Moja kwa moja, Watu watano wauawa huku Urusi ikianzisha mashambulizi mapya ya anga kote nchini Ukraine
Raia wa tano wa Ukraine ameripotiwa kuuawa katika mashambulizi ya Urusi yaliyofanyika usiku kucha.
Muhtasari
Kamanda wa jeshi la Iran atangaza zawadi ya "kuua au kuwakamata" wanajeshi wa Marekani
Arsenal vs Manchester City
Urusi yazindua wimbi la mashambulizi dhidi ya Ukraine huku Kyiv ikishambulia kampuni kubwa karibu na Moscow
Idadi ya waliofariki katika ajali ya boti nchini Zimbabwe yapanda hadi 68 huku miili zaidi ikipatikana
Kamanda wa CENTCOM ahitimisha ziara yake Mashariki ya Kati baada ya kutembelea nchi sita na meli moja
Iran yataka kutumwa kwa timu ya wataalamu kufuatia Qatar kukanusha madai ya "kushikiliwa" kwa marubani wake
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu: Mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon yanaongeza hatari ya vita kusambaa
Waokoaji wanawatafuta manusura wa tetemeko kubwa la ardhi nchini Indonesia
Qatar yakanusha kuwakamata marubani watatu wa Iran baada ya kutungua ndege za kivita
Moja kwa moja
Abdalla Seif Dzungu
Kamanda wa jeshi la Iran atangaza zawadi ya dola 30,000 hadi 60,000 kwa ajili ya "kuua au kuwakamata" wanajeshi wa Marekani
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Hatami
Amir Hatami,
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema kuwa jeshi hilo
limeandaa mpango mpya ambapo yeyote atakayemuua au kumkamata na kumkabidhi
askari wa Marekani atapokea "zawadi yenye thamani ya dola 30,000 au tomans
bilioni tano."
Amesema kuwa
kiasi cha zawadi kwa ajili ya wanawake kitakuwa mara mbili ya kile cha wanaume,
yaani dola 60,000.
Alitoa kauli
hizo katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Waandishi wa Habari iliyofanyika
katika Shirika la Itikadi ya Kisiasa la Jeshi.
Kamanda huyo
wa jeshi la Iran aliendelea kusema, "Silaha ya mtu yeyote atakayefanikiwa
kumuua mvamizi wa Marekani itanunuliwa kwa bei mara mbili ya thamani yake na
atapewa silaha mpya.
Silaha ya
mtu huyo pia itawekwa katika makumbusho yaliyopangwa maalum."
Arsenal vs Manchester City
Chanzo cha picha, Getty Images
Mabingwa wa
ligi ya England Arsenal wanajibwaga uwanjani hii leo dhidi ya Manchester City katika kombe la Community Shield
Wachezaji wa Arsenal watakaoanza:
Raya, White, Mosquera, Gabriel, Calafiori, Lewis-Skelly, Guimaraes, Odegaard,
Madueke, Tzolis, Havertz
Enzo Maresca
amemuweka Elliot Anderson katika safu ya kati huku Erling Haaland akiongoza
safu ya mashambulizi. Jack Grealish ametajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wa
akiba wa City.
Wachezaji wa Manchester
City wanaoanza XI: Donnarumma, Khusanov, Dias, Guardiol, O'Reilly, Kovacic,
Anderson, Semenyo, Foden, Doku, Haaland
Chanzo cha picha, Getty Images
Tanzania yapinga kutuma watu kuingilia uchaguzi wa Zambia
Serikali ya Tanzania
imepinga madai yaliotolewa na mgombea wa urais wa Zambia Brian Mandubile kwamba
Tanzania ilituma watu kwenda kuingilia
uchaguzi mkuu wa taifa hilo uliofanyika hivi karibuni.
Mgombea huyo wa urais wa Zambia, aliwaonya Watanzania
anaodai wamehusika katika siasa za Zambia, akiwataka kuondoka nchini humo.
Lakini katika
taarifa iliotumwa katika mitandao ya kijamii, Tanzania imejibu kupitia barua
kwa ubalozi wake nchini Zambia ikitaka maelezo ya kina kuhusu sababu za mgombea
huyo kuzua madai kama hayo.
Tanzania
imesena inachukulia tuhuma hizo kwa uzito na kwamba inawahakikishia Watanzania na jamii ya kimataifa kwamba
haijatuma mtu yeyote Zambia kuvuruga uchaguzi wa taifa hilo.
