Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ukraine yajitahidi kurejesha umeme baada ya mashambulio ya Urusi
Ukraine imesema karibu yaasilimia 50 ya mahitaji ya umeme nchini humo yamekatizwa, baada ya mashambulizi makubwa ya makombora ya Urusi wiki hii.
Shirika la umeme la Ukrenergo limesema kipaumbele kilikuwa kurekebisha miundombinu muhimu lakini ukarabati huo sasa unachukua muda zaidi.
Rais Volodymyr Zelensky alisema "hali ngumu zaidi" ya umeme na usambazaji wa maji ilikuwa katika mikoa 15, ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa Kyiv.
Majira ya baridi kali inashuhudiwa kote nchini Ukraine, kukiwa na theluji na halijoto ya chini ya sufuri.
Kuna hofu watu wanaweza kufa kutokana na athari ya baridi kali.
Alhamisi asubuhi, karibu 70% ya wakaazi wa Kyiv walijpata bila nguvu za umeme.
Meya wa Kyiv Vitali Klitschko aliiambia BBC Ukraine kuwa haimaanishi "hali ni mbaya zaidi" kiasi cha jiji hilo kukosa kabisha huduma za umeme na maji.
Lakini baadaye siku hiyo mamlaka ya ya Ukraine ilisema kwamba usambazaji wa umeme na maji ulikuwa ukirejeshwa hatua kwa hatua katika mikoa yote.
"Maji yanaendelea kurudi polepole. Bado hakuna umeme," Roman, mkazi wa Kyiv, aliiambia BBC saa 15:00 saa za Ukraine(12:00 GMT) siku ya Alhamisi. Saa kadhaa baadaye, aliongeza: "Hatimaye, [mamlaka] imerudisha umeme - baada ya zaidi ya saa 24."
Tonya, Kyvan mwingine, aliambia BBC jioni ya Alhamisi kwamba hakuwa na umeme kwa saa 48
"Subiri kwa siku 120"
Mamlaka ya Ukraine inasema imeweka zaidi ya "vituo 4,000 vya dharura" - mahema ya moto ya muda ambapo watu wanaweza kuchaji simu zao na kunywa chai au kahawa.
Katika hotuba yake kwa taifa kupitia video usiku wa Alhamisi, Rais Zelensky alisema wanajeshi wa Urusi "hawajui kupigana".
Katika hotuba yake kwa taifa kupitia video usiku wa Alhamisi, Rais Zelensky alisema wanajeshi wa Urusi "hawajui kupigana".
Kitu pekee ambacho wanaweza kufanya ni ugaidi. Iwe ni ugaidi wa nishati, ugaidi wa mizinga, au ugaidi wa makombora – hayo ndiyo mambo wanayoweza kufanya-Urusi imeshusha hadhi ya viongozi wake wa sasa," alisema.
Wakati huo huo, Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine, Iryna Vereshchuk aliambia kipindi cha BBC World Tonight: "Urusi imeanzisha vita vya nishati dhidi yetu, lengo lake ni kuleta janga kubwa la kibinadamu. Changamoto kubwa kwetu ni makundi yaliyo hatarini zaidi - wazee, wanawake wenye watoto na wagonjwa hospitalini."
"Watu wetu wanapaswa kusubiri kwa siku 120, kwa sababu hizo ni siku za baridi, miezi ya baridi na hilo ndilo jambo ambalo Urusi inalenga. Inataka kuwatesa watu wetu wakati wa majira ya baridi."
Bi Vereshchuk alisema baadhi ya maeneo ya Ukraine - kama vile mji wa kusini wa Kherson - bado yanakabiliwa na mashambulizi ya kila siku, na kwamba serikali ya Ukraine tayari imeanza kuwahamisha watu kwa hiari.
Ukraine na washirika wake wa Magharibi wamesema mara kwa mara kwamba kwa kulenga miundombinu muhimu ya kiraia Urusi inafanya uhalifu wa kivita - shutuma zilizokanushwa na Moscow.
Siku ya Alhamisi, msemaji wa Rais wa Urusi Vladimir Putin, Dmitry Peskov alipendekeza kwamba viongozi wa Ukraine wanaweza kumaliza "mateso ya wakazi wa eneo hilo" kwa kutimiza matakwa ya Urusi ya kumaliza vita ambavyo Moscow ilianza tarehe 24 Februari.
Akijibu hili, msaidizi wa rais wa Ukraine Mykhailo Podolyak alitweet: "Kutoa wito wa amani wakati unarusha makombora katika miji yenye amani – Ni kiwango cha juu zaidi cha matatizo ya kiakili."