Katika tamasha la muziki Israel, miili 260 yapatikana

Iliyochapishwa

Wapenzi wa muziki walikuwa wakitazama kwa hamu tamasha la Supernova, lililofanyika jangwani kusini mwa Israeli - likienda sanjari na sherehe ya Kiyahudi ya Sukkot.

"Wakati umefika ambapo familia zitakusanyika tena," waandalizi waliandika kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kuanza. "Furaha kubwa itakuwa!"

Saa chache baadaye, kurasa zao za mitandao ya kijamii zilijaza watu waliohamanika wakijaribu kutafuta wapendwa wao, baada ya wanamgambo wa Kipalestina kuvamia tamasha hilo na kufyatua risasi.

Zaidi ya miili 260 imeripotiwa kupatikana katika eneo la tamasha, kulingana na shirika la uokoaji Zaka.

Simulizi za Waathirika

Mshiriki mmoja, anayeitwa Ortel, alisema ishara ya kwanza kwamba kuna kitu kibaya ni wakati king'ora kilipolia alfajiri, onyo kuhusu roketi. Walioshuhudia wanasema roketi hizo zilifuatwa na milio ya risasi.

"Walizima umeme na ghafla wakaanza kufyatua risasi kila upande," aliiambia Channel 12 ya Israel. "Magaidi 50 walifika wakiwa kwenye magari - wamevalia sare za kijeshi," alisema.

Watu walijaribu kukimbia kwenye mchanga na kuingia kwenye magari yao ili kuondoka. Washiriki wa sherehe wanasema kulikuwa na magari yaliyojaa watu wenye bunduki, wakifyatua risasi.

“Walirusha milipuko, ikafika mahali kila mtu akasimamisha gari lake na kuanza kukimbia, nikaingia kwenye kichaka, wakaanza kushambulia watu, nikaona majeruhi wengi. Nikiwa katika mti nikijaribu kutafakari nini kinaendelea."

Eneo la tamasha - lenye majukwa tatu, eneo la kambi, baa na eneo la chakula - lilikuwa katika jangwa la Negev, karibu na Kibbutz Re'im. Sio mbali na Ukanda wa Gaza, ambapo wapiganaji wa Hamas walivuka alfajiri na kuanzisha mashambulizi yao. Walijipenyeza katika miji na vijiji, wakichukua mateka makumi ya watu.

Mshiriki wa tamasha Adam Barel aliiambia Haaretz - kila mtu kwenye tamasha alikuwa akifahamu kuwa kuna uwezekano wa kurushwa roketi katika eneo hilo.

Kama wengine wengi, alijaribu kutoroka kutumia gari lake - lakini watu wenye bunduki walikuwa wakiwafyatulia risasi, kwa hivyo alitoka na kukimbia. "Watu walipigwa risasi. Tulijificha. Kila mtu alikimbia."

Esther Borochov aliambia Reuters - alikuwa akiendesha gari lake wakati liliposhambuliwa. Alimwona kijana akiendesha gari lingine, ambaye alimwambia aingie. Akaingia - lakini mwanamume huyo alipigwa risasi. Esther anasema alijifanya amekufa hadi alipookolewa na jeshi la Israeli.

Wahudhuriaji wengi wa tamasha - kama Ortel - walijificha kwenye vichaka kwa saa nyingi, wakisubiri wanajeshi kuwasili na kuwaokoa.

"Niliitoa simu yangu sauti, kisha nikaanza kutambaa kwenye shamba la michungwa," Ortel alisema. "Risasi zilikuwa zikipiga juu yangu."

Gili Yoskovich aliiambia BBC jinsi alivyojificha kwenye bustani ya mabalungi." Walikuwa wakienda mti kwa mti na kupiga risasi. Niliona watu wanakufa pande zote. Nilikaa kimya. Sikulia, sikufanya chochote."

Hatimaye, baada ya saa tatu, alisikia baadhi ya sauti za askari wa Israel, na kuamua kukimbia hadi mahali salama.

Shahidi mwingine aliiambia Channel 12 ilikuwa "saa nne hadi tano za sinema ya kutisha. Tulikimbia kama vichaa."

"Ni mauaji," alisema Yaniv, daktari wa dharura . Aliliambia shirika la utangazaji la umma la Kan News:

"Sijawahi kuona kitu kama hicho maishani mwangu. Ni shambulizi lililopangwa. Watu walipokuwa wanakimbia kupitia mlango wa dharura, vikundi vya magaidi vilikuwa vinawasubiri na kuanza kuwachukua.

"Kulikuwa na watu 3,000 kwenye hafla hiyo, kwa hivyo labda walijua. Walikuwa na habari za kijasusi."

Familia Za Waliopotea

Miongoni mwa waliotoweka ni Muingereza Jake Marlowe, 26, alikuwa akifanya kazi kama mlinzi katika hafla hiyo, na mtalii wa Ujerumani, Shani Louk, ambaye mama yake anaamini alitekwa nyara.

Mwanamke mwingine, Noa Argamani mwenye umri wa miaka 25 anaaminika kutekwa katika tamasha hilo, familia yake na marafiki wanasema.

Rafiki wa Noa, Amit Parpara, aliambia BBC alikuwa akimtumia ujumbe alipokuwa mafichoni.

"Saa 2:30 ndio ujumbe wa mwisho niliupokea kutoka kwake," alisema. Baadaye Amit aliona video kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha akichukuliwa mateka.

"Inamuonyesha akiwa kwenye pikipiki, akichukuliwa kutoka kwa mpenzi wake. Unaweza kuona hofu yake akipelekwa Ukanda wa Gaza."

Wazazi wa Mmarekani-Israel Hersh Golberg-Polin mwenye umri wa miaka 23 pia wanamtafuta mtoto wao wa kiume, alikuwepo katika tamasha baada ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.

Waliambia Jerusalem Post kwamba walipokea jumbe fupi mbili kutoka kwake Jumamosi asubuhi zikisomeka: "Nakupenda" na "samahani."

Takriban Waisraeli 700 wameuawa tangu mashambulizi hayo kuanza, kulingana na taarifa za hivi punde katika vyombo vya habari vya ndani.

Mapigano kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Kipalestina yanaendelea, na Israel imeanzisha mashambulizi ya anga huko Gaza. Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya takriban watu 413, maafisa wa Palestina wanasema.