‘’Kama
ilivyo nchi zingine za Jumuiya ya Maendeleo , kusini mwa Afrika SADC, Tanzania inao
uwakilishi wa waangalizi wa uchaguzi nchini Zambia wanaofanya kazi kulingana na
miongozo ya waangalizi wa uchaguzi wa SADC sambamba na waangalizi wengine
waliopo Zambia na sio kuingilia Uchaguzi kama ilivyotuhumiwa na bwana Mandubile’’.
Bwana
Mandubile alinukuliwa akisema kwamba
Zambia si
Tanzania na kwamba mbinu za kisiasa zinazoweza kufanya kazi Tanzania haziwezi
kutumika nchini Zambia.
Alisema: "Ndugu
zangu Watanzania ambao mmekodiwa, tafadhali tokeni katika nchi yetu."
Alisema
chama tawala cha UPND hakiwezi kushinda uchaguzi huo na kukituhumu kutumia kile
alichokiita "mbinu ya Tanzania" ili kupata ushindi.
"UPND
hawawezi kushinda uchaguzi huu, hakuna muujiza. Sasa wameamua kutumia mbinu ya
Tanzania. Zambia si Tanzania. Hii ni Zambia. Wale wanaofikiri wanaweza kuingiza
katika nchi hii mbinu inayofanya kazi Tanzania, hawawezi kufanikiwa
kamwe."
Kauli ya
Mundubile imekuja wakati mchakato wa kuhesabu kura katika uchaguzi wa Zambia
ukiendelea chini ya ulinzi mkali, baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zambia
kusimamisha kwa muda zoezi hilo kufuatia taarifa za mashambulizi dhidi ya
maafisa wa uchaguzi na kuibwa kwa kura.
Tume hiyo
imesisitiza kuwa wagombea hawapaswi kujitangaza washindi kabla ya matokeo rasmi
kutangazwa.
Mundubile,
ambaye ni mmoja wa wagombea wakuu wa upinzani, tayari amejitangaza mshindi wa
uchaguzi huo, licha ya Tume ya Uchaguzi ya Zambia kutokuwa imetangaza matokeo
ya mwisho.
Jeshi la Israel limetangaza kuuawa kwa kamanda mkuu wa Kikosi cha Hezbollah
Jeshi la
Israel limetangaza kuuawa kwa Abu Hassan Alaa, kamanda mkuu wa Kikosi cha Badr
cha Hezbollah.
Katika
ujumbe kwenye mtandao wa X, jeshi la Israel lilisema kuwa lilimuua kamanda huyo
mkuu ikiwa ni jibu kwa vitendo vya Hezbollah dhidi ya vikosi vya jeshi la
Israel katika eneo la usalama.
Ujumbe wa
jeshi la Israel unasema: "Hassan Alaa alishiriki katika kupanga na
kutekeleza mashambulizi mengi dhidi ya vikosi vya jeshi la Israel vilivyokuwa
vikifanya operesheni katika eneo la usalama, ikiwa ni pamoja na kurusha ndege
zisizo na rubani zilizobeba vilipuzi dhidi ya vikosi vya jeshi la Israel kusini
mwa Lebanon."
Habari za hivi punde, Urusi yazindua wimbi la mashambulizi dhidi ya Ukraine huku Kyiv ikishambulia kampuni kubwa karibu na Moscow
Chanzo cha picha, Reuters
Raia wa tano
wa Ukraine ameripotiwa kuuawa katika mashambulizi ya Urusi yaliyofanyika usiku
kucha.
Meya wa
Kryvyi Rih anasema mwanamume mwenye umri wa miaka 44, ambaye awali aliripotiwa
kupotea, amepatikana akiwa amefariki dunia chini ya vifusi.
Mtu mwingine
aliuawa na wafanyakazi 14 wa kiwanda cha chuma walijeruhiwa. Urusi inasema eneo
hilo lilikuwa likitengeneza vipuri vya silaha.
Watu wawili
wenye umri wa miaka ya 60 walifariki dunia baada ya nyumba kuharibiwa huko
Zaporizhzhia.
Idara za
huduma za dharura zinasema moto uliokuwa ukiwaka katika soko moja jijini Kyiv
umezimwa, baada ya soko hilo kushambuliwa usiku kucha.
Rais wa
Ukraine Volodymyr Zelensky anasema watu sita wamejeruhiwa jijini humo kufuatia
mawimbi manne ya mashambulizi ya anga yaliyofanyika usiku na asubuhi ya leo.
Rais alitaja
kifo cha tano kilichotokea jana jioni huko Sumy, ambapo gari moja
lilishambuliwa.
Urusi
inasema mashambulizi yake dhidi ya Kyiv usiku uliopita yalilenga kituo
kilichokuwa kikizalisha vipuri vya makombora ya Ukraine aina ya Flamingo,
pamoja na kiwanda kilichokuwa kikizalisha vipuri vya ndege zisizo na rubani
(drones).
