Unasumbuliwa na ukungu wa ubongo? fahamu njia ya kutatua tatizo hilo

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

1. Jipende na ujihurumie

Maisha yanapokuwa na shughuli nyingi na viwango vya msongo wa mawazo kuongezeka, si jambo la kushangaza kujikuta ukiingia kwenye chumba na kusahau ulikuwa unaenda kufanya nini, kupoteza mwelekeo wa mawazo katikati ya sentensi au kushindwa kuwa na umakinifu.

Hasa baada ya wikendi, inaweza kuwa vigumu kurejea katika hali ya kufanya kazi au kusoma.

Hali hii ya ukungu wa kiakili, ambayo mara nyingi huitwa "brain fog" kwa kiingereza, si ugonjwa wa kiafya wenyewe. Badala yake, ni mkusanyiko wa dalili zinazohusiana na utendaji wa ubongo, kukosa umakini, kusahau mambo na kuhisi mawazo yako yanaenda taratibu.

Sababu zinazoweza kusababisha hali hii ni pamoja na kukoma kwa hedhi au kipindi cha kuelekea kukoma kwa hedhi pamoja na hali kama Covid na magonjwa ya kingamwili kama lupus. Hata hivyo, brain fog inaweza pia kukupata unapokuwa na mambo mengi sana yanayokusumbua kwa wakati mmoja.

Daktari wa tiba na mtaalamu wa kipindi cha Morning Live, Dkt. Tharaka, ana vidokezo hivi vinne vinavyoweza kukusaidia kuondoa hali hii ya ukungu wa akili.

Ukungu wa ubongo unaweza kumpata mtu yeyote na si ishara ya kushindwa wala kwamba huwezi kukabiliana na maisha.

Mara nyingi, ni njia tu ambayo ubongo wako unatumia kukuambia kwamba umechoka, una msongo wa mawazo au umelemewa na mambo mengi kwa wakati mmoja.

Jikumbushe kwamba ukungu wa ubongo kwa kawaida huwa ya muda tu, na ni sawa kupunguza kasi ya kufanya mambo, kugawa majukumu kwa wengine au kuomba msaada unapouhitaji.

Ikiwa una wasiwasi kuhusu hali hiyo, unapaswa kuwasiliana na daktari.

2. Tengeneza ratiba

Punguza uchovu unaotokana na kufanya maamuzi mengi kwa kuwa na ratiba maalum ya kila siku. Muundo unaotabirika wa siku unaweza kupunguza mzigo kwenye kumbukumbu yako ya muda mfupi.

Kujua kinachofuata kunaondoa hitaji la ubongo wako kuendelea kujiuliza, "Leo ninafanya nini?"

Ni vyema kuwa na ratiba ya asubuhi na jioni. Hata jambo rahisi kama kuandaa nguo utakazovaa au kuandaa kifungua kinywa mapema linaweza kuipa akili nafasi ya kupumzika kutokana na kufanya maamuzi kila mara.

3. Pumzika

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Chukua mapumziko mara kwa mara ili kuupa ubongo wako nafasi ya kupumzika. Unapohisi umepoteza umakini au mawazo yako yamekuwa mazito, simama kidogo, pumua na uondoke kwenye kazi unayofanya kwa muda.

Ni rahisi kujaza ratiba yako kwa shughuli zinazofuatana bila nafasi ya kupumua mikutano, hafla za kijamii, shughuli za kila siku na majukumu mbalimbali bila kuacha muda wa kupumzika.

Lakini kuendelea kufanya shughuli moja hadi nyingine bila mapumziko kunaweza kuufanya ubongo ukose muda wa kujirekebisha, jambo linaloweza kuongeza uwezekano wa kupata brain fog, yaani ukungu wa akili.

Jaribu kupanga kwa makusudi mapumziko mafupi kati ya shughuli zako, hata kama ni dakika 5 au 10 tu za kujinyoosha, kunywa maji au kinywaji, kutoka nje kidogo au kukaa kimya.

Fikiria mapumziko haya kama "kinga za kiakili",yanaipa ubongo wako nafasi ya kuchakata kile ambacho umemaliza kufanya, kuachilia msongo wa mawazo uliobaki na kujiandaa kwa shughuli inayofuata.

4. Tumia kalenda na vikumbusho

Kujaribu kukumbuka kila miradi, kazi na jambo muhimu kichwani kunaweza kusababisha msongamano wa mawazo na kusahau mambo kwa urahisi.

Acha teknolojia ikusaidie kukumbuka, tumia kalenda na vikumbusho ili kupunguza mzigo kwenye akili yako.

Panga majukumu yanayojirudia ili yafanyike kwa utaratibu. Kwa mfano, tenga muda wa chakula cha mchana kwenye kalenda yako kila siku au weka vikumbusho vya kila wiki vya kulipa gharama na kufanya kazi za nyumbani.

Hii inamaanisha hutalazimika kuendelea kujiuliza, "Ni jambo gani ninapaswa kukumbuka baadaye?"

Swans

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Pamoja na mikakati hii ya kila siku, Dkt. T pia anapendekeza kutumia kifupi cha maneno SWANS ili kukusaidia kuimarisha afya ya ubongo na kuongeza umakini.

Kila herufi inawakilisha tabia muhimu inayoweza kusaidia kuondoa ukungu wa akili na kuufanya ubongo wako ufanye kazi kwa ufanisi zaidi:

S – Usingizi

Usingizi wa kutosha ni muhimu sana huupa ubongo muda wa kupumzika na kuhifadhi kumbukumbu. Lenga kulala kati ya saa 7 na 9 kila usiku.

W – Maji

Mwili wa binadamu una takribani asilimia 60 ya maji, na hata upungufu mdogo wa maji mwilini unaweza kukufanya ushindwe kuwa na umakini. Kwa hiyo, weka maji karibu na unywe mara kwa mara.

A – Shughuli za mwili

Kusogeza mwili huongeza mtiririko wa damu na oksijeni kwenda kwenye ubongo, jambo linaloweza kukusaidia kufikiria kwa uwazi zaidi. Jaribu kutembea kwa muda mfupi, kukimbia taratibu au kujinyoosha mara kwa mara.

N – Lishe

Lishe bora huupa ubongo virutubisho muhimu. Kula vyakula vya asili na vyenye virutubisho badala ya vyakula vilivyosindikwa sana. Choline ni kirutubisho muhimu kwa afya ya ubongo, hivyo kula vyakula vyenye choline kwa wingi kama mayai, samaki na karanga kunaweza kusaidia kuongeza umakini.

S – Msongo wa mawazo

Msongo wa mawazo wa muda mrefu husababisha mwili kutoa kiasi kikubwa cha cortisol, homoni inayosaidia kudhibiti mwitikio wa mwili unapokuwa na msongo.

Hali hii inaweza kufanya mawazo yako yasiwe wazi. Tafuta njia za kupunguza msongo wa mawazo, kama vile mazoezi ya kupumua, mindfulness na kufanya shughuli unazozipenda.