Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kupigwa marufuku kwa dawa ya nguvu za kiume Tanzania 'Mkongo' kwazua gumzo mtandaoni
Na Veronica Mapunda
BBC Swahili ,Dar es Salaam
Julai tarehe 27 Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini Tanzania lilipiga marufuku matumizi na kuifutia usajili dawa ya Hensha maarufu kama ‘mkongo’ ambayo iliuzwa kwa msingi wa kusaidia kuboresha nguvu za kiume.
Baraza hilo limeitaka kampuni inayotoa dawa hiyo kuhakikisha inaondolewa sokoni mara moja vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watengenezaji wa dawa hiyo.
Dawa ya Hensha ‘Mkongo’
Ni dawa ya asili inayotengenezwa na kituo cha Nyasosi Traditional Clinic cha jijini Dar es Salaam ambacho hutengeneza dawa mbalimbali za asili
Ilijipatia umaarufu nchini Tanzania, wengi waliitumia hata kuleta mzaha katika mitandao ya kijami huku baadhi wakiipa jina la ‘Vumbi la Kongo’
Dawa hii kawaida hutengenezwa kutokana na mchanganyiko wa majani, mizizi na magome ya mti wa Mkongo unaosemekana kupatikana katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Inauzwa na wazalishaji wengine chini ya majina tofauti ya chapa Na iliyopigwa marufuku yenye usajili namba TZ17TM0027
Kupigwa kwake marufuku kumezua maoni mchanganyiko katika mitandao ya kijamii huku wengine wakiendeleza mzaha juu ya dawa hiyo.
Kwanini ‘Mkongo’ imepigwa marufuku
Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini humo Profesa Hamis Malepo alitoa sababu za dawa hiyo kupigwa marufuku ambazo zilizingatia uchunguzi waliofanya hivi karibuni wa dawa za tiba asilia zilizo sokoni.
Ambapo baadhi ya vitu walivyogundua ni
• Kubainika kwa uwepo kwa mapungufu madogo hasa kwenye uandishi wa lebo na vifungashio.
• Pia dawa hiyo imegunduliwa kuwa imechanganywa na dawa ya kisasa ya nguvu za kiume iitwayo sildenafil, kwa jina maarufu la biashara Viagra ama Erector kitendo ambacho ni kinyume cha sheria na miongozo ya usajili wa dawa za tiba asili na tiba mbadala.
• Kuchanganywa kwa dawa mbili na vimelea ambavyo ni kiashiria cha hali duni ya usafi wa mazingira ya kutengenezea dawa.
Je kuna sababu nyingine zaidi?
Baraza linasema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 15(1) cha kanuni ya dawa asili ya mwaka 2008,” kinabainisha kuwa ni kosa kutangaza dawa na huduma ya tiba asili na tiba mbadala bila kuwa na usajili na ithibati ya bara.
Mkongo ni dawa iliyojipatia umaarufu katika mitandao ya kijami lakini pia kituo kinachotengeneza dawa hiyo kimekuwa kikifanya matangazo na kutengeneza maudhui mbali mbali kuhusu dawa inazotengeneza katika mtandao wa Youtube.
Mwenyekiti wa baraza anasema mtu anayehitaji kutangaza dawa yake ni lazima afuate utaratibu wa kusajili dawa kwa kupima ubora, usalama na baadae kuomba kibali cha matangazo kutoka katika baraza hilo.
Kifungu cha 13(1) kinasema kuwa baraza lina wajibu wa kuziondoa dawa ambazo usalama na ubora wake haupo katika viwango sahihi kama ambavyo limefanya kupitia dawa ya mkongo
Wananchi wanahimizwa kutumia tiba lishe zinazoboresha afya ili kujikinga na maradhi ya aina mbalimbali.
Tanzania inahimiza matumizi ya dawa za asili na mwaka 2020 iliidhinisha uuzaji na utumiaji wa dawa tano za kienyeji sokoni za kuongeza nguvu za kiume.