Wizara ya
Ulinzi ya Urusi inasema kuwa katika eneo la Poltava, ilishambulia kiwanda cha
kusafisha mafuta cha Kremenchuk, ambacho inasema kinasambaza mafuta kwa jeshi
la Ukraine.
Urusi
inasema ilishambulia meli ya mizigo karibu na Odesa, ikidai kuwa ilikuwa imebeba
vifaa vya kijeshi.
Chanzo cha picha, Reuters
Idadi ya waliofariki katika ajali ya boti nchini Zimbabwe yapanda hadi 68 huku miili zaidi ikipatikana
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Mtu anayesaidia kubeba jeneza anasimama karibu na majeneza wakati wa ibada ya ukumbusho kwa wahanga wa kivuko cha abiria cha Shirika la Maendeleo ya Miundombinu Vijijini (RIDA) kilichopinduka katika Ziwa Kariba, katika Uwanja wa Nyamhunga mjini Kariba, Zimbabwe, tarehe 13 Agosti 2026. Boti hiyo ilipinduka siku ya Jumanne na kusababisha vifo vya watu kadhaa.
Miili
mingine 22 imepatikana kufuatia ajali ya boti katika ziwa nchini Zimbabwe,
polisi walisema Jumamosi, na hivyo kufanya idadi ya waliofariki kufikia 68.
Boti hiyo
ilipinduka tarehe 11 Agosti katika Ziwa Kariba.
Uchunguzi
unaonyesha kuwa boti hiyo ilikuwa imebeba watu au mizigo kupita kiasi wakati
ilipopinduka kutokana na upepo mkali.
Jeshi la
Polisi la Zimbabwe lilithibitisha idadi hiyo mpya ya waliofariki kupitia
mitandao ya kijamii.
Kamanda wa CENTCOM ahitimisha ziara yake Mashariki ya Kati baada ya kutembelea nchi sita na meli moja
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Kamanda wa Centcom Admirali Brad Cooper
Kamanda wa
Kamandi Kuu ya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati (CENTCOM) ameondoka
eneo hilo baada ya ziara ya siku 10.
Katika ziara
hiyo, Admirali Brad Cooper alitembelea nchi sita na meli ya kubeba ndege za
kivita ya Jeshi la Wanamaji la Marekani inayofanya kazi katika Bahari ya
Uarabuni.
Wakati wa
ziara yake, alikutana na maafisa wa ngazi ya juu wa kiraia na kijeshi nchini
Bahrain, Iraq, Israel, Jordan, Saudi Arabia, na Falme za Kiarabu, na pia
alikutana na vikosi vya Marekani vilivyopo katika eneo hilo.
Zaidi ya
wanajeshi 50,000 wa Marekani wanatekeleza misheni mbalimbali kote Mashariki ya
Kati.
Kamanda huyo
wa CENTCOM alikutana na mabaharia pamoja na wanajeshi wa 'Marines' waliopo
kwenye meli ya kubeba ndege za kivita ya *Abraham Lincoln* kwa mara ya pili
mwaka huu wakati wa ziara yake.
Awali,
aliitembelea meli hiyo mwezi Februari akiwa na Steve Whittaker, mjumbe maalum
wa Marekani kwa ajili ya misheni za kulinda amani, na Jared Kushner, mkwe wa
Donald Trump.
"Kikosi
cha Mashambulizi cha Lincoln (Lincoln Strike Group) ni timu imara ya Wamarekani
wachapakazi na wenye mafanikio makubwa, ambao wanajivunia sana na kuwa na imani
na mafanikio yao.
Historia itaandika kupelekwa kwa kikosi hiki
kama mojawapo ya vipindi vikali na muhimu zaidi vya operesheni katika nyakati
za kisasa," aliwaambia wanajeshi wote wa meli ya Lincoln wakati wa ziara
yake ya hivi karibuni.
Meli ya
*Abraham Lincoln*, ambayo kituo chake kikuu kiko San Diego, ilitumwa eneo hilo
mwezi Novemba na kuwasili Mashariki ya Kati mwezi Januari.
Kikosi hicho
cha mashambulizi kimefanya maelfu ya safari za ndege za kivita kikiunga mkono
Operesheni Epic Fury, katika vita dhidi ya Iran, na misheni za usalama wa
kikanda, pamoja na hatua inayoendelea ya Marekani ya kuweka kizuizi cha majini
dhidi ya Iran.
