Baraza la Mawaziri Tanzania: Karata za uchaguzi 2024, 2025 na mtihani wa usawa wa kijinsia

    • Author, Na Rashid Abdullah
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

Jumatano Agosti 30, 2023 Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alilifanyia mabadiliko madogo baraza lake la mawaziri. Si mabadiliko ya kwanza tangu aingie madarakani Machi 2021.

Kila wakati ambapo baraza la mawaziri linabadilika, kuna matokeo ya aina tatu hujitokeza; Mawaziri hubadilishwa kutoka wizara moja na kupelekwa wizara nyingine. Pili, mawaziri huondoshwa katika nafasi zao moja kwa moja na tatu, mawaziri wapya huingizwa.

Mabadiliko haya yamekuja na matokeo kama hayo. Vilevile, wapo wanaohusisha panga pangua hii na uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025!

Historia yajirudia

Dkt. Stergomena Lawrence Tax aliandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, nafasi ambayo haikuwahi kushikwa na mwanamke katika historia ya Tanzania tangu kupatikana uhuru wa nchi wakati huo ikiitwa Tanganyika.

Aliteuliwa wakati wa mabadiliko ya pili ya baraza la mawaziri yalipofanyika, Septemba 2021, kufuatia kuteuliwa kuwa mbunge wa Bunge la Tanzania. Awali alikuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Dkt. Stergomena amerejeshwa katika wizara ya Ulinzi, kutoka wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Hii ina maana kwamba ile historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kushikilia wizara hiyo, anaendelea kuishikilia mwenyewe.

Tangu uhuru wa Tanganyika na baadaye kuundwa Tanzania upatikane, nafasi ya Naibu Waziri Mkuu imeshikwa na watu watatu. Mabadiliko haya yameweka historia kwa kumfanya Dkt. Dotto Buteko kuwa mtu wa tatu kushika wadhifa huo.

Mwanasiasa mkongwe pia mwanadiplomasia, Dkt. Salim Ahmed Salim aliwahi kuwa Naibu Waziri Mkuu, mwaka 1986 hadi 1989, wakati Waziri Mkuu akiwa Jaji Joseph Warioba, na baadaye Cleopa Msuya chini ya uongozi wa Rais Ali Hassan Mwinyi.

Mwanasiasa aliyeanza safari yake ya kisiasa katika chama tawala CCM kisha akawa upinzani, mwendazake Augustino Lyatonga Mrema, alishika wadhifa wa Naibu Waziri Mkuu kutoka 1993 hadi 1995 wakati huo wa Rais Mwinyi.

Jambo lingine, si mara ya kwanza kwa rais Samia kufanya mabadiliko ya kimuundo katika Wizara. Mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri yaliyofanyika Januari 2022, yalikuja na wizara mpya ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu.

Mabadiliko ya wakati huu pia yamekuja na Wizara mpya kwa kufuta Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na kuunda wizara mpya mbili; Wizara ya Ujenzi na Wizara Uchukuzi. Ujenzi amepewa Innocent Bashungwa na Uchukuzi akikabidhiwa Profesa Makame Mbarawa.

Safari ya usawa wa kijinsia

Septemba 15, 2021 akihutubia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia, katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, Rais Samia aliweka wazi mkakati wake wa kuendelea kuwateua wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi na kushughulikia haki za wanawake na usawa wa kijinsia.

Katika eneo la naibu mawaziri, kuna naibu waziri mwanamke mmoja miongoni mwa watano walioteuliwa– Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalumu (Ruvuma), akiteuliwa kuwa naibu waziri wa Nishati.

Kuna watu watatu walioondoshwa katika nafasi zao. Wawili ni manaibu mawaziri – mmoja ni mwanamke – alikuwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mary Masanja, nafasi yake inachukuliwa na Dunstan Kitandula.

Waziri aliyeondolewa, ni mwanamke, Dtk. Angelina Mabula, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, nafasi yake imechukuliwa na mbunge wa Ukonga, Jerry Slaa.

Kwa hesabu za haraharaka hii inaifanya idadi ya wanawake katika baraza la mawaziri kupungua huku idadi ya wanaume ikiongezeka katika nafasi zote mbili; uwaziri na unaibu waziri. Mabadiliko haya ya sasa, yanadhihirisha kwamba malengo ya kuleta usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi yana safari ndefu kuyafikia.

Ni dhahiri kuwa utekelezaji wa dhamira ya Rais Samia ya kuleta usawa wa kijinsia inakwenda kwa hatua za kwenda mbele na kurudi nyuma. Katika nchi jirani, serikali ya Rwanda inasifika barani Afrika na duniani kwa kuwa na uwakilishi mkubwa wa wanawake.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, katika ripoti yake ya Novemba 2020, takriban theluthi mbili ya Bunge la Rwanda ni wanawake, huku baraza la mawaziri likiwa na asilimia 52 ya wanawake.

Mabadiliko kuelekea 2024 na 2025

Mtaji wa vyama vya upinzani katika kampeni za uchaguzi, hujengwa kwa msururu wa ahadi ambazo huzitoa kwa wapiga kura – ikiwa watachaguliwa watafanya hiki na kile. Vilevile, hukumbushia namna rais wa wakati huo alivyotekeleza ahadi na mipango na kufanikiwa kuleta ustawi wa watu au alivyoshindwa.

Kwa upande mwingine, rais aliyepo madarakani hujenga ushawishi wake ili ateuliwe tena kwa kutekeleza mambo kadhaa yenye manufaa kwa watu – hasa yale ambayo aliyaahidi wakati wa kampeni au hata baada ya kuingia Ikulu.

Yumkini kuna tafsiri nyingi kwanini Rais Samia ameamua kuongeza idadi ya naibu mawaziri, kuongeza wizara na kuteua Naibu Waziri Mkuu – ila moja kati ya hizo tafsiri ni msukumo wa kujaribu kuongeza kasi ya utendaji wa serikali yake.

Mambo mengi yakitelekezwa katika kipindi hiki kuelekea 2024 na 2025 – yatakuwa ni mtaji wa kuwaeleza wapiga kura wakati wa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu. Hawa ni wateule ambao kwa hesabu za kisiasa wanaweza kumsaidia kufanikisha azma hiyo.