Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tunajua nini kuhusu kikosi cha Marekani cha Delta kilichotumwa Israel?
Msemaji wa Pentagon, Patrick Ryder alisema kuwa vikosi maalum vya Marekani vinavyohusika na kuwakomboa mateka vimewasili Israel.
Ryder aliongeza kuwa na kutumwa kwa shehena ya ndege za Marekani mashariki mwa Mediterania ni "ujumbe wa kuzuia Hezbollah na Iran kutoingilia vita," akibainisha kuwa ndege hizo zina uwezo wa kijasusi, ufuatiliaji na kushambulia. ”
Amesema Washington itaziacha ndege za kivita za F-35 katika eneo hilo, na itaongeza ndege za F-16 na F-15, ili kuifanya Marekani kuwa na machaguo kadhaa.
Kikosi cha Delta
Kikosi cha Delta ni kitengo maalumu cha Jeshi la Marekani kinachoshughulika miongoni mwa kazi nyingi, ni operesheni za kuwakomboa mateka na operesheni za kupambana na magaidi.
Kitengo hiki kilianzishwa mwaka wa 1977 na Kanali Charlie Beckwith, ambaye aliona haja ya kuwa na kikosi maalumu cha mashambulizi ndani ya jeshi, baada ya kufanya kazi na kikosi cha anga cha Uingereza katika miaka ya 1970, kama sehemu ya kubadilishana uzoefu wa kijeshi kati ya Washington na London.
Delta inahusika kupambana na makundi ya kigaidi, upelelezi wa kimkakati na maandalizi ya uendeshaji wa vita, lakini pia inashiriki katika shughuli za uokoaji wa mateka na misheni ya siri na CIA.
Katika kitabu kuhusu Delta Force, Sean Naylor, mwandishi wa jarida la Army Times, alisema kuna takribani askari 1,000 wa Delta Force.
Kulingana na tovuti ya American Special Ops, masharti ya kujiandikisha ni kwamba waombaji lazima wawe na umri wa angalau miaka 21, wawe wanajeshi waliohitimu, na wawe na historia safi na nidhamu.
Operesheni maarufu za Delta
Mojawapo ya operesheni mashuhuri ambayo Kikosi cha Delta kilishiriki mwanzoni mwa kuanzishwa kwake ni 1980, wakati wa jaribio la kuwaokoa mateka wa Kimarekani walioshikiliwa huko Tehran, Iran.
Ingawa operesheni hiyo ilielezwa kufeli, kutokana na hitilafu ya mitambo ya anga, na kusababisha vifo vya Wamarekani nane, ilizingatiwa kuwa ni lipo la kujifunza kwa ajili ya operesheni zijazo.
Kwa mujibu wa tovuti ya "Insider", Julai 1983, Delta Force ilishiriki kuwakomboa wamisionari watano wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na raia wawili wa Marekani, waliokuwa wakishikiliwa mateka na watu wenye silaha kutoka Kusini mwa Sudan. Pia ilishiriki katika Operesheni Desert Storm kuikomboa Kuwait baada ya uvamizi wa Iraq mwaka 1991.
Mwaka 1993, Delta ilifanya operesheni Mogadishu, Somalia kwa lengo la kumkamata kiongozi wa Jeshi la Taifa la Somalia, Jenerali Mohamed Farah Aidid, lakini ilipata pigo kubwa baada ya wapiganaji wake 18 kuuawa na wengine 73 kujeruhiwa.
Kitengo hicho pia kilishiriki katika uvamizi wa Afghanistan mwaka 2001 na Iraq kati ya 2003 na 2011, na kutekeleza operesheni maarufu ya "Red Dawn" ya kumkamata hayati Rais wa Iraq, Saddam Hussein.
Kulingana na tovuti ya Jeshi, kuna operesheni nyingine maarufu ambazo ilishiriki, kama vile kuondoshwa kwa wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani nchini Libya wakati wa shambulio la Benghazi la 2012.
Kukamatwa kwa mfanyabiashara wa dawa za kulevya wa Mexico Joaquin "El Chapo" Guzman, na uvamizi nchini Syria ambao ulisababisha kuuawa kwa kiongozi wa ISIS, Abu Bakr al-Baghdadi.
Ahadi ya Marekani
Rais wa Marekani Joe Biden alisema "analaani mauaji ya raia wa Israel yaliyofanywa na Hamas, ni kitendo kiovu kabisa," na kuahidi uungaji mkono kamili wa Marekani kwa Israel wakati ikijibu mapigo ya Hamas.
Biden alisema atahakikisha Israel inapata kila inachohitaji, ikiwa ni pamoja na silaha za ziada na makombora ya ulinzi wa anga. Alithibitisha Wamarekani kumi na nne waliuawa na wengine wanashikiliwa mateka na Hamas.