho yao yote

Katika mapishi ya wapemba , wanasema kuwa kuanzia kiamsha kinywa hadi chakula cha jioni wanatumia viungo tofauti vinavyotumiwa kama dawa au tiba pia. wanaamini kuwa mapishi yote yanafaa kufanyiwa katika jiko la mawe matatu , au kwa kutumia kuni pekee .

Ngoma na densi zinatumika sana kuwasilisha msimu na mavuno

Wakati wa mavuno , wapemba wanangoma na densi spesheli za kufurahia mazao kutoka mashamba yao , ngoma hii na michezo huchezwa maalumu na kina mama ambao wako kwenye ndoa , kina mama hawa pia wanangoma maalum ambazo huwasuta wachache katika jamii ambao hawakufanya bidii mashambani na hawana chakula kwa kukosa kulima kwa wakati ufaao.

Mchezo maalum wa ‘mnara mnara ’

Huu ni mchezo maalum unaochezwa na wanawake walioko kwenye ndoa kwa wapemba wanafahamika kama mamengwa . mchezo huu huchezwa na wanawake ambao hukaa kwa kuunda mzunguko , huku kila mmoja akiwa na jiwe ndogo mkononi , wanapigisha jiwe hilo ardhini huku wakiwa wamechuchumaa na kuyazungusha kutoka kwa mwanamke mmoja kwa mwengine , huku wakiimba nyimbo za kumsuta yeyote aliyekuwa mvivu wakati wa kupanda mashambani .

Wanaume wanabeba mikoba , wamama vikapu

Katika jamii ya wapemba wanaume hubeba mikoba , mikoba hii huwa na stakabadhi tofauti , pamoja na vitu vya maana kwa kwao , upande mwengine wanawake hubeba vikapu mle ndani utapata jembe na vifaa vengine vya kuendea shambani , wanaume pia hufika sokoni kununua bidhaa mbalimbali ambazo wanaweka ndani ya vikapu yao au ‘posta’ kama wanavyoviita.