'Fursa kubwa hujitokeza pale mlango wa kwanza unapofungwa'

.

Chanzo cha picha, Anna Lunguya

    • Author, Elizabeth Kazibure
    • Nafasi, BBC Swahili, Dar es Salaam
    • Akiripoti kutoka, Dar es Salaam
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Anna Peter Lunguya hakuwahi kufikiria kwamba angejenga maisha yake katika tasnia ya mitindo.

Mwaka 2014, alihitimu shahada ya Computer Science akiwa na matumaini ya kupata kazi katika taaluma aliyosomea. Hata hivyo, hali ya soko la ajira ilimlazimu kutafuta njia nyingine ya kujikimu.

Badala ya kukata tamaa, aliamua kugeukia kipaji alichokuwa nacho tangu akiwa shuleni, ubunifu wa mavazi.

"Nilipokosa kazi nikaanza kuangalia upande wa pili, nina ujuzi gani, nikajikuta kwamba nina ujuzi wa mambo ya uanamitindo," anasema Anna.

Alianza rasmi safari yake mwaka 2017 kama fundi cherehani, akiwa na ujuzi mdogo wa ushonaji na bila uzoefu wa kuendesha biashara.

Mwanzo haukuwa rahisi.

Wakati huo, alikuwa akipokea oda kutoka kwa wateja na kuwapeleka mafundi wengine kuzitekeleza. Mara nyingi matokeo hayakuwa kama alivyotarajia.

"Unataka mtindo huu, na fundi anakushonea mtindo mwingine. Unapeleka kwa mteja, nguo imekosewa," anakumbuka.

Makosa hayo yalimgharimu baadhi ya wateja waliokuwa wamemuamini.

Mbali na changamoto ya kutokuwa na ujuzi wa kutosha katika ushonaji, Anna pia anasema alikuwa hana maarifa ya kutosha kuhusu biashara. Hivyo, alilazimika kujifunza hatua kwa hatua, kuanzia kushona na kukata nguo, kutengeneza bombwe hadi kuelewa misingi ya biashara.

"Katika kila kosa ambalo nilikuwa nafanya, ilibidi nikae chini niangalie katika huu ushonaji nahitaji kufanya nini. Nikaanza kujifunza taratibu," anasema.

Computer Science haikupotea

Ingawa aliondoka katika taaluma ya Computer Science, Anna anasema elimu hiyo imeendelea kuwa sehemu muhimu ya mafanikio yake katika mitindo.

Anatumia programu za kompyuta katika kubuni, mitandao ya kidijitali kutafuta fursa na kujifunza, pamoja na teknolojia katika kutengeneza maudhui na kufanya matangazo.

Pia anasema ujuzi huo umemsaidia kutumia akili mnemba yaani AI, katika ubunifu wa mitindo.

"Teknolojia imenisaidia kwa asilimia kubwa na imekuwa rahisi mimi hata namna ninavyotumia AI katika ubunifu wangu wa mavazi," anasema.

Kwa Anna, kuacha taaluma aliyosomea hakumaanishi kwamba miaka yake ya kusoma Computer Science ilipotea.

Badala yake, alitafuta namna ya kuunganisha maarifa hayo na taaluma yake mpya.

Anaona ujuzi wa teknolojia umemwezesha kuingia katika eneo la teknolojia ya mitindo an ubnifu katika teknolojia, pamoja na kutumia mifumo na programu mbalimbali katika biashara yake.

Kutoka Anna Collections hadi AFA

.

Chanzo cha picha, Anna Lunguya

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baada ya kujenga Anna Collections kwa miaka kadhaa, Anna aliona changamoto nyingine katika tasnia hiyo; upungufu wa ujuzi miongoni mwa watu waliotaka kuingia katika biashara ya mitindo.

Mwaka wa tano wa Anna Collections, wazo la kuanzisha Anna Collection Fashion Academy, maarufu kama AFA, lilianza.

Anna anasema watu wengi walikuwa wakimfuata wakitaka kujifunza na kupata ujuzi aliokuwa nao.

"Hakukuwa na chuo rasmi chenye weledi ambacho unaweza ukaenda ukasoma ukapata ujuzi ambao niko nao mimi," anasema.

AFA sasa ina miaka mitatu na, kulingana na Anna, imewafundisha zaidi ya wabunifu 2,000 kutoka Tanzania na nchi nyingine za Afrika, zikiwemo Congo, Zambia, Uganda, Zimbabwe na Kenya.

Lakini lengo lake si kuwafundisha wanafunzi kushona pekee.

Anasema chuo hicho kinawafundisha pia kuhusu biashara, ufungashaji wa bidhaa, ubora, masoko na namna ya kutafuta wateja.

