Vita vya Ukraine : Madai katika hotuba ya Putin yahakikiwa

Putin akihutubia taifa

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Reality Check
    • Nafasi, BBC News
  • Iliyochapishwa

Rais Vladimir Putin alihutubia umma wa Urusi katika hotuba ya kitaifa iliyodumu kwa karibu saa mbili.

Katika hotuba hiyo, alitoa madai kadhaa kuhusu vita vya Ukraine na alikosoa sana nchi za Magharibi.

Tumeangalia baadhi ya kauli zake.

"Utawala wa Nazi mamboleo ulioanzishwa nchini Ukraine baada ya 2014"

Bw Putin amerudia mara kwa mara madai yasiyo na msingi kuhusu "utawala wa Nazi mamboleo" nchini Ukraine kama uhalali wa uvamizi wa Urusi nchini humo.

Katika uchaguzi uliopita wa bunge wa Ukraine mwaka 2019, uungwaji mkono kwa wagombea wa siasa kali za mrengo wa kulia ulikuwa 2%, chini sana kuliko katika nchi nyingine nyingi za Ulaya.

Ikumbukwe pia kwamba Rais Volodymyr Zelensky ni Myahudi na watu wa familia yake walikufa katika mauaji ya Holocaust.

Lakini kumekuwa na makundi ya mrengo mkali wa kulia nchini Ukraine - yenye hadhi ya juu zaidi ni Azov ambayo imeonesha kuunga mkono itikadi ya Nazi.

Iliundwa kupinga watu wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi, ambao waliteka maeneo ya mashariki mwa Ukraine mnamo 2014, na baadaye kuchukuliwa kama kitengo ndani ya jeshi la Ukraine.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Moja ya brigedi za jeshi la Kiukreni ... ilipewa jina la Edelweiss, kama kitengo cha Hitler"

Hapa, Bw Putin alilinganisha kitengo cha jeshi la Ukraine na Idara ya 1 ya Milima ya Wanazi - ambayo ilikuwa na ua la Edelweiss kwenye alama yake na kufanya uhalifu wa kivita katika Vita vya Pili vya Dunia.

Mnamo tarehe 14 Februari, Rais Zelensky aliipa Brigedi ya 10 ya Mashambulizi ya Milimani jina la heshima: Edelweiss.

Siku iliyofuata, Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi ilionesha hii kama "ushahidi" wa Wanazi huko Ukraine katika tweet.

Lakini ua la Edelweiss - ambalo huota katika maeneo ya Alpine - limetumika kama ishara na vitengo vingine vya kijeshi vya mlima vya Ulaya, ikiwa ni pamoja na Huduma ya Uokoaji ya Milimani ya Croatia, majenerali wa Jeshi la Uswizi na Brigade ya 21 ya Rifles ya Poland.

Hata Urusi ilikuwa na kitengo maalum kilichoitwa Edelweiss. Kikosi cha 17 cha madhumuni maalum cha Rosgvardia kilipewa jina hili mnamo 2011. Jina lilibadilishwa kuwa Avanguard mnamo 2016.

"Pia tunakumbuka majaribio ya serikali ya Kyiv kupata silaha za nyuklia, kwa sababu walizungumza kuhusu hilo hadharani."

Hakuna ushahidi kwamba Ukraine imejaribu kupata silaha za nyuklia, na Bw Putin ambaye ametoa madai haya hapo awali hakutoa ushahidi wowote.

Ilipokuwa sehemu ya Muungano wa Kisovieti wa zamani, silaha za nyuklia zilikuwa nchini Ukraine, lakini mwaka wa 1994 Ukraine ilitia saini Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Nyuklia na kuziacha, ili kurudisha dhamana ya usalama.

Mnamo 2021, balozi wa Ukraine nchini Ujerumani, Andriy Melnyk, alisema kwamba ikiwa Ukraine haiwezi kujiunga na Nato, inaweza kulazimika kufikiria upya kutokuwa na nyuklia.

Mnamo 2022, Rais Zelensky alisema kwamba ingawa Ukraine "imeachana" na uwezo wake wa nyuklia, "haina usalama".

Lakini serikali ya Ukraine haijaeleza nia ya kupata silaha za nyuklia na hati ya mkakati wa kijeshi iliyochapishwa mwaka 2021 haikurejelea hilo.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya nyuklia, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), linasema halijaona dalili zozote nchini Ukraine za "kupotoshwa kwa nyenzo za nyuklia, zinazokusudiwa kwa shughuli za amani, kwa madhumuni mengine."

"Pato la Taifa mnamo 2022 limepungua kwa 2.1% tu na nitakukumbusha kwamba mnamo Februari au Machi walitabiri kuanguka kwa uchumi wa Urusi"

Kauli ya Bw Putin ni yakweli kwamba uchumi wa Urusi umeshuka chini ya ilivyotarajiwa.

Shirika la takwimu la Urusi linasema uchumi unaopimwa kwa Pato la Taifa ulipungua kwa 2.1%, ambayo ni karibu na makadirio ya 2.2% katika ripoti ya hivi karibuni kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Upungufu huo bado unaifanya kuwa nchi iliyofanya vibaya zaidi katika orodha ya IMF.

IMF ilisema kuwa biashara ya Urusi ilikuwa ikielekezwa kwa nchi ambazo hazijaiwekea vikwazo.

India na China zimekuwa wanunuzi wakubwa wa mafuta ya Urusi, kwa mfano, kwani mataifa ya Magharibi yanazuia ununuzi na kuweka vikwazo.

Mnamo Julai 2022, IMF ilikuwa ikitabiri kupungua kwa 6% katika Pato la Taifa la Urusi kwa mwaka huo.