Iran yataka kutumwa kwa timu ya wataalamu kufuatia Qatar kukanusha madai ya "kushikiliwa" kwa marubani wake
Chanzo cha picha, Reuters
Mohammad
Bagherzadeh, kamanda wa Kamati ya Kutafuta Watu Waliopotea chini ya Makao Makuu
ya Jeshi, akijibu hatua ya Qatar kukanusha madai ya "kushikiliwa" kwa
marubani wa Iran, aliitaka Doha kuandaa mazingira ya kutumwa kwa timu ya
wataalamu wa Jeshi la Anga la Iran nchini humo.
Alisema kuwa
wataalamu wa Jeshi la Anga la Iran wamekuwa wakisubiri kwa miezi kadhaa kuingia
Qatar na kufanya uchunguzi wa kina kuhusu suala hilo, lakini "vitendo vya
hujuma na ucheleweshaji wa mara kwa mara unaofanywa na mamlaka za Qatar"
vimezuia marubani hao kurejea nchini mwao hadi sasa.
Bw.
Bagherzadeh alisisitiza kuwa badala ya kupinga suala hilo, Qatar inapaswa
kuruhusu timu ya wataalamu na wachunguzi wa Jeshi la Anga kwenda nchini humo.
Kamanda huyo
wa Kamati ya Kutafuta Watu Waliopotea pia alitoa wito kwa Shirika la Msalaba
Mwekundu kufuatilia suala hilo mara moja.
Pia alionya
kuhusu hatima ya raia wanne wa Iran ambao alisema wanashikiliwa nchini Kuwait,
akibainisha kuwa mamlaka za Kuwait bado hazijatoa taarifa kuhusu hali zao.
Majid
Ansari, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, jana alikanusha vikali
madai ya Iran kuhusu "kushikiliwa" kwa marubani watatu wa Iran nchini
Qatar, akisema alishangazwa sana na "kauli za kupotosha katika kipindi
hiki," ikizingatiwa juhudi za kidiplomasia zinazoendelea kupunguza
mivutano katika eneo hilo.
Bw. Ansari
aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba aliwasiliana na marubani hao wa
Iran baada ya anga ya Qatar kukiukwa mwezi Machi na kuthibitisha njia
waliyokuwa wakifuata.
Alisema kuwa
baada ya marubani hao kutojibu ujumbe uliotumwa, Qatar ilichukua hatua za
kulinda eneo lake "kwa mujibu wa sheria za migogoro na matakwa ya sheria
za kimataifa."
Pia alisema
kuwa timu za utafutaji na uokoaji za Qatar zilifanya operesheni ya kuwatafuta
marubani hao na kwamba serikali ya Qatar imewasiliana na Iran ili kukabidhi
mabaki ya mmoja wa marubani hao aliyepatikana.
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu: Mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon yanaongeza hatari ya vita kusambaa
Jumuiya ya
Nchi za Kiarabu ililaani mashambulizi yanayoendelea ya Israel dhidi ya Lebanon,
ikiyataja mashambulizi ya jana—ambayo yalisababisha vifo vya watu 11—kuwa
"ongezeko hatari la uhasama" linaloweza kuharibu juhudi za kusitisha
mapigano na kufikia suluhisho.
Msemaji wa
Jumuiya hiyo alisema kuwa sera na vitendo vya Israel "vinaonyesha wazi nia
ya wavamizi hao ya kuendeleza mgogoro, kukwamisha mazungumzo, na kulazimisha
hali mpya ardhini, jambo ambalo halikubaliki kabisa na linapingwa vikali."
Alionya
kuhusu uwezekano wa migogoro hiyo kusambaa, akisema kuwa iwapo jumuiya ya
kimataifa, na hasa Washington, haitazuia "mashine ya vita" ya Israel
na kuilazimisha nchi hiyo kutii Azimio namba 1701 la Baraza la Usalama la Umoja
wa Mataifa, hali hiyo itaendelea kuzidi kuwa mbaya.
Azimio hilo,
lililopitishwa mwaka 2006, linataka kusitishwa kabisa kwa uhasama kati ya
Israel na Hezbollah na kusisitiza kukomeshwa mara moja kwa mashambulizi yote ya
Hezbollah pamoja na operesheni zote za kijeshi za mashambulizi zinazofanywa na
Israel.
Waokoaji wanawatafuta manusura wa tetemeko kubwa la ardhi nchini Indonesia
Chanzo cha picha, Reuters
Vikosi vya
uokoaji nchini Indonesia vimekuwa vikiwatafuta manusura wa tetemeko kubwa la
ardhi la siku ya Jumamosi ambalo limesababisha vifo vya watu wasiopungua 47.