"Tunabadilisha ile fikra ya zamani kuwa ushonaji ulikuwa ni kwamba ni kukaa kibarazani usubirie mteja aje," anasema.

Kwa baadhi ya wanafunzi, mafunzo hayo yamekuwa mwanzo wa kuajiriwa, huku wengine wakianzisha biashara zao wenyewe.

Anaona ubunifu wa mitindo kama mnyororo wa fursa

Anna anaamini bado kuna fursa nyingi ambazo hazijatumika kikamilifu katika tasnia ya mitindo Tanzania.

Anasema mtu anayeingia katika sekta hiyo si lazima awe mbunifu wa nguo pekee.

Kuna nafasi za kuwa mratibu wa mavazi, mtaalamu wa kutengeneza michoro ya vipimo vya mavazi, msambazaji wa bidhaa, mfanyakazi wa uzalishaji, mkaguzi wa viwango vya ubora, mtaalam wa masoko, muuzaji, mpiga picha au hata mmiliki wa kiwanda.

Kwa mtazamo wake, tasnia hiyo ina mnyororo mpana wa thamani unaoanzia kwa wazalishaji na wauzaji wa vitambaa hadi kwa mtumiaji wa mwisho.

"Ukishasema ubunifu wa mitindo, ni sehemu ndogo tu ambayo iko katika mnyororo mzima wa thamani," anasema.

Ndiyo maana mipango yake ya baadaye inaenda zaidi ya Anna Collections na AFA Academy.

Anataja pia AFA Machine Hub, AFA Fashion Night na mipango ya kuanzisha kiwanda.

Mafanikio si yake peke yake

Pamoja na kukua kwa biashara zake, Anna anasema hawezi kudai kwamba amefika hapo alipo kwa juhudi zake peke yake.

Anasisitiza umuhimu wa timu yake na anasema hapendi kuwaita watu wanaofanya naye kazi "wafanyakazi".

"Mimi huwa siwaiti wafanyakazi wangu, napenda kuwaita wafanyakazi wenzangu," anasema.

Kwa sasa, Anna anasema Anna Collections imeajiri watu 50.

Kwake, mafanikio si ukubwa wa biashara pekee, bali pia kuona watu wanaofanya kazi naye wakiboresha maisha yao.

Anasema anafurahia anaposikia mfanyakazi amefanikiwa kununua kiwanja au kupiga hatua nyingine kwenye maisha.

"Mafanikio yangu ni pamoja na kuwaona kwamba timu yangu iliyoko nyuma yangu, kwa pamoja tumeweza kufanikiwa," anasema.

Safari bado inaendelea

.

Chanzo cha picha, Anna Lunguya

Anna anakiri kwamba safari yake haijawa na mafanikio pekee.

Kabla ya AFA, alikuwa na chuo kingine alichokuwa amekiendesha kwa kushirikiana na mtu mwingine. Baada ya miaka miwili, mradi huo ulivunjika kutokana na kutofautiana kwa maono.

Alisema alihisi kukata tamaa na kuanza upya kutoka sifuri.

Lakini wanafunzi na wafanyakazi waliokuwa wamehusika katika mradi huo walipomfuata wakitaka kujua hatima yao, aliona bado anaweza kufanya jambo.

Ndipo AFA ilipoanzishwa kama mradi wake binafsi.

Leo, anaona ilivyokua na kusema imekuwa na mafanikio zaidi kuliko alivyotarajia.

"Anza kidogo, lakini usibaki kuwa mdogo."

Kwa vijana na wanawake wanaotaka kuanza biashara lakini wanaona changamoto za fedha au mazingira mengine kuwa kikwazo, Anna ana ujumbe mmoja: wasikate tamaa.

Anasema mafanikio wanayoyaona leo yanaweza kuficha miaka ya maumivu, hasara na nyakati za kukata tamaa.

"Wakati mwingine unaviona vitu vipo Anna Collection, mtu anaweza akaona vitu vimefanikiwa lakini nyuma yake kulikuwa na maumivu," anasema.

Anaamini pia watu wanapaswa kutumia fursa wanazopata, kujenga mahusiano mazuri na kuonyesha uwezo wao.

Na kwa wale wanaoanza kwa kiwango kidogo, ana ushauri mfupi: Anza kidogo, lakini usibaki kuwa mdogo.

Kwa Anna mwenyewe, safari yake imechukua miaka minane kufika alipo leo.

Lakini anaamini hakuna wakati mmoja unaofaa kwa kila mtu.

"Mimi imenichukua miaka nane kufika hapa nilipo lakini mwingine itamchukua miaka mitatu, watu tunatofautiana," anasema.