Biden amtembelea Zelensky na kusema Putin "amekosea" juu ya vita vya Ukraine

Chanzo cha picha, UKRAINIAN PRESIDENTIAL PRESS SERVICE -HANDOUT
Marekani itaiunga mkono Ukraine katika vita vyake dhidi ya Urusi "haijalishi ni kwa muda mrefu kiasi gani", Rais wa Marekani Joe Biden amesema katika ziara ambayo haikutangazwa mjini Kyiv.
"Tuna imani kubwa kwamba utaendelea kushinda," alisema.
Safari ya kwanza ya Bw Biden nchini Ukraine kama rais inawadia siku chache kabla ya maadhimisho ya mwaka wa kwanza wa uvamizi wa Urusi.
Alisema kuwa Rais wa Urusi Vladimir Putin alikuwa "amekosea" kufikiria kuwa Urusi inaweza kuishinda Ukraine na washirika wake wa Magharibi.
Alikutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na wawili hao walitembelea eneo la kumbukumbu ya wanajeshi waliofariki katika kipindi cha miaka tisa tangu Urusi ilipotwaa eneo la Crimea na vikosi vyake vilivyomuunga mkono kutwaa sehemu za eneo la mashariki la Donbas.
Kuwepo kwa Bw Biden kulikusudiwa kuthibitisha tena "dhamira thabiti ya Marekani kwa demokrasia ya Ukraine, mamlaka yake na uadilifu wa eneo", kulingana na taarifa ya Ikulu ya White House.
Alikuwa amesafiri kwa treni kwa saa 10 kutoka Poland hadi kufika Kyiv kwa siri, kisha akarudi Poland.
Urusi ilifahamishwa kuhusu safari hiyo saa chache kabla ya kuondoka kwa Rais Biden kwa "madhumuni ya kumaliza mzozo", afisa wa Marekani alisema.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baada ya ziara hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alitangaza kifurushi kipya cha usaidizi wa usalama kwa Ukraine wenye thamani ya $450m (£373m), ikiwa ni pamoja na silaha za howiters, mfumo wa roketi wa Himars, makombora ya Javelin na rada za uchunguzi wa anga.
Marekani pia itaipatia Kyiv kutafuta msaada wa ziada wa $10m wa dharura ili kupata misaada ya nishati ya Ukraine, Bw Blinken alisema.
Marekani pia itaipatia Ukraine msaada wa ziada wa $10m wa dharura ili kudumisha miundombinu ya nishati, Bw Blinken alisema.
Bw Zelensky alisema ushindi wa Ukraine dhidi ya Urusi unategemea azimio na kwamba aliona azma kama hiyo kwa Bw Biden
"Ni sasa na nchini Ukraine kwenye hatima ya utaratibu wa dunia, ambayo ni msingi wa sheria, juu ya ubinadamu ... inaamuliwa," alisema
Aidha amesema viongozi hao wawili wamejadiliana kuhusu uwezekano wa kutuma silaha nyingine. Bw Zelensky amekuwa akitoa wito mara kwa mara wa ndege za kivita za F-16 kutumwa, jambo ambalo Marekani na washirika wengine hadi sasa wamegoma kuliidhinisha.
Akizungumzia safari hiyo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi Maria Zakharova alisema kushindwa kutawapata wale ambao, kama alivyosema, "waliuza roho zao kwa Wamarekani".
Katika tukio ambalo liliongeza mshangao katika ziara hiyo ya hadhi ya juu zaidi nchini Ukraine tangu vita kuanza, ving'ora vya mashambulizi ya anga vililia wakati Rais Biden na Bw Zelensky wakiwa katika Kanisa Kuu la St Michael's Cathedral katikati mwa Kyiv.
Ving'ora vinasikika mara kwa mara mjini.

Chanzo cha picha, Reuters
Wakati viongozi wengine wa dunia wameitembelea Ukraine katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kujitokeza kwa rais wa Marekani mjini Kyiv wakati wa vita ambavyo wanajeshi wa Marekani hawapigani ni onyesho la umoja wakati ambapo Urusi inasema uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa Ukraine unapungua.
Ziara hiyo ilikaribishwa na watu wa Ukraine huko Kyiv.
"Ninashukuru sana kwa msaada wake - ina maana kubwa kwetu," Roksoliana Gera aliiambia BBC. "Nashukuru ujasiri wake, kwamba alichukua changamoto hii na kuja kuonyesha uungwaji mkono wa taifa la Marekani."
Oleksandra Soloviova alisema ziara hiyo ilionyesha Urusi kwamba "Marekani inatuunga mkono na itaendelea kutuunga mkono, kwa vikwazo na zana za kijeshi".
Mkuu wa wafanyikazi wa rais wa Ukraine, Andriy Yermak, alisema ziara hiyo imekuwa ya kimkakati na ya kihistoria.
“Masuala mengi yanatatuliwa na yale ambayo yamekwama yataharakishwa,” alisema.
Marekani ni mojawapo ya washirika wakubwa wa Ukraine na idara ya serikali hadi sasa imetangaza $24.9bn kama msaada wa kijeshi.
Mnamo Januari, Bw Biden alitangaza kwamba Marekani itatuma vifaru 31 vya kivita na makombora ya masafa marefu pia yako njiani.
Hata hivyo, kuna mgawanyiko wa kisiasa unaokua nchini Marekani kuhusu kiasi cha misaada ambayo Ukraine inapaswa kupokea katika siku zijazo.
Ziara ya Rais Biden mjini Kyiv ilifanyika kabla ya ziara ya siku tatu nchini Poland ambapo atakutana na Rais wa nchi hiyo, Andrzej Duda, na wanachama wa Umoja wa Kijeshi wa Nato.
Katika hatua nyingine, waziri wa mambo ya nje wa China amesema Beijing ina wasi wasi mkubwa kutokana na kuongezeka kwa vita nchini Ukraine na hatari ambayo inaweza kuzuka bila kudhibitiwa.
"Tutaendelea kuhimiza amani na mazungumzo na kutoa hekima ya China kwa ajili ya suluhu la kisiasa la mgogoro wa Ukraine," Qin Gang aliambia kongamano mjini Beijing.
Awali, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alizungumza kuashiria kwamba China ilikuwa inafikiria kusambaza silaha na risasi kwa Urusi kwa ajili ya vita - madai ambayo yalikanushwa vikali na China.