Tetemeko
hilo lenye ukubwa wa 7.7 katika kipimo cha Richter lilikumba kisiwa cha Flores
muda mfupi kabla ya saa 05:00 asubuhi (saa 22:00 GMT siku ya Ijumaa) na kitovu
chake kilikuwa katika kina cha kilomita 15, kulingana na taarifa ya shirika la
hali ya hewa na jiolojia la Indonesia.
Ripoti za
awali zilionyesha kuwa zaidi ya nyumba 900 na mamia ya majengo mengine
yaliathirika vibaya kutokana na tetemeko hilo pamoja na mitetemo 341
iliyofuata, shirika la kitaifa la usimamizi wa majanga (BNPB) lilisema.
Hata hivyo,
ukubwa kamili wa janga hilo bado haujajulikana, na taarifa za tetemeko la pili
lenye ukubwa wa 6.9 katika upande mwingine wa Indonesia zilitumika kama
ukumbusho wa sababu inayofanya eneo hili kuitwa "Pete ya Moto" (Ring
of Fire).
Mitetemo
kutoka kwa tetemeko hilo kali la Jumamosi iliripotiwa kuhisiwa na wakazi hadi
maeneo ya magharibi katika Wilaya na Jiji la Bima, BNPB ilisema, lakini jimbo
la Manggarai ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi.
Takwimu za
awali zinaonyesha kuwa vifo 24 viliripotiwa huko, huku vifo 17 vikiripotiwa
katika jimbo la Manggarai Mashariki, vitatu katika jimbo la Sikka, na angalau
kifo kimoja katika kila moja ya majimbo ya Ngada, Ende na Manggarai Magharibi.
Angalau watu
wengine wawili walijeruhiwa vibaya na 11 walipata majeraha madogo.
BNPB ilisema
kuwa zaidi ya watu 5,000 bado wako katika vituo vya muda vya kuhifadhi
waathirika na vifurushi 10,500 vya misaada vimepelekwa katika maeneo
yaliyoathirika.
Qatar yakanusha kuwakamata marubani watatu wa Iran baada ya kutungua ndege za kivita
Chanzo cha picha, UK MOD
Iran imetoa
wito wa kuachiwa huru kwa marubani watatu ambao ilisema walitekwa na Qatar
baada ya ndege zake mbili za kivita kupigwa na mifumo ya ulinzi wa anga wakati
wa operesheni ya kijeshi mwanzoni mwa vita kati ya Marekani na Iran.
Katika barua
kwa mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), Brigedia Jenerali
wa Iran Mohammad Bagherzadeh alisema marubani hao - Javad Salehi, Abdul Majid
Dashtian na Imran Behroshian - walikuwa wakishikiliwa mateka kwa miezi sita.
Alisema
mwili wa rubani wa nne, Majid Kazemi, ulikuwa umerejeshwa baada ya kuuawa
katika operesheni hiyo hiyo mnamo tarehe 2 Machi 2026 - siku ya tatu ya vita.
Qatar
"ilikanusha vikali" madai ya Iran na kusema ilikuwa
"imeshangazwa na kauli hizi za kupotosha".
Jenerali
Bagherzadeh alisema marubani hao watatu walitekwa na Qatar baada ya kuruka nje
ya ndege zao wakati wa operesheni ya kivita iliyolenga kambi ya kijeshi ya
Qatar.
Katika barua
hiyo kwa mkuu wa ICRC Mirjana Spoljaric, iliyochapishwa na vyombo vya habari
vya Iran, aliishutumu Qatar kwa kukiuka "haki zisizoweza kuondolewa za
wafungwa hawa, kinyume na sheria na kanuni zote za kimataifa".
Barua hiyo
pia ilidai kuwa marubani hao watatu hawakuruhusiwa kukutana au kuwasiliana na
familia zao.
Msemaji wa
mambo ya nje wa Qatar, Majed Mohammed Al Ansari, alisema mawasiliano yalifanywa
na marubani hao "baada ya kukiuka anga ya Qatar", lakini kwamba
hawakupata majibu.
"Hatua
stahiki zilichukuliwa kulinda eneo letu kwa mujibu wa sheria za
kimataifa," aliongeza katika taarifa kwenye mtandao wa X.
Al Ansari
alisema timu za utafutaji na uokoaji za Qatar "zilitekeleza majukumu yake
kikamilifu katika kutafuta mabaki ya marubani hao".
Alisema
Qatar iliwasiliana na Iran ili "kuratibu makabidhiano ya mabaki ya mmoja
wa marubani hao yaliyopatikana" na kwamba Tehran bado haijajibu mwaliko wa
kupitia maelezo ya operesheni hiyo ya utafutaji na uokoaji.
Natumai